loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TIC yasajili miradi ya trilioni 4.6/-

MAZINGIRA bora ya uwekezaji, yameifanya Tanzania kuendelea kuvutia wawekezaji wengi, ambao kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili miradi 227 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 2.00693 (Sh trilioni 4.6) kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, huku ikishika nafasi ya saba kati ya nchi 20 za Afrika zinazovutia wawekezaji.

Utekelezaji wa miradi hiyo 227, utasaidia kutengeneza ajira zaidi 38,000 kwa Watanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya viwanda, usafirishaji, biashara ya huduma, utalii, nishati, fedha, mawasiliano na kilimo.

Kati ya miradi hiyo, sekta ya viwanda iliongoza kwa kusajili miradi 128, usafirishaji miradi 29, biashara ya huduma miradi 18, kilimo miradi 14, majengo ya biashara miradi 10, rasilimali watu kama vile vyuo miradi 6 na sekta zingine ikiwemo fedha na mawasiliano miradi miwili au mmoja.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe amesema jijini Dar es Salaam kuwa, kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji, kunatokana na juhudi za serikali kuimarisha miundombinu ya nishati, usafirishaji kama vile barabara, reli na anga, kuondoa baadhi ya kodi kwa wawekezaji na uhamasishaji unaofanywa na kituo hicho kuwavutia wawekezaji.

Mwambe amesema ripoti za tafiti za uwekezaji na biashara, zilizofanywa na taasisi huru za kimataifa za ABSA Group Limited na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IFC) ambayo iko chini ya Benki ya Dunia, zinaonesha Tanzania kupanda katika kuvutia wawekezaji na biashara.

Amesema ripoti ya ABSA Group Limited ya Oktoba 2019 imeitaja Tanzania kushika nafasi ya saba kati ya nchi 20 za Afrika katika masoko ya uwekezaji Afrika mwaka huu, ikilinganishwa na nafasi ya 15 iliyoishika mwaka 2018.

IFC imeitaja Tanzania kushika nafasi ya 141 kati ya nchi 190 duniani, ilizozifanyia utafiti kuhusu mazingira bora ya kufanya biashara, ikilinganishwa na nafasi ya 144 kati ya 190 iliyoishika mwaka uliopita.

Pamoja na matokeo hayo chanya ya utafiti kwa Tanzania, Mwambe alisema matokeo ya tafiti za taasisi hizo wakati mwingine zina walakini, kwa sababu hazipati taarifa sahihi za nchi kutoka katika vyanzo sahihi serikalini.

Alisema taasisi kama ya IFC wakati mwingine hutumia watu binafsi, wataalamu washauri au kampuni za uwakili, kupata taarifa kuhusu maboresho ya sheria au sera za uwekezaji, yaliyofanyika katika nchi husika na huzitumia taarifa hizo kuishindanisha na nchi zingine duniani.

Aliongeza kuwa utaratibu huo, unaweza kuwafanya wasipate taarifa za kutosha na kuipa nchi nafasi isiyostahili.

Amesema kuna utaratibu utaandaliwa wa kuziwesha taasisi hizo kupata taarifa sahihi kutokana serikalini.

“Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema serikali itatengeneza mpango (Blueprint) utakaosaidia kushughulikia maeneo yote yaliyokuwa yakikwamisha juhudi za uwekezaji kisera, kisheria, kikanuni, kimatamko ili tuwe na mazingira bora na shindani zaidi ya uwekezaji, kila nchi duniani huwa inafanya hivyo,” alieleza Mwambe.

Alisema uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia saba, ikitanguliwa na Ethiopia yenye uchumi unaokua kwa asilimia nane.

Alisema Tanzania ni ya tano kati ya mataifa 10 ambayo uchumi wake unakua kwa kasi duniani.

Kwa mujibu wa Mwambe, ripoti ya IFC imeyataja maeneo ambayo Tanzania imefanya vizuri katika kuvutia uwekezaji na biashara kuwa ni namna inavyoendesha masuala ya zabuni, mtu kuanzisha biashara tangu aisajili hadi kupata namba ya mlipa kodi, vibali vya ujenzi, mazingira rahisi ya kulipa kodi ikiwamo kupitia simu za mkononi na kuwalinda wanahisa wadogo dhidi wanahisa wakubwa katika kufanya maamuzi.

Alisema IFC inatumia vigezo 11 katika kushindanisha nchi mbalimbali duniani kuhusu mazingira rahisi ya ufanyaji biashara. Kati ya nchi hizo 190, zimo zenye uchumi mkubwa kama vile nchi za Ulaya na Marekani zenye uchumi wa kati na za uchumi mdogo.

KATIBU Tawala Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora, amewaomba wamiliki ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi