loader
Jangwani kujengwa daraja la juu, boti kubeba watalii kuwa kivutio

Jangwani kujengwa daraja la juu, boti kubeba watalii kuwa kivutio

ILE adha ya mafuriko katika Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam, inayosababisha Daraja la Jangwani kufunikwa na maji, imepatiwa ufumbuzi. Wakati wowote kuanzia sasa, daraja hilo litafumuliwa na kujengwa upya kwa kunyanyuliwa mita 300.

Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda wakati akizungumza kwenye kongamano maalumu kuelekea uchaguzi, uchumi wa viwanda, amani, mahusiano, uzalendo na ustawi wa Taifa lililoandaliwa na Kamati ya Amani mkoani humo.

Makonda alisema; “ninaomba radhi ya kuchelewa kuhudhuria kongamano hili kwa wakati, nilikuwa nifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani kwangu, na niwaeleze tu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatelekezwa, tumepata fedha Dola za Marekani milioni 120 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya mafuriko Bonde la Msimbazi, tunafumua Daraja la Jangwani na kulinyanyua kwa mita 300.”

Alisema fedha hizo zimepatikana kutoka Benki ya Dunia za kuijenga upya Jangwani. Tayari upembuzi yakinifu umefanyika ili kumaliza changamoto ya mvua na mafuriko eneo hilo, yanayosababisha mawasiliano kuvunjika.

“Lengo ni kumaliza changamoto kubwa tulizozoea kuziona hasa kwenye bonde hilo la Msimbazi lakini kubwa katika daraja hilo la Jangwani…sasa tunalinyanyua mita 300 na kila upande tunatengeneza maeneo ya kutalii na kujenga hoteli na pia tutaweka boti za utalii katika mto huo ili wanaopenda kuona mto huo kuelekea baharini wafanya utalii wao,” alisema Makonda.

Alisema baada ya kunyanyua daraja hilo, maji yatapita kwa urahisi na kwa kasi kuelekea baharini. Kwamba mtaalamu mshauri kwenye upembuzi yanikifu, alichora michoro itakayotumika kunyanyua daraja hilo ili pia kuruhusu boti kupita chini yake na maji mengi nayo kusafiri bila kikwazo.

Akizungumza kujengwa upya kwa barabara kuanzia Buguruni hadi kuunganisha na barabara ya Morogoro, kuelekea kwenye daraja hilo yenye umbali wa kilometa nane, Makonda alisema njia hiyo inafumuliwa na kujengwa upya na kwamba ujenzi huo utaanza muda wowote kuanzia sasa. Awali, akitoa mada kuhusu uhusiano wa kufanya kazi kwa bidii na ustawi wa Taifa kwenye kongamano hilo, Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe alisema Tanzania ina bahati ya kumpata Rais John Magufuli anayehimiza wananchi kufanya kazi.

“Tanzania tuna bahati ya kumpata Rais anayehimiza watu wake kufanya kazi, yeye mwenyewe ni mchapakazi na kauli yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ ni nzito isichukuliwe kimzaha na kama tukimpa muda zaidi Rais Magufuli atatufundisha kufanya kazi zaidi kwa manufaa yetu,” alisema Askofu Kakobe.

Akitoa salamu zake, Mufti wa Tanzania, Abubakari Zubeir alisema viongozi wa dini wana jukumu la kusimamia uzalendo na kuhimiza waumini wao kufanya matendo ya amani ili nchi iwe na maendeleo ya kweli.

“Viongozi wa dini tuna wajibu mkubwa wa kuwahimiza na sisi pia kuwa mfano wa kuwa wazalendo na kuhimiza amani kwani ni alama dhahiri ya mtu aliyeshika dini, tunapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao tuhakikishe tunahimiza waumini wetu kushiriki kwenye uchaguzi huo na kuchagua viongozi sahihi kwa maslahi ya maendeleo yetu,” alisema Mufti Zubeir.

Aliongeza nchi haina dini ila watu wake wana dini na kinachoongoza nchi ni Katiba ambayo imeweka bayana jinsi ya kupata viongozi kwa kufanya uchaguzi, ambao wananchi wake wanapaswa kushiriki kikamilifu ili kupata viongozi waadilifu watakaoshirikiana na wananchi kuleta maendeleo.

Akisoma hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara alisema mchango wa taasisi na madhehebu ya dini katika kujenga ustawi wa watu na nchi, umechangia maendeleo nchini.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e6002dbdf17d389cbbb0497a6a4c2aa6.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi