loader
Makonda- Siogopi kuongeza wanaonichukia

Makonda- Siogopi kuongeza wanaonichukia

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kutopewa kazi tena, mkandarasi wa Kampuni ya Nyanza Road Works katika mkoa huo kwa alichoeleza kuwa amekua anababaisha kwenye utekelezaji wa miradi.

Makonda alisema hayo jana katika ziara yake alipoingia kwenye mzozo na mkandarasi huyo ambaye alisema anafanya kazi kwa mujibu wa programu kama walivyokubaliana kitu ambacho kilionekana kumkera Makonda.

“Tanroads (viongozi wa Wakala wa Barabara) huyu Nyanza Road Works aliharibu mradi wa ujenzi barabara Temeke lakini mmempa tena kufanya mradi huu, kuna nini kinachoendelea?” amehoji Makonda na kuongeza;

“Nasema mradi huu ndio wa mwisho. Sasa mumpe tena mradi mwingine mtanijua kama mimi ndio mkuu wa mkoa au nyie,” alisema na kumgeukia Ofisa Tawala wa Ilala, Jabiri Makame akimfokea.

Makonda alisema mkandarasi Nyanza Road Works ameharibu miradi mingi ikiwemo wa Nyakanazi kwenda Kakonko, Musoma na Temeke huku akishangaa kwa nini anaendelea kupewa miradi licha ya kuvurunda.

“Mamlaka zinakula rushwa, haiwezekani mtu analalamikiwa lakini bado anapewa kazi. Siogopi kuongeza idadi ya wanaonichukia, Nyanza Road Works tumempa zaidi ya sh milioni 800 lakini mpaka sasa anasuasua, vifaa hana ujanja ujanja tu,” amesema Makonda.

Kauli ya Makonda imetolewa siku chache baada ya kuagiza wakandarasi hao wa Nyanza Road Works na wenzao wa Chicco Engineering wanaojenga mradi wa mto Ng’ombe kuswekwa lupango kabla ya kutolewa kwa dhamana na kutakiwa kuendelea na ujenzi wa miradi yao.

Kuhusu mradi wa mto Ng’ombe, tayari wameshaanza kusafisha na kuongeza vifaa tayari kwa ujenzi huo na Makonda ameridhishwa kwa hatua ambazo zimeanza kutekelezwa na Mkandarasi wa Kampuni ya CHICCO ambae mradi wake wa mto Ng’ombe unagharimu Shilingi bilioni 32 na tayari amelipwa zaidi ya Sh bilioni 4.8.

Mbali na miradi hiyo miwili, Makonda alitembelea pia mradi wa machinjio ya Vingunguti na ule wa ujenzi wa soko la kisasa la Tandale na kudai kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo.

Akiwa katika ukaguzi wa mradi huo unaogharimu Sh bilioni 12.5, Makonda alilipongeza Shirika la Nyumba (NHC) ambao ndio wanautekeleza kuwa wanafanya kazi nzuri na wategemee kupewa miradi mingi zaidi.

Kwa upande wa soko la Tandale ambao unatekelezwa na Namis Corporate Limited kupitia meneja wa mradi huo, James Msumari, Mkuu huyo wa Mkoa, Makonda alisema anasubiri fungu la fedha kutoka serikalini ili wakandarasi waongeze kasi zaidi kwenye utekelezaji wake ambao kwa sasa unakwamishwa na uhaba wa fedha.

Makonda alimtaka mkandarasi kutekeleza mradi kwa asilimia 15 ndipo malipo yafanyike na kuwataka wakandarasi wote katika mkoa wa Dar es Salaam kukabidhi miradi yao kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6a574b368650d59b24525f1e88d53dd0.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi