loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Katavi tusimwangushe JPM usafiri wa anga

RAIS John Maguful amemaliza ziara yake mkoani Katavi kwa kuzindua safari za ndege za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Mpanda.

Baada ya uzinduzi huo uliofanyika Kiwanja cha Ndege cha Mpanda, Rais alienda Dodoma alikotarajiwa kujiandikisha Daftari la Wapigakura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa. Uzinduzi huo ulikuwa ni kutimizwa kwa ahadi yake ya safari za ndege kuanzishwa Mpanda ili kuwapa wananchi wa Katavi, usafiri wa haraka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi alisema wataanzisha safari za mara moja kwa wiki kati ya Mpanda- Dar es Salaam.

Tunaungana na wana Katavi na wananchi wengine hususani wanaopenda kutumia usafiri wa anga kumpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi huo na ATCL kwa kuutekeleza haraka. Katavi ambao ni mkoa mpya uko pembezoni na kufuatia changamoto ya miundombinu, usafiri wa ndege utaharakisha maendeleo ya wananchi.

Katavi inasifika kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara lakini imekuwa na tatizo la usafirishaji kwa kutegemea barabara chache. Hata usafiri wa reli ni wa kusuasua kutokana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutopeleka mabehewa ya kutosha kubeba shehena hizo.

Ndio maana tumeguswa na hatua ya Rais JPM kuwapunguzia machungu watu wa Katavi na maeneo jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuanzisha usafiri wa ndege.

Ni matarajio yetu usafiri huu wa ndege utakuwa mwanzo wa kujenga Katavi mpya kiuchumi na wananchi watautumia vyema kusafiri haraka. Kwa kupanda ndege, wakazi wa Katavi sasa watakuwa na uhakika wa kufanya shughuli zao kwa ufanisi kwenda sambamba na wengine.

Usafiri huu utakuwa ni nyongeza ya mpango wa serikali kuifungua Katavi kwa kujenga barabara za lami zitakazoiunganisha na mikoa mingine. Kwa wana Katavi, tunasema, wana deni kubwa kwa Rais Magufuli la kufanya kazi kwa juhudi kuzalisha zaidi ili kujenga uchumi wa Taifa hili.

Wafanye hivyo wakijua ndege iliyokuja jana ni zao la fedha za walipa kodi wote wa nchi hii na hivyo ili iendelee kuwahudumia, inabidi ilipiwe.

Na hakuna njia ya mkato ya kuilipia zaidi ya watu kupanda na kufanya safari za kwenda Mpanda na kurudi Dar es Salaam ziwe na tija.

Kwa Rais Magufuli tunasema ahsante tena kwa kuguswa na shida za wananchi wanyonge na kuchukua hatua za haraka kuwasaidia shida zao. Tunaamini baada ya Katavi, hatachoka kusaidia maeneo mengine yenye shida ya usafiri wa haraka wa maji, nchi kavu au angani. Hongera.

HATIMAYE safari za ndege kati ya Tanzania na Kenya zimerejea ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi