loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga vs Pyramids: Ni kufa au kupona Kirumba

WAWAKILISHI pekee nchini kwenye michuano ya kimataifa, Yanga, wanatarajiwa kutoana jasho dhidi ya Pyramids ya Misri katika mchezo wa ply-off kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Kombe la Shirikisho Afrika katika mchezo utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Yanga awali ilishiriki katika michuano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa wa Afrika, lakini baada ya kutolewa na Zesco ya Zambia, ikaangukia katika Kombe la Shirikisho na inacheza mchezo huo wa mchujo ili kusaka kucheza hatua ya makundi.

Timu itakayopata ushindi wa jumla katika mechi mbili za nyumbani na ugeni, basi itakuwa imekata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu kwa kila upande kwa kuwa kila timu inahitaji matokeo chanya hususani kwa Yanga wanahitaji zaidi ushindi wa mabao mengi kumaliza mapema mechi kabla ya kujipanga kwa mchezo wa marudiano unaotarajiwa kupigwa Novemba 2 nchini Misri ili kutinga hatua ya makundi.

Ushindi kwa Yanga ni muhimu sana hasa ukizingatia kuwa Tanzania licha ya kuingiza timu nne katika mashindano mawili ya Afrika (Ligi ya Mabingwa na yale ya Kombe la Shirikisho), lakini imebaki peke yake baada ya Simba, Azam na KMC kutolewa.

ZAWADI NONO

Pamoja na Yanga kuangukia katika mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambayo ni ya pili ukilinganisha na yale ya Ligi ya Mabingwa, bado zawadi zake ni nono endapo watafanya vizuri. Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lilisema kuwa limetenga kiasi cha dola za Marekani milioni 14.2 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 32), ambazo zitagawanywa kwa timu nane bora ambazo zitafanikiwa kutinga hatua ya makundi.

Caf inaendelea kueleza kuwa endapo timu itafanikiwa kutinga hatua ya mtoano kutoka katika robo fainali, ambayo ni hatua ya makundi, nchi hiyo itaondoka na kitita cha dola za Marekani 800,000 (sawa na Sh bilioni 1.8).

USHINDI MUHIMU

Aidha, wanahitaji kupata matokeo chanya ili kujihakikishia kutinga hatua ya makundi na kunyakua kitita hicho cha fedha, lakini hilo halitawezekana kama hawatapambana kufa au kupona. Yanga sio tu inahitaji ushindi, bali inatakiwa kupata ushindi mnono ili kujiweka vizuri kupata ushindi wa jumla watakaporudiana ugenini Misri.

MAANDALIZI YANGA

Kila timu inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali ya ushindi baada ya kutoka kushinda kwenye michezo yao ya ligi za nyumbani wakati wenyeji Yanga wenyewe walipata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Mbao ya Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Ligi ya ndani wenyeji Yanga walitoka kuvuna ushindi mbele ya Mbao kwa bao 1-0 mchezo wa muendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye uwanja huohuo wanaotarajiwa kuutumia kesho.

Matokeo yanayowafanya kushika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi nne, huku wakiwa na balaa la kuanza ligi hiyo kwa kusuasua. Aidha, wapinzani wao Pyramids nao walitoka kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya El Entag El Harby kwenye mchezo wa Ligi Kuu Misri uliopigwa Uwanja wa Al Salaam. Matokeo ambayo yanawaweka kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na hazina ya pointi 11. Kwa ujumla michezo hiyo ilikuwa ni maandalizi ya mwisho kwa timu zote kabla ya kukutana katika mpambano wa kesho wa mchujo ili kutinga hatua ya makundi.

UGUMU WA MCHEZO

Mchezo huo utakuwa mgumu lakini Yanga kama watajipanga vizuri wanaweza kushinda, lazima wapambane na wachezaji wake wajitume mwanzo mwisho. Pyramids sio timu maarufu sana Misri, lakini ile tu kumaliza katika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya nchi hiyo msimu uliopita, kunatosha kabisa kuichukulia timu kwa umakini mkubwa, kwani sio timu ya kuibeza. Klabu za Misri kwa miaka mingi zimekuwa zikiisumbua Yanga bila kujali ukubwa au ukongwe wao, hivyo Yanga wanahitaji kuwa makini sana kesho wanapokutana na timu hiyo pamoja na kucheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Yanga wana uwezo mkubwa wa kupata ushindi kama benchi la ufundi litakuwa limefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo iliyopita ya kimataifa na ile ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kitu ambacho kinaweza kuwapatia mabao mengi katika mchezo huo.

REKODI ZA KIMATAIFA

Yanga pamoja na mechi za ligi kuanza kwa kusuasua, lakini kwenye mechi za kimataifa walikuwa wanaonesha uhai kwa kutoa ushindani mkubwa ingawa hawakupata matokeo ambayo walikuwa wanategemea kuyapata. Tatizo hilo linachangiwa zaidi kwa asilimia kubwa kikosi hicho kimetawaliwa na wachezaji wageni ambao wanahitaji muda wa kuzoeana na kupata muunganiko mzuri.

Rekodi zinaonesha Yanga wameshinda mchezo mmoja wa mkondo wa pili dhidi ya Township Rollers kwa bao 1-0 ugenini, huku wakipoteza mechi moja mbele ya Zesco kwa mabao 2-1 ugenini Zambia na kupata sare mechi mbili dhidi ya Rollers na United yote ya mkondo wa kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa. Wakati wapinzani wao Pyramids walishinda michezo yote miwili dhidi ya Etoile du Congo kwa jumla ya mabao 5-2 na kupata ushindi wa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya CR Belouzizdadi ya Algeria na kufanikiwa kukutana na Yanga.

Idadi hiyo ya mabao waliyokwishafunga inaifanya Pyramids kuwa ni miongoni mwa timu yenye safu bora ya ushambuliaji inayowafanya kuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao matatu kwenye kila mchezo waliocheza. Rekodi ambazo zinatakiwa kuchungwa zaidi na wachezaji wa Yanga ambao safu yao ya ulinzi hadi sasa imeruhusu mabao manne ikiwa sambamba na kufunga idadi ya mabao matatu.

MKALI WA PYRAMIDS

Pyramids wanajivunia mshambuliaji wao matata, Abdalla Said analiyeibeba timu hiyo kwa kuifungia mabao sita kwenye ligi yao ya ndani akiwa na wastani wa kufunga angalau bao moja kila mchezo. Kikosi hicho kinachonolewa na aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Sébastien Desabre kina thamani kubwa ya kifedha Sh bilioni 52.7 huku wachezaji wake 12 ni miongoni mwa nyota wanaunda kikosi cha timu ya taifa ya Misri.

WANACHOTAKIWA KUFANYA

Kuhakikisha wanatumia vema faida ya uwanja wa nyumbani na uwingi wa mashabiki, Yanga wanatakiwa kupambana kufa au kupona ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono, kwani Wamisri wanajulikana wanacheza kwao, hivyo ni muhimu Yanga wakashinda kesho. Yanga wanatakiwa kuingia uwanjani huku wakijiamini na kuondoa kabisa dhana kuwa timu za Misri hazifungiki, kwani hilo litawezekana tu kama wachezaji wake watapambana vizuri tena bila kuchoka.

TIMU ya soka ya Polisi Zanzibar inayoshiriki Ligi Kuu ya ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi