loader
Msekwa: Kuna mambo yalinihuzunisha kabla Nyerere hajafa

Msekwa: Kuna mambo yalinihuzunisha kabla Nyerere hajafa

Mwandishi: Watanzania wanaelekea Oktoba 14, kuadhimisha miaka 20 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere, Unakumbuka mambo gani katika maadhimisho haya?

Msekwa: Wakati Mwalimu anaaga Bunge, alisema anaacha madaraka nchi ikiwa na amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa na akija, atafurahi kuona Watanzania wanamuenzi kwa kuyaendeleza mambo hayo. Ikitoke muujiza akarudi, atafurahi kuona ndoto yake ya kuhamishia makao makuu ya Serikali jijini Dodoma aliyoiasisi mwaka 1973, imetekelezwa na Rais John Magufuli.

Hili nalikumbuka na kulifurahia sana maama lilikwamishwa na mambo matatu makubwa; Vita vya Kagera baina ya Tanzania na Uganda, kupanda kwa bei ya mafuta duniani na kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hali iliyosababisha serikali kugharamia uendeshaji wa reli, huduma za ndege, posta na simu ambazo awali ziliendeshwa na jumuiya hiyo.

Yapo mengi sana ambayo Rais Magufuli anayatekeleza likiwamo la kuwataka wajuhumu uchumi kurejesha mali za umma. Nyerere aliwahi kutamka; enzi zile Waziri Mkuu Edward Sokoine ameanzisha vita ya wahujumu uchumi akasema, ‘Hawa tunaowaita wahujumu uchumi, wakikiri na kuwa tayari kurudidsha fedha za umma, tutawasamehe.’

Mwandishi: Unadhani Nyerere alitumia mbinu gani kujenga amani, umoja na mshikamano huo kwa Watanzania?

Msekwa: Kitendo cha Mwalimu Nyerere kuanzisha kambi za vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lililowaunganisha kutoka mikoa, wilaya, makabila na dini mbalibali sambamba na mwingiliano wa vijana katika shule mbalimbali nchini zikiwamo za sekondari wa kabila hili au dini hii wanakwenda wanachanganyika kimasomo katika upande mwingine bila shida, ni mambo aliyoyafanya yaliyojenga , kuchochea na kuimarisha umoja wa kitaifa kwa Watanzania.

Mwandishi: Wewe ulikuwa miongoni mwa viongozi wa mwisho kuzungumza na mwalimu Nyerere akiwa London, Uingereza kwa matibabu. Ni mambo gani ya mwisho uliyozungumza naye?

Msekwa: Kwa kweli ninaweza kusema mimi nilikuwa kiongozi wa mwisho nchini kuzungumza naye kabla hajakata kauli. Nafurahi kwamba mambo aliyoniambia niwafikishe watawala, niliyafikisha na yameendelea kutekelezwa

Mwandishi: Ni mambo gani hasa yanayokusisimua unapokumbuka namna mlivyokutana na Mwalimu katika siku za mwisho mwisho, kabla hajafariki dunia?

Msekwa: Yapo mambo mawili makubwa. La kwanza, ni lile la kumpelekea Nyerere zawadi niliyotumwa na Bunge, lakini nilipofika Butiama nimefurahi, nikakuta Baba wa Taifa anaumwa; yupo nyumbani na anajiandaa kwa safari ya kwenda London Uingereza kwa matibabu. Hilo ni la kwanza. La pili, linalonihuzunisha hadi sasa, ni lile la kumkuta ameruhusiwa kutoka hospitali mjini Londoni Uingereza na Mwalimu Nyerere akaniambia anajiandaa kurudi nyumbani, lakini siku hiyo hiyo, hali yakeikabadilika; ikawa mbaya sana, akarudishwa hospitali na kukata kauli.

Mwandishi: Katika matukio hayo mambo yalikuwaje?

Msekwa: … Baada ya mwalimu kuliaga Bunge kwamba anang’atuka, Bunge liliazimia kumpa zawadi ya vitabu aina ya Encyclopedia Britanica Volume (juzuu) 32. Bunge liliona hii itakuwa zawadi maalumu maana kutokana na bei yake, vilikuwa havipatikani kwa urahisi madukani maana maduka yalikuwa hayavileti kutokana na ugumu wa bei yake; hivyo yakawa hayaviagizi.

Kwa msingi huo, nikatumwa niviagize kutoka London. Huko London wakasema vimekwisha, lakini baada ya kujua kuwa ni kwa ajili ya Mwalimu Nyerere, wakasema watachapisha toleo maalumu. Ilipita kama miaka mitatu, nikatumwa kumpelekea hiyo zawadi Butiama.” “Sasa nimepeleka zawadi, nikakuta Mwalimu ninayempelekea zawadi anaumwa mkanda wa jeshi; madonda yapo tumboni.

Akanieleza namna anavyopata tabu. Mwalimu akaniambia Pio (Pius), wiki ijayo nitakwenda hospitali nikatibiwe. Nikamkabidhi zawadi hiyo. Ulikuwa mwezi Agosti 1999. Kwa hiyo ilinihuzununisha sana mtu unayempelkea zawadi, unakuta ana hali mbaya na anakwenda nje kwa matibabu. (anatulia kwa huzuni)

Mwandishi: Tukio la pili lilikuwaje?

Msekwa: Hili la pili lenyewe, ni pale mwezi Oktoba 1999. Tulikuwa na mkutano wa maspika wa bunge huko West Indies ambako kwenda na kurudi lazima upite London. Siku ya kurudi nikapita hapo kumjuliana hali baada ya balozi kunifanyia mpango nimuone. Nikamkuta akiwa na mkewe Mama Maria Nyerere. Nikafurahi kumuona amepata nafuu na akaniambia, ‘Pio (Pius) ninajiandaa kurudi nyumbani wiki ijayo…” Siku hiyo, ndiyo nilikuwa naondoka Uingereza kwa ndege ya usiku kurudi Tanzania.

Nlipofika, niliwajulisha viongozi wa juu akiwamo Waziri Mkuu, Frederck Sumaye (wakati huo) kuhusu maendeleo ya kiafya ya Mwalimu Nyerere na kwamba, mambo yanakwenda vizuri na anajiandaa kurejea Tanzania. Nao wakafurahi sana. Sasa, kesho yake baada ya kufika, waziri mkuu akaniita na kuniuliza wewe si ulisema Mwalimu anaendelea vizuri na anarudi nyumbani wiki ijayo; mbona balozi anasema amerudishwa hospitali na amekata kauli?

Nikamwambia hayo ni mapenzi ya Mungu; ndivyo nilivyomkuta hata balozi aliniambia hivyo hivyo na hiyo ilikuwa Septemba 25, 1999… Kwa kweli, hiyo iliumiza na kunitia huzuni sana. Fikiria unamkuta mgonjwa hali ni nzuri anajiandaa kurudi, unaleta taarifa nyumbani wanafurahi, ghafla unaambiwa amekata kauli, wewe utajisikiaje, lakini nafurahi aliyoniambia niyafikishe kwa watawala, niliyafikisha.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d48ff19f11a17a905bd6257e13e83f26.jpg

NDUGU msomaji katika makala yangu ya leo nimeyakumbuka ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi