loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mume, mke, watoto 3 walivyokufa maji

VIFO vya watu watano wa familia mmoja, waliokuwa wakiishi Goba jijini Dar es Salaam, vimeongeza majonzi zaidi baada ya Mtawa Regina Mndeme kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mother Theresa of Calcutta ya Same mkoani Kilimanjaro, kuelezea yaliyomsibu mtoto aliyeachwa yatima.

Mtawa Mndeme ni mlezi wa wanafunzi katika shule hiyo, anayosoma mtoto Anna Lingston Zambi.

Lingston Zambi na mkewe Winfrida Lyimo, na watoto wao, Lulu, Andrew na Grace, wamekufa kwa ajali ya gari baada ya gari hilo kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa wilayani Handeni mkoani Tanga.

Miili yao ilifikishwa nyumbani kwao Goba, karibu na Shule ya English Medium ya Hekima Wordolf, saa 4:04 juzi usiku na kuibua simanzi kubwa kwa ndugu na majirani wa familia hiyo, iliyokuwa inaenda katika mahafali ya binti yao, Anna, yaliyopangwa kufanyika Jumamosi iliyopita.

Akitoa salamu za rambirambi kwa waombolezaji nyumbani kwa marehemu jana, Mtawa Mndeme alisema Jumapili akiwa amelala kutokana na kutokujisikia vizuri, alisikia mtu akilia kwa sauti kubwa, kisha aliendelea kulala.

Alisema sauti ile iliongezeka, ambayo ilikuwa ni ya kupiga mayowe, hivyo aliamka ili kwenda kuangalia kuna nini, baada ya kufika hapo alimkuta Anna ambaye sasa ni yatima, akilia huku akieleza kuwa amesoma miaka minne wazazi wake wameshindwa kwenda kwenye mahafali yake.

Mtawa asimulia Mtawa huyo alisema alimwambia Anna kuwa jana yake siku ya mahafali walizungumza na watoto ambao wazazi wao wanaishi Dar es Salaam, kuwa walishindwa kwenda kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha, kusababisha mafuriko na kuwataka wawe na utulivu.

“Jumamosi ilikuwa ni siku ya mahafali hapa shuleni, wazazi wa Dar es Salaam walishindwa kufika, wanafunzi wakapata huzuni wakalia lakini tuliwatuliza.

“Siku ya pili nilikuwa nikijisikia vibaya nikanywa dawa na kupumzika, kuna umbali kidogo nilipokuwepo na kwenye mabweni ya wanafunzi lakini nilisikia mwanafunzi anapiga mayowe kwa sauti kubwa nikatoka na kuangalia nikamkuta Anna.

Nilipomuuliza analia nini akasema nimesoma miaka minne wazazi wangu wameshindwa kuja kwenye graduation yangu,” amesema mtawa huyo.

Kwa maelezo ya mtawa huyo, huwa linapotokea jambo, roho huwa zinawasiliana japo kwa mtazamo wa macho ya kawaida unaweza usione.

Hivyo, ndivyo ilivyokuwa kwa binti huyo, aliyeachwa na wazazi wake, anayetarajia kufanya mitihani yake ya kumaliza kidato cha nne wiki ijayo.

Miili ilipowasili juzi nyumbani, waombolezaji walilia kwa sauti kubwa, huku baadhi yao kwa kupokezana wakiwa wanaingiza jeneza moja baada ya jingine ndani ya nyumba hiyo kuanzia baba, mke wake na watoto wao watatu.

Ijumaa iliyopita, Zambi ambaye ni Ofisa Uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani, mkewe na watoto wao watatu, waliondoka kwenda kwenye mahafali ya binti yao, anayetarajiwa kuanza mitihani yake wiki ijayo.

Ndugu waongea

Mzungumzaji wa familia ambaye ni mtoto wa kaka yake marehemu, Ibrahimu Zambi alisema taarifa za msiba huo mzito kwa familia yao, alizipata Jumatatu saa tano asubuhi kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, ambaye alimpigia simu na kumuuliza kama ana uhusiano na marehemu akamjibu ndiyo.

“Mkurugenzi aliniambia unajua yuko wapi? Nikasema sijawasiliana naye ndani ya wiki hii, ila ninajua atakuwa ama kazini kwake Chalinze au nyumbani kwake Goba.

“Akaniambia amepata taarifa kutoka Handeni kwamba wamemuokota mtu ambaye alikuwemo katika ajali ya gari ambayo imezama kwenye mto na katika ile ajali huyo mtu amekutwa na cheti kwenye mfuko kilichomtambulisha anaitwa Lingston Zambi ambaye ni Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze,” amesema.

Alisema mkurugenzi huyo, alimweleza kuwa baada ya kukuta vyeti, hivyo walituma watu kwenda kuutambua mwili huo na kuthibitisha ndiye hivyo alimwagiza awasiliane na ndugu zao wengine kuwapa taarifa hiyo.

“Mimi niliwasiliana na nyumbani kwa marehemu, bahati mbaya sikupata simu zao nikawasiliana na shangazi yake ambaye yuko karibu na hilo eneo na kunieleza kuwa familia nzima ilikwenda kwenye mahafali ya mtoto wao,” alisema.

Alielezwa familia iliondoka Ijumaa, lakini alikuwa hawapati kwenye simu hadi alipopewa taarifa za msiba. Alisema alipokuwa akiwasiliana zaidi na mkurugenzi huyo, alimweleza kuwa pia kuna maiti ya mwanamke mtu mzima na watoto wawili waliopatikana kwenye ajali hiyo ya maji.

Alisema walipata ushirikiano kutoka Halmashauri ya Chalinze na kwenda Handeni, walipofika walifanya utambuzi wa miili na kutambua mwili wa Zambi, mkewe Winfrida na watoto wake wawili; Andrew wa darasa la kwanza na Lulu wa darasa la tano.

Kichanga cha mwisho Mtoto mchanga, Grace alipatikana juzi Jumanne, ndipo safari ya Dar es Salaam nyumbani kwa marehemu ilianza.

“Baada ya hatua hiyo tuliripoti polisi kuwa sisi ni ndugu zake nao wakatupa utaratibu, tukaanza mchakato wa kujua wapi tunaenda kuzika, kulipokucha Jumanne kitu cha kwanza tuliamua kwenda eneo la tukio ili labda tungeweza kubahatisha kupata mwili wa huyo mtoto ambaye alikuwa hajapatikana.

“Kwa bahati nzuri baada ya kutafuta kwa masaa matatu tukabahatika kuupata mwili wa mtoto huyo ambao ulikuwa umeanza kuharibika…watu wa fire walikuwepo kwa ajili ya uokozi kisha tukaendelea kufanya utaratibu mwingine kwa ajili ya safari ya kuja nyumbani kwake Dar es Salaam,” alisema.

“Tumepokea taarifa hii kwa majonzi makubwa sana kwa sababu ni pigo kubwa kwa familia moja kufiwa na watu watano kwa pamoja. Na tunaomba Mungu aendelee kututia nguvu,” alisema.

Ridhiwani atoa neno

Akizungumza nyumbani kwa wafiwa hao, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema wamesikitishwa na msiba huo kwani kwao ni mkubwa.

Alisema kwa bahati mbaya katika halmashauri hiyo, wamepata misiba mikubwa miwili, ambayo yote ilikuwa kwenye gari moja ukiwamo huo wa familia ya Zambi pamoja na watu wengine sita wa familia moja wanaotoka Kijiji cha Kihangaiko Kata ya Msata.

Alisoma watu hao sita nao walikuwa kwenye gari moja na familia hiyo ya Zambi, wao wameshazikwa tangu juzi katika Kitongoji cha Madesa na marehemu hao watano wamezikwa jana eneo la Goba.

“Leo (jana) tumekuja kushiriki msiba wa mwenzetu ambaye alikuwa Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Chalinze, Zambi ambaye amefariki na mkewe na watoto wake watatu,” alisema.

Alisema ni wiki ngumu kwao ndani ya Chalinze. Alimwelezea Zambi kuwa walikuwa naye kwenye kazi ya kuandaa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika kushawishi na kuhamasisha watu wajitokeze kujiandikisha.

MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania anayefanya shughuli zake Marekani, Flaviana ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

1 Comments

  • avatar
    jenipha
    21/11/2019

    wanga wa milele uwaangazie wapumzike kwa amani

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi