loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzanite ya mabilioni yapotea Mirerani

MADINI ya Tanzanite yanayokadiriwa kuwa na thamani ya mabilioni ya shilingi, yanadaiwa kuyeyuka na serikali imewataka wamiliki wa migodi ya Tanzanite Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, kueleza yaliko kabla haijawachukulia hatua za kisheria.

Serikali imesema haijaoneshwa kama yameuzwa nchini au nje, kwa kuwa hakuna nyaraka wala kumbukumbu, zinazoonesha yameuzwa katika masoko ya madini nchini.

Wamiliki hao wa migodi na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa madini ya Tanzanite jijini Arusha, wanaidaiwa kuihujumu serikali ya Rais John Magufuli kwa kuficha madini hayo majumbani mwao ama kufanya biashara haramu, kwa kusafirisha kwa njia ya panya nje ya nchi na kuifanya serikali kukosa mapato na wao kujinufaidisha.

Ofisa Madini Mfawidhi Mkazi Kanda ya Mirerani, Daud Ntalima amesema nchi inahujumiwa na wafanyabiashara wakubwa wa Tanzanite.

Alieleza kuwa kuna genge la wafanyabiashara wakubwa 25, aliowataja kwa majina (majina tunayo), wanaoihujumu serikali katika biashara hiyo na kuikosesha mapato mengi.

Ntalima alikuwa akizungumza katika mkutano, uliofanyika ofisi za Wizara ya Madini Mirerani na kushirikisha wamiliki wa migodi ya Tanzanite, viongozi na wanachama wakubwa wa Chama cha Kuuza na Kununua Madini nchini (TAMIDA), wanunuzi wa kati na wadogo, viongozi na wanachama wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Manyara (MAREMA) na viongozi wa FEMATA,

Alisema genge hilo linahusisha wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia na wengine wazawa ambao wanakaa vikao katika hoteli kubwa za Arusha kupanga namna ya kuihujumu serikali kwa kushusha thamani ya Tanzanite kwa kuficha madini hayo majumbani na wengine kusafirisha nje kwa njia za panya na kuifanya serikali kukosa mapato.

Ofisa huyo amesema wafanyabiashara wakubwa na wenye ukwasi mkubwa wa fedha jijini Arusha, kwa sasa wameamua kususa kununua Tanzanite kutoka kwa wauzaji wa kati na wadogo, kwa visingizo visivyokuwa na maana, ili watekeleze malengo yao ya kushusha thamani ya madini hayo, kwa maslahi yao binafsi ya kibiashara.

Alisema kutokana na hali hiyo, amewapa siku saba wamiliki wa migodi ya Tanzanite Mirerani, kujisalimisha kwa kupeleka madini hayo katika ofisi za Mirerani au kupeleka nyaraka zinazoonesha walifanya biashara katika masoko yaliyotengwa na serikali; au nyaraka zinazoonesha yaliuzwa nje ya nchi na serikali kupata mapato yake.

Alisema ni mapema kutaja kiasi na thamani ya madini, kilichothaminiwa na ofisi yake, lakini baada ya kukutana na wamiliki wa migodi hiyo baada ya siku saba, anaweza kuelezea kila mmoja alichozalisha lakini kiasi ni kikubwa.

Alieleza kuwa wafanyabiashara hao wa Tanzanite, wanaichezea serikali kwa maslahi yao kwa kuuza madini hayo kinyemela na kwa njia ya panya kwa raia wa Bara la Asia; na ndio maana wanaifanya Kenya na India, ziongoze kwa kuuza tanzanite duniani huku serikali ikikosa mapato.

KATIBU Tawala Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora, amewaomba wamiliki ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Simanjiro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi