loader
Picha

China inatekeleza wajibu kuhifadhi wanyamapori

BIASHARA ya totoaba, ambaye ni aina ya samaki mkubwa kutoka Mexico, ilipigwa marufuku tangu mwaka wa 1976, wakati aina hii ya samaki ilipoorodheshwa katika Mkataba wa biashara ya kimataifa kuhusu wanyama na mimea walio hatarini kutoweka maarufu kama CITES.

Aina hii ya samaki ni maarufu kwani asilimia kubwa ya watu wanaamini kuwa ina thamani ya lishe na kimatibabu.

Na kwa sababu ya ongezeko la mahitaji yake, samaki huyu ameorodheshwa kama mnyama aliye hatarini sana kutoweka.

Ni kutokana na hatua hiyo, China iliamua kujiunga na mataifa mengine katika kupiga marufuku samaki hao kutoingizwa katika mipaka. Ili kuangamiza kabisa biashara hiyo, China ilizindua msako wa kukamata mtu yeyote anayeshiriki katika biashara ya samaki huyo.

Washukiwa kadhaa walikamatwa na maofisa kutoka Idara ya Forodha katika uwanja wa ndege wa Guilin, mkoani Guangxi Zhuang nchini humo mwaka jana walipokuwa wakijaribu kupenyeza samaki hao kwa njia ya magendo.

Mahakama iliwahukumu watuhumiwa wawili kwenda jela miaka mitano na miezi miwili kwa kushiriki uhalifu wa biashara ya magendo ya bidhaa za thamani za wanyamapori. Tangu mwanzoni mwa 2018, Mamlaka ya Forodha iligundua ushirika wa waendeshaji biashara haramu ya totoaba nchini China.

Hadi sasa watuhumiwa 32 wamekamatwa huku bidhaa za magendo zenye thamani ya dola milioni 45 za Marekani zikinaswa.

Huu ni mfano mmoja tu ambao unaonesha wajibu wa China katika vita dhidi ya biashara haramu katika bidhaa za wanyamapori.

Kwa kweli, katika miaka ya hivi karibuni, China imefanya juhudi kabambe katika kupambana na biashara hii haramu na hii inadhihirika katika kukamatwa kwa wanaoishiriki na uchunguzi unaofanywa juu yake, katika masoko na asili ya bidhaa hizo.

Katika miezi michache iliyopita, mashirika ya usalama ya China yameshughulikia takriban kesi 600 zinazohusu biashara ya spishi zilizo hatarini, ambazo nyingi ni wanyamapori.

Kwa hakika, biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori inahusisha fedha nyingi mno huku ikikadiriwa kuzoa dola 7,000,000,000 hadi dola 23,000,000,000 za Marekani kwa mwaka.

Bidhaa za wanyamapori zinauzwa kama chakula, mapambo, dawa za jadi, na bidhaa nyingine za wanunuzi. Tamko la Lima ambalo China ni mwanachama limeimarisha ushirikiano katika udhibiti wa biashara hii mpakani.

Biashara hii ya jinai haipunguzi tu idadi ya wanyamapori lakini pia inachangia uharibifu wa mazingira ya asili huku ikihatarisha watu na makazi ya asili.

Dunia leo iko kwenye hatari hasa kuhusiana na idadi ya ndovu. Mauaji haramu ya tembo, kwa kiasi kikubwa, ni kwa sababu ya pembe zao. Hili kwa sasa ni tishio kubwa sana kwa idadi ya wanyama hao barani Afrika na duniani kote.

Maelfu ya ndovu wanaendelea kuuawa kila mwaka kinyume na sheria huku takwimu zikionesha kuwa idadi ya wanyama hao inaendelea kupungua hasa katika bara la Afrika.

Hatari hii kwa tembo inatokana na ukosefu wa sheria muafaka kuzuia kuuawa kwao, usafirishaji wa pembe zao, pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya pembe za ndovu. Ili kuondoa hatari hii kwa upande wake, China iliboresha utekelezaji wa sheria pamoja na kampeni za kuhamasisha umma kubadili mwenendo wao na kuacha kununua pembe za ndovu.

Kwa muda mrefu, serikali ya China imedhihirisha ahadi na nia yake ya uhifadhi wa wanyamapori kwa kuongeza bajeti ya mabilioni ya pesa inayotengewa ili kufikia juhudi hizo.

Waziri Mkuu wa China Li Keqiang, hivi karibuni alitangaza kwamba serikali ya China inayoongozwa na Chama cha CPC imetenga mamilioni ya fedha ili kuimarisha juhudi za kulinda mazingira ya asili na wanyamapori. Mwaka 2014, Li alizuru Hifadhi ya Taifa ya Nairobi nchini Kenya kama ishara ya kujitolea kwa China katika mapambano dhidi ya ujangili na biashara ya magendo ya bidhaa za wanyamapori kwa taifa lake.

Serikali ya China baadaye ilitangaza kwamba itasaidia kuanzisha Kituo cha Mazingira ya Ikolojia na Wanyamapori katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi. Punde tu baada ya tangazo hilo, huduma za wanyamapori nchini Kenya (KWS) zilifichua kuwa China iliahidi kutoa ruzuku ya kuwezesha shirika hilo kupata vifaa vya uchunguzi na ukaguzi wa wanyama hasa wakati wa usiku.

Ishara hii ilimiminiwa sifa kedekede kutoka kwa wanamazingira ambao walipongeza kuwa China hatimaye imekuwa inaonesha kujitolea kwake kulinda mazingira na wanyamapori barani Afrika.

Lakini kando na mchango huo wa kifedha, serikali ya China kupitia Idara ya Misitu, ambayo inashughulikia masuala ya bidhaa za wanyama, ilianza kutoa fursa nyingi za ubadilishanaji wa mawazo kwa mamia ya maofisa kutoka Afrika na wadau wengine kutoka sehemu mbalimbali wanaohusika na uhifadhi wa wanyamapori.

Kwa wakati mmoja, China ilikosolewa na wengi kwa madai ya kutofanya lolote katika kusaidia vita dhidi ya biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori.

Hata hivyo wataalamu na maofisa wa serikali ya China wanapinga hoja hizi vikali na kuzitaja kuwa ni madai yasiyo na msingi wowote kwani kulingana na wao China imetoa mchango mkubwa zaidi katika kupambana na walanguzi wa bidhaa za wanyamapori.

“ China imetengeneza mfululizo wa sheria na taratibu za uhifadhi wa wanyamapori. Kwa sasa, vitendo vya ununuzi, uuzaji na usafirishaji haramu wa pembe za ndovu na bidhaa zingine nyingine za wanyamapori vinaadhibiwa vikali, “alisema Wang Weisheng kutoka Idara ya Misitu ya Taifa la China.

Takwimu kutoka katika Idara ya Misitu zinatoa ushahidi mahsusi na kuonesha kwamba kuanzia mwaka 2012 hadi 2014, watu 458 walikamatwa kwa tuhuma za kufanya biashara ya magendo ya pembe za ndovu.

Wale waliokamatwa na pembe za ndovu zenye thamani ya zaidi ya dola 145,000 za Marekani walihukumiwa kwa angalau miaka 10 gerezani.

Maofisa hao wanasisitiza kuwa China haifanyi mzaha kuhusiana na matendo yanayoathiri uhifadhi wa wanyamapori. Wanalaumu mtazamo huu kwa kutoa taarifa potofu, ambayo wanasema ndio sehemu wanayoweka juhudi ili kuukomesha na badala yake kuendeleza juhudi za kulinda wanyamapori.

“Adhabu yetu kwa biashara haramu ya wanyamaporiwanyamapori ni miongoni mwa zile kali zaidi ulimwenguni. Hiyo ndiyo halihalisi. Ni ukweli kabisa,” alisema Li Tiansong kutoka Idara ya Usimamizi wa Misitu ya Taifa ya China.

Wakati mwingine, baadhi ya watu wanaoendesha biashara hii haramu wamehuhukumiwa kifungo cha maisha na mali zao kutwaliwa na serikali.

Katika ripoti iliyochapishwa na gazeti la China Daily, kampuni 12 kati ya kampuni 14 za uchakataji wa pembe za ndovu zilifungwa mwaka 2017 pekee yake. Ripoti hiyo pia inasema idadi ya wauzaji wa pembe za ndovu imepungua kutoka 149 hadi 94. China pengine inaelewa umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori kuliko wengi wanavyodhania. Nchi hiyo huvutia baadhi ya watalii wengi zaidi wa kimataifa kila mwaka. Lakini kando na ziara za watalii wa kimataifa, utalii wa ndani pia umeshamiri.

Unapozuru mojawapo ya vivutio vya utalii nchini China, kwa mfano, ni dhahiri kuwa wenyeji wanatembelea maeneo hayo kwa wingi.

Aidha, si siri kuwa idadi ya watalii kutoka China wanaozuru Afrika imeongezeka mno. Hadhi inayotolewa kwa wanyama na mazingira ya asili nchini China itasaidia katika jitihada za uhifadhi kote duniani ikiwemo barani Afrika.

Juhudi za China katika kuendeleza utunzaji na uhifadhi wa wanyamapori pia zitasaidia ukuaji wa uchumi katika nchi ambazo zinategemea utalii.

Kama mojawapo wa wanachama wa Azimio la Lima, China inasema kuwa inachukulia biashara haramu katika bidhaa za wanyamapori kama uhalifu mkubwa katika sheria na kanuni za kitaifa, na kwa hivyo inatoa adhabu na faini ambazo zinaendana na uhalifu huo.

Hii ndio maana China imezipa nguvu zaidi taasisi za umma zinazohusika na vita dhidi yakupambana na biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori huku ikisaidia hatua za kufanikisha kuzuia usambazaji na kupunguza mahitaji ya bidhaa za wanyamapori kinyume na sheria, ikiwa ni pamoja na maeneo yahifadhi za asili yaliyohifadhiwa.

WAKULIMA wa Kijiji cha Manda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi