loader
Picha

Wanafunzi 9 waliokufa maji Morogoro watajwa

WANAFUNZI tisa ni miongoni mwa watu 12 waliofariki dunia kutokana kusombwa na maji ya mvua zilizonyesha maeneo ya wilaya za Mkoa wa Morogoro na wengine baada ya kuzidiwa na maji wakiwa mtoni wanaogelea.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wilboad Mutafungwa alisema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya athri za mvua zilizonyesha mwanzoni mwa mwezi huu mkoani Morogoro.

Kati ya wanafunzi hao, watano ni kutoka Shule ya Msingi Nyachiro Kata ya Kibongwa, Tarafa ya Matombo, wawili wa Shule ya Msingi Kibwaya, Kata na Tarafa ya Mkuyuni na wawili Kijiji cha Mtego wa Simba katika Kata ya Mikese, zote ni za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Kamanda Mutafungwa alisema wanafunzi watano kutoka shule ya Nyachiro walifariki dunia Oktoba 12, mwaka huu saa 12: 30 jioni baada ya kuzama katika mto Mvuha. Aliwataja wanafunzi hao ni Neema Rajab (10), Latifa Khalid (9) wote wa darasa la pili, Munira Khalid (11) mwanafunzi wa darasa la tatu, Omary Khalid (14) ambao miili yao ilipatikana huku Zanisha Adam (9) wa darasa la pili mwili wake haujapatikana na juhudi za kuutafuta kwa kushirikiana na wananchi zinaendelea.

Alisema katika ajali hiyo, mwanafunzi Said Rajabu (11) wa darasa la tatu alikimbia baada ya kuona maji yanazidi na alianguka na kuumia usoni na mkononi na anaendelea na matibabu katika Zahanati ya Kibongwa. Alisema katika ajali nyingine, Oktoba 11, mwaka huu saa nane mchana katika kitongoji cha Kisemo, Kijiji cha Kibwaya wanafunzi wawili walifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye dimbwi la maji walilokuwa wakiogelea.

Aliwataja wanafunzi hao ni Rajab Issa (11) mwanafunzi wa darasa la tatu na mwenzake Shabani Msimbe (15), wote wakiwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibwaya. Kamanda huyo alitaja tukio jingine la Oktoba 14, mwaka huu saa sita mchana katika Kitongoji cha Ulundo, Kijiji cha Mtego wa Simba, kata na Tarafa ya Mikese, Karimu Athumani (13) na Hussein Hassan (14), mwanafunzi wa darasa la sita mkazi wa Ulundo walifariki dunia kwa kuzidiwa na maji wakiwa mtoni wanaogelea.

Alisema miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na daktari wa Zahanati ya Mikese na kubaini sababu ya kifo ni kunywa maji kwa wingi na kukosa hewa na miili yao imekabidhiwa kwa familia kwa taratibu za mazishi. Mbali na wanafunzi hao, mkazi wa Kijiji cha Kipera wilayani Mvomero, Yassini Ally (50) alifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye dimbwi la maji akiogelea maji yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Aidha, tukio jingine lililotokea Oktoba 13, mwaka huu Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro, Jabibu Mzungu Chris (40) mvuvi mkazi wa Manzese alifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye Bwawa la Mindu. Chris alikuwa katika shughuli za uvuvi kutokana na mtumbwi wake kupoteza uelekeo kisha kutumbukia majini na mwili wake umehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi.

Oktoba 14, mwaka huu, saa 3 asubuhi katika bwawa la kuhifadhia uchafu utokanao na miwa (Morasisi) la Kiwanda cha Sukari Kilombero (K2), Kata ya Ruaha wilayani Kilosa, wakulima wakazi wa Ruaha, Ramadhani Mkuku (28) na Frank Mdegera (25) walikutwa wamekufa ndani ya bwawa hilo baada ya kuzamia wakijaribu kuchota Morasisi. Kutokana na matukio hayo, Kamanda Mutafungwa amewataka wananchi kuwa na tahadhari na kuwa na uangalizi wa kutosha wa watoto wao ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Nicodemus Mwangela ametoa siku saba ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi