loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania yavuna Barrick

JITIHADA za Rais John Magufuli za kuhakikisha rasilimali za Tanzania zinalindwa, zimeanza kuzaa matunda baada ya serikali na Kampuni ya Barrick Gold Corporation kuingia ubia na kuanzisha kampuni mpya ya Twiga Mining Co. Ltd inayochukua nafasi ya Kampuni ya Acacia.

Kampuni ya Twiga iliyosajiliwa nchini na makao yake makuu yatakuwa Mwanza, Serikali ya Tanzania itamiliki asilimia 16 na Barrick Gold Corporation itakuwa na asilimia 84. Sasa ndio itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa inasimamiwa na Acacia ambayo ni Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara na itaendesha shughuli zake zote nchini.

Hatua hiyo, imekuja baada ya Kampuni ya Barrick kuizika rasmi Acacia na kufunga ofisi zake zilizokuwepo jijini London, na kufuta kesi na madeni yote ambayo kampuni hiyo ya Acacia iliyafungua dhidi ya serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema hatua hiyo imeingiza Tanzania katika historia mpya ya ukombozi wa kiuchumi.

“Katika ubia huu wa Kampuni ya Twiga, Barrick Gold Corporation inamiliki hisa asilimia 84 na serikali asilimia 16 huku katika kila mgodi kati ya hiyo mitatu serikali ikimiliki asilimia 16,” alieleza Kabudi ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais katika majadiliano na kampuni mbalimbali za madini.

Alisema kuanzishwa kwa kampuni hiyo mpya sasa kumefuta migogoro yeyote iliyokuwepo baina ya serikali na Acacia ambayo hisa zake za asilimia 63.9 zote zilinunuliwa na hivyo kumilikiwa na Barrick Gold Corporation.

Alieleza kuwa pamoja na kufuta migogoro hiyo, pia wamekubaliana kuwa Barrick itailipa Tanzania kiasi cha dola za Marekani milioni 300 kwa ajili malipo ya kodi zote zilizokuwa haijalipwa na migogoro mingine.

Alisema matunda ya mafanikio hayo yalianza kuonekana baada ya kampuni ya Barrick kununuliwa rasmi na Kampuni ya Rand Gold Resources ya Afrika Kusini, Januari mwaka huu ambayo kupitia mmiliki wake ambaye sasa ndiye Rais wa Barrick Gold Corporation, Mark Bristow iliazimia kumaliza mgogoro baina ya Acacia na serikali.

Profesa Kabudi alieleza kuwa katika kuonesha nia ya kufikia muafaka juu ya migogoro iliyokuwa inaendelea baina ya serikali na kampuni hiyo ya Acacia, uongozi mpya wa Barrick uliamua kuifuta kampuni ya Acacia na kufunga ofisi zake zilizopo jijini London.

Alisema baada ya hatua hiyo chini ya uenyekiti wake na Rais wa Barrick, Bristow kumekuwepo na mazungumzo kadhaa juu ya namna ya kufikia muafaka kamili kuhusu uendeshaji wa migodi hiyo mitatu na ndipo walipokubaliana kuanzisha kampuni hiyo ya Twiga.

“Hata hivyo, kuna nyaraka takribani tisa tumeziwasilisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili zipitiwe na hadi kufikia Novemba 15, mwaka huu mapitio hayo yatakuwa yamekamilika na nyaraka nyingine zitatiwa saini,” alisisitiza Profesa Kabudi.

Alieleza kuwa tangu safari ya Rais Magufuli aliyoianza ya kupigania rasilimali za Tanzania ianze ikiwamo mapambano yake dhidi ya wizi uliokuwa unafanywa na Acacia, kumekuwepo na watu waliobeza jitihada hizo na kuikatisha tamaa serikali.

“Wapo waliodai kuwa hatutashinda, wapo waliodai tutafunguliwa mashtaka na Acacia na kweli walitufungulia kesi London na tulikuwa tunadaiwa matrilioni ya shilingi lakini leo kwa hatua hii tumeshinda, Dk Magufuli alikuwa na hoja ndio maana tumefikia hapa,” alisisitiza. Kwa upande wake, Rais wa Barrick alitangaza rasmi kuwa sasa Kampuni ya Barrick Gold Corporation imerejea tena kufanya kazi Tanzania.

Alielezea namna Barrick ilivyopitia changamoto mbalimbali ikiwamo mgogoro uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na Acacia, lakini kutokana na njia muafaka zilizotumika za mazungumzo leo (jana), pande zote zimesherehekea ushindi.

Alitaja makubaliano waliyofikia kuwa ni pamoja na kila upande kunufaika kwa asilimia 50 kwa 50 na rasilimali hiyo ya madini na kuwepo kwa ushirikiano na ubia wa kweli kwa pande zote mbili jambo ambalo limefanikiwa.

“Tangu miaka ya 90 Tanzania imekuwa mstari wa mbele kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye madini na leo naamini tukiangalia historia ya nyuma jambo hili linapaswa kupongezwa si tu Tanzania bali Afrika nzima,” alisema Bristow.

Alisema kampuni ya Barrick iko tayari kufanya kazi na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wananufaika na kile kinachozaliwa na migodi hiyo mitatu mikubwa nchini.

Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Acacia ziliingia katika mgogoro Machi, mwaka 2017, baada ya kuzuiliwa kwa makontena 256 ya mchanga wa dhahabu (makinikia) kwenye bandari ya Dar es Salaam.

Makontena hayo yalizuiwa baada ya kubainika kuwa Acacia haitoi taarifa sahihi ya kiwango cha madini kilichopo katika makinikia hivyo kulipa tozo zisizo sahihi kwa karibu miongo miwili jambo lililopingwa na kampuni hiyo.

Baada ya mgogoro huo, Rais John Magufuli aliunda kamati mbili za kuchunguza suala hilo ikiwemo kutafuta muafaka juu ya mgogoro huo ambapo sasa matunda yake yameanza kuonekana.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi