loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Al Kasusu gumzo nguvu za kiume

NI saa mbili asubuhi katikati ya Jiji la Dar es Salaam katika Mtaa wa Samora, nakutana kijana amebeba chupa mbili za chai zenye kinywaji maarufu hivi sasa mjini cha Al Kasusu!

“Al Kasusu, al Kasusu hiyo! yalikuwa maneno ya kijana huyo huku baadhi ya wateja wanaume wakimwita na kuwahudumia kichwaji hicho, kinachouzwa kwa bei ya kati ya Sh 500 hadi 700 kwa kikombe kidogo.

Nikatamani kujua ni kinywaji gani hicho, maana wengi wetu tumezoea kuona vijana kama hao, wakitembeza kuuza kahawa, uji au maziwa, lakini hiyo Al Kasusu ni ingizo jipya!

Katika uchunguzi wa gazeti hili, tulibaini kuwa katika jamii kuna hulka ya watu hasa jinsia ya kiume, kupenda kunywa juisi ya tende, kinywaji kinachozidi kuwa maarufu kila kukicha.

Kinywaji kinachochanganywa na mihogo, karanga mbichi huku wengine wakiongezea unga uitwao Abati Soda na unga mwingine unaitwa Watu.

Niliamua kufanya udadisi kujua kinywaji hicho cha Al Kasusu ni kitu gani, kwani siku moja nikiwa ofisini nilisikia baadhi ya wafanyakazi, wakibishana kuhusu kinywaji hicho, na baadhi walisema ni cha kuongeza nguvu za kiume na ndio kinywaji maarufu hivi sasa mjini.

Niliingia mitaani kufuatilia kuanzia asubuhi hadi jioni katika vijiwe tofauti jijini Dar es Salaam na ndipo asubuhi moja ninakutana na kijana huyo anayetembeza alkasusu!

Siku nne za ufuatiliaji wa suala hilo, nilitembelea maeneo kadhaa jijini humo yakiwamo matatu maarufu kwa uuzaji wa kahawa hizo pamoja na dawa nyingine ziaminika kuongeza nguvu hizo za kiume.

Kijiwe cha Mtoni Mtongani Kijiwe hiki kipo nyuma ya kituo cha mabasi yanayoelekea njia ya Mbagala, ambako hapa ni zaidi inauzwa kahawa huku wateja wengi ni watu wa rika la kati na watu wazima. Kuna mabirika mengi kidogo, huku wanywaji wakitumia muda wao mwingi kunywa na kuzungumza masuala mbalimbali.

Nilijumuika nao na kuagiza kahawa, nilianza na kahawa ya kawaida nikichanganyia na kashata, lakini kadri muda ulivyozidi kwenda nikaagiza hiyo Alkasusu!

Huku stori za siasa zikiendelea wengine wakizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wengine wakizungumzia timu zinazocheza Ligi Kuu nchini, ndipo nikaamua hasa kutaka kujua undani wa hii Al Kasusu.

Baada ya kunywa nusu kikombe cha Al Kasusu, iliyokuwa ikinywewa kwa kiasi kikubwa na watu waliokuwa kwenye eneo hilo, nikagundua ni kinywaji chenye ladha ya kahawa, maziwa na sukari kwa mbali, lakini ukiinywa unabainisha kuwa kuna kitu cha nyongeza.

Niliamua kuvunja ukimya kwa kuzungumza na muuzaji wa kinywaji hicho, Ali Mzee ambaye bila kusita alibainisha kuwa kinywaji hicho kinatengenezwa kwa maziwa, unga na kahawa kidogo. Nikajikuta ninavutiwa zaidi kufahamu kuhusu unga huo, ambao unachanganywa.

Alibainisha kuwa unga huo unasaidia kuamsha msisimko wa kufanya tendo la ndoa, kwa kuongeza ashiki ya tendo kwa wanaume na kuwa wengi wa wanaokunywa, wanaupenda zaidi unga huo kwa kuwa unawasaidia.

Alibainisha kuwa kwa siku, anaweza kuuza hadi chupa tatu kubwa za chai na kuwa zinawahi kuisha huku wateja wakiwa watu wa rika zote.

Kuhusu undani kama Al Kasusu ni kweli inasaidia kama alivyodai muuzaji wake, mmoja kati ya watumiaji waliozungumza na gazeti hili, alibainisha kuwa kwa upande wake ilimsaidia siku ya kwanza alipoitumia, lakini haoni kama inamsaidia zaidi, isipokuwa yupo kwenye uwezo wake wa kawaida.

Alisema, “Al Kasusu itakuwa inawakubali watu na watu na pengine sio wote inayowasaidia,kwa upande wangu ninaona ni kawaida tu na nimeamua kuacha na kuendelea kutegemea uwezo wa asili.”

Wakati akimalizia kunieleza kuwa Al Kasusu haimsaidii, nilikuwa nimeshafikisha kinywaji changu hicho nusu kikombe na nikaamua kuishia hapo na kuendelea kusikiliza stori nyingine za kijiweni hapo.

Kijiwe cha Magomeni

Kesho yake niliamua kwenda Magomeni Mapipa mahali ambapo ni maarufu zaidi kwa uuzwaji wa tende, Al Kasusu na dawa nyingine, zinazosemekana kuwa ni za kuongeza nguvu za kiume. Niliwasili majira ya saa 11 jioni na kumkuta mwanadada wa makamo, akimuuzia tende mteja kwenye duka lake hilo.

Nilimsikia akiuliza kama amuongezee abat soda katika juisi hiyo ya tende na hapo nikaanza tena kudadisi ni nini hasa kinachowekwa kwenye juisi hiyo, huku nikiulizia kama wanauza na Al Kasusu.

Mwanadada huyo aliyejitambulisha kwa jina la Sophia, alisema anatengeneza Al Kasusu, tende dawa na tende za juisi za kawaida, huku akibainisha kuwa anazo dawa ya Viksi ambayo yenyewe inatokea Congo, ni ya kupaka katika uume, huku nyingine za Kasongo na Power Haute zenyewe ni za kunywewa na zinauzwa Sh 10,000.

Kutokana na maelezo yake hayo, ndipo nikabaini kuwa kumbe kuna aina mbalimbali ya dawa za asili za kuongeza nguvu za kiume; na ndio pia sababu ya watu kupendelea kwenda kwenye maeneo kama hayo, kupata kinywaji cha Al Kasusu au tende, huku pia wakihudumiwa na dawa hizo.

Niliongeza wigo wa utafiti wangu na kuingiwa na shauku ya kutaka kujua zaidi, kujua utendaji kazi wa hizo aina nyingine za dawa, hasa hiyo ya kupaka ya Viksi, ambapo Sophia alibainisha kuwa ina wateja wengi, lakini ni hatari iwapo kama mtumiaji atazidisha kipimo.

Alisema mtumiaji anapaswa kupaka kidogo katika uume wake, lakini wapo ambao wamekuwa wakipaka nyingi na mwisho wa siku uume unashindwa kufanya kazi.

Sophia alisema huwa hawashauri watu kutumia dawa hiyo, hasa kutokana na kuwa ina uwezo mkubwa, lakini pia inafanya kazi kwa wakati mmoja, hasa pale mtumiaji anapotaka kufanya tendo la ndoa.

“Mimi hakika huwa siwaambii wanunue hii, kwa kuwa kama mtu akitumia vibaya inamwathiri yaani ni bora hata hii ya kunywa ya Power Haute ambayo inamwezesha mtumiaji kufurahia zaidi kwa kuwa yenyewe anakuwa anakunywa kama juisi,” amesema.

Kuhusu namna anavyowasaidia wenye uhitaji, alisema wanaopendelea kuongeza ashiki ya tendo la ndoa, huwatengenezea juisi ya tende, kisha huwachanganyia abat soda na watu viungo vinavyoongeza ashiki ya tendo.

Alieleza kuwa unga huo wa abat soda, ndio unaongeza ashiki zaidi ya tendo huku akibainisha kuwa juisi ya asili ya Power Haute, yenyewe mbali na kusaidia kuongeza ashiki katika tendo, pia inatibu magonjwa mengine kama ngiri, pumu na mengineo.

Nikamrejesha kwenye mjadala wa Al Kasusu ambao mwanadada huyo anayeandaa kinywaji hicho, alitoa maelezo ya utengenezwaji wake yanayofanana na ya yule muuzaji wa Mtoni Mtongani.

Alisema kuwa anaununua unga huo Vingunguti kisha kuuchanganya na maziwa na kahawa.

Kijiwe cha Posta Samora

Kama ilivyo vijiwe vingine vya kahawa jijini Dar es Salaam, kijiwe kimoja eneo la Mtaa wa Samora nako kinywaji hicho Al Kasusu kipo.

Mbali na kuuzwa kwenye kijiwe hicho, pia wapo wengine wanakitembeza chupa mbili za chai na kusema Al Kasusu, Al Kasusu hiyoo! Haikupita dakika mbili, unasikia mteja anaitwa njoo leta hapa, hali hiyo nikafahamu kuwa kinywaji hicho kinatumika wakati wowote asubuhi na zaidi pia wakati wa jioni.

Unga wa Al Kasusu Kesho yake asubuhi nilienda Vingunguti karibu na njia ya reli na kukuta muuzaji akiwa kwenye nyumba moja, akiupakia unga huo kwa ujazo wa sawa na kikombe cha chai na kuuza kwa Sh 10,000 kwa pakiti moja.

Hapo ndipo nikaongeza wigo zaidi wa kufuatilia suala la tiba za asili za upungufu wa nguvu za kiume, kwa kuwa kumbe Al Kasusu na hata maelezo ya yule dada wa Magomeni, yanaashiria kuwa kuna tiba za asili ambazo wananchi wanaaminishwa kuwa zinatibu nguvu hizo.

Juma Nassoro ni muuzaji wa unga huo, anabainisha kuwa wanauagiza unga huo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC), ambako wanachukua unga mwingi kabla ya kuanza kuufungasha kwenye pakiti za kawaida.

Nassoro alisema unga huo ni wa aina yake, kwa kuwa unasaidia kuongeza ashiki ya tendo la ndoa na kwa watumiaji huamini kuwa unawaongezea uimara kwenye tendo.

Wasemavyo watumiaji

Mmoja kati ya waliowahi kutumia dawa hizo, Haule Mzee alisema kuna athari kubwa kwa watumiaji wa dawa hizo, kwani yeye awali alikuwa na uwezo wa kawaida kwenye tendo.

Anasema alipoanza kutumia dawa hizo alijiona uwezo unaongezeka mara mbili na zaidi, lakini kadri muda ulivyosonga ukaanza kupungua na kuwa mdogo kuliko awali.

Alisema hali ilizidi kuwa mbaya, ikambidi aende hospitalini na alieleza ukweli na kuambiwa aache kutumia na kushauriwa kula vyakula vya kumsaidia kurutubisha afya yake hadi hali yake ilipoanza kurejea kawaida.

Hata hivyo, hivi sasa hatumii dawa ya aina yoyote ya kuongeza nguvu za kiume.

Naye Ashura Saleh alibainisha kuwa mpenzi wake hutumia zaidi hiyo dawa, lakini haoni kama inasaidia kitu chochote, huku akionesha kuwa mumewe huyo ameshawahi kutumia aina nyingine ya dawa za asili iitwayo Mungungu, ambayo ilimsaidia kwa siku za mwanzo tu.

“Mimi ninaona ni vema tu aache kwa kuwa kwanza ninaona ni kama kawaida tu akitumia au asipotumia ila sijui ni kwa nini anapenda kutumia hizo dawa, na hiyo Mungungu akiitumia inakuwa na nguvu siku hiyo hiyo aliyotumia,” alieleza Ashura alipozungumza na gazeti hili.

Gazeti hili limebaini uwepo wa dawa aina mbalimbali zinazouzwa kwa lengo la kuongeza nguvu za kiume, kama vile Mundende na Vumbi la Congo zinazotokea DRC, lakini pia zipo Mungungu, Kahawa dawa na nyinginezo za nchini.

Habari hii itaendelea kesho kwa kushirikisha wataalamu zaidi wa tiba za asili na watengenezaji zaidi wa dawa hizo.

WANAFUNZI wenye ulemavu wanaosoma shule za msingi mkoani Dodoma wameiomba ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi