loader
Makonda awakalia kooni wakandarasi wenye miradi inayosuasua

Makonda awakalia kooni wakandarasi wenye miradi inayosuasua

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku tano kwa wakandarasi wote wa mkoa huo wenye miradi inayosuasua kuhakikisha wanatekeleza kwa sababu inatia doa utendaji kazi wa viongozi wa mkoa.

Amezitaka bodi zote za zabuni zifanye kazi kwa weledi na kuacha kupokea rushwa kwa kuwa inakwamisha miradi. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makonda alisema ametoa siku tano kuanzia jana kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ndani ya mkoa huo kuhakikisha wanakuwa kwenye maeneo ya kazi na kutekeleza zabuni zao, vinginevyo hatasita kuwachukulia hatua hata kama miradi hiyo zabuni zake zilitolewa na wizara.

“Ninawapa siku tano wakandarasi wote wenye miradi inayosuasua mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wako ‘site’ na wanaendelea na kazi, kwa sababu tumebaini baadhi yao walidanganya kwenye makaratasi waliandika wana uwezo na ni daraja la kwana ila ukweli hawana uwezo huo na fedha pia hawana, nitashughulika nao hata kama zabuni hazikutolewa na ofisi ya mkoa,” alisema Makonda.

Kauli ya Makonda imekuja ikiwa ni mwendelezo wa hatua kadhaa alizoanza kuzichukua baada ya Rais John Magufuli kukerwa na kutoridhishwa kwa utekelezwaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo ya mkoani humo Septemba mwaka huu, na kutoa maagizo kwa viongozi wa mkoa huo. Septemba 16, mwaka huu, Rais Magufuli alifungua kiwanda cha kutengeneza mabomba na pia kutembelea Mradi wa Upanuzi wa Kiwanja cha Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) kisha alifanya ziara ya kushtukiza kwenye machinjio ya Vingunguti ambako alioneshwa kukerwa na kusuasua kwa utelekezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha, Rais Magufuli alihoji utendaji kazi wa viongozi wa mkoa huo na katika kutekeleza maagizo ya kiongozi mkubwa wa nchi, Makonda alianza kuchukua hatua kwa kutangaza kufanya kazi kwenye maeneo ya miradi na sasa amehamia kwa wakandarasi wa miradi inayosuasua kwa kuagiza wawe kwenye maeneo yao kuanzia jana. Makonda alisema kusuasua pia kwa baadhi ya miradi hiyo ya maendeleo kumesababishwa na baadhi ya viongozi wa bodi za zabuni kutoa zabuni hizo kwa njia ya rushwa huku wakifahamu wazi kwamba wakandarasi wanaowapa kazi hawana uwezo wa kifedha na vifaa.

“Tumebaini kuwa baadhi ya wakandarasi wamedanganya na hili limefanyika kwa ushirikiano na baadhi ya bodi za zabuni ambazo wamepokea rushwa na kutoa zabuni kwa wakandarasi wanaofahamu wazi kuwa hawana uwezo wa kutekeleza kazi husika, na mimi nasema nitawafukuza na sitasita kuvunja mikataba yao,” alisema Makonda.

Akitoa mfano, alisema mradi kama wa Maboresho ya Mto Ng’ombe wilayani Kinondoni, unaogharimu Sh bilioni 32 ukiwa na urefu wa kilometa 7.5, ambao haujaanza kutekelezwa ilhali mkataba ulishasainiwa Juni 16, mwaka huu.

“Mfano mradi huu viongozi wa wilaya wanadanganya kuwa mkandarasi yupo site anaendelea na kazi lakini ukweli hakuna mkandarasi eneo la kazi, na miradi mingine kama ule wa Hospitali ya Kivule,” alisema.

Mbali na Rais Magufuli kukerwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo, pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amechukizwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka watendaji wa mkoa kubadili kazi ya utendaji kazi wao. Katika hatua nyingine, Makonda ametangaza kamati maalumu ya watu 14 ya kuratibu matibabu ya watoto 500 wa ugonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kupitia mpango wa mkuu wa mkoa.

Kamati hiyo itaongozwa na Mtendaji Mkuu mstaafu wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei akiwa na wajumbe wengine 13 ambao wataratibu upatikanaji wa Sh bilioni moja kwa ajili ya matibabu ya watoto hao 500. Makonda alisema katika kuelekea mwisho wa mwaka ameamua kuandaa kamati hiyo ili kusaidia watoto hao wenye mahitaji ya tiba ili nao wapone na kuendelea na maisha yao.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c31e576d5df6c7037a1e8409f2253942.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi