loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Pwani kuwa na kiwanda cha mabasi

Mkoa wa Pwani unajiandaa kuwa na kiwanda cha mwekezaji Mtanzania cha kuunganisha mabodi ya mabasi.

Mkuu wa Mkoa huo, mhandisi Evarist Ndikilo amesema mjini Kibaha kuwa kiwanda cha BM Motors Company Limited kilichopo Zegereni Kibaha kinasubiri kupata namba ya chesesi ili kuanza kazi hiyo.

“Yeye (Jonas Nyagawa) ni mmiliki wa mabasi, amechoka kununua mabasi nje ya nchi sasa ambacho kinakosekana ni kuwa na ile chesesi namba,na chesesi namba ikipatikana maana yake ni kwamba ataanza kuunganisha mabasi hapa hapa Tanzania”amesema.

Ndikilo amesema, mkoa huo umetekeleza kwa mafanikio ajenda ya Serikali ya kuiwezesha nchi kuwa na uchumi wa kati kupita viwanda ambavyo hadi sasa vimetoa ajira 60,000 mkoani humo zikiwemo 20,000 za kudumu.

Kwa mujibu wa Ndikilo viwanda 1,192 kwenye mkoa huo vikiwemo vikubwa, vya kati, vidogo na vidogo sana vimeongeza mapato ya Serikali na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa zikiwemo zilizokuwa zikiagizwa nje ya nchi.

Ameyasema hayo kabla ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda kufunga maonesho ya pili ya viwanda mkoa wa Pwani yaliyoshirikisha viwanda 329 vikiwemo 41 vikubwa na vya kati, 102 vidogo, taasisi wezeshi 17, benki tano, na wajasiriamali 56.

Amesema chimbuko la maonesho hayo ni malalamiko ya wenye viwanda kukosa soko la bidhaa kwa sababu mbalimbali ukiwemo ushindani na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

“Kutokana na athari ya masoko baadhi ya viwanda vimekuwa vikipunguza uzalishaji na vingine kufungwa. Hii ni ishara mbaya kwa sababu inaweza kuua viwanda vyetu lakini pia kuhatarisha ajira za watu wetu. Hiyo haikuwa ishar nzuri kwa maendeleo ya sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji katika mkoa wetu na hata kwa nchi kwa ujumla”amesema Ndikilo.

Amesema mkoa pia ulianzisha maonesho hayo kwa kuwa baadhi ya bidhaa zilikuwa hazifahamiki hivyo mkoa huo na wadau wakabuni wiki ya maonesho ya viwanda.

“Maonyesho haya yametangaza mafanikio tuliyoyapata kama mkoa na taifa katika ujenzi wa viwanda. Ni imani yetu kupitia maonyesho haya umma wa wana Pwani na Watanzania kwa ujumla wamepata fursa ya kuona bidhaa zinazopatikana hapa Pwani na mikoa jirani”amesema Ndikilo.

Amesema watu 10,000 wametembelea maonesho ya mwaka huu na yatafanyika kila mwaka.

SERIKALI imetumia Sh Bilioni 15 kwa ajili mikopo ya pembejeo ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo, Kibaha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi