loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wagunduzi sasa kutumia kuro kudhibiti mbung’o

MNYAMA aitwaye kuro (waterbuck) anayepatikana kwa wingi katika nchi za kusini mwa Jangwa wa Sahara ikiwamo Tanzania, moja ya sifa zake ni kutoshambuliwa na mbung’o, mdudu ambaye pia huitwa ndorobo (tsetse fly) kama ilivyo kwa wanyamapori wengine.

Kwa hapa Tanzania wanyamapori hawa ambao kwa jina la kisayansi huitwa Kobus Ellipsirymnus wanapatikana kwenye hifadhi karibu zote za taifa zikiwemo Serengeti, Tarangire, Saadani na kwenye Pori la Akiba la Selous ambalo liko katika harakati za kugawanywa na kupatikana hifadhi mpya ya Nyerere.

Kuro ni mnyama anayependelea kukaa jirani na mito na mabwawa kwa ajili ya kujikinga na adui zake wakiwemo mbung’o ambao wanashindwa kumsogelea kutokana na kutoa harufu isiyowapendeza. Kitendo cha kuro kutoshambuliwa na mbung’o kimewaibua watafiti wa mifugo kuchunguza kwa kina ili kubaini kilichomo kwenye harufu ya mnyama huyo ambayo mbung’o huiogopa na kushindwa kumkaribia.

Ofisa mifugo na mtafiti kutoka Wakala wa Maabara za Veterinary (TVLA), kituo cha Tanga, Deusdedit Malulu, anasema mbung’o wanaosababisha vimelea vya nagana kwa wanyama na vimelea vya ugonjwa wa malale kwa binadamu hawajawahi kumng’ata kuro. Anasema TVLA kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo ya Kenya (KALRO) wamegundua kwamba kemikali zenye harufu alizonazo mnyama huyo (kuro) zinatokana na tezi zao za kuzuia jasho zinazosababisha watoe harufu fulani inayosababisha wadudu mbalimbali wakiwemo mbung’o washindwe kuwasogelea.

Malulu anatoa ugunduzi huo kwa waandishi wa habari walioshiriki mafunzo kuhusu uandishi wa habari za sayansi, teknolojia na ubunifu yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) yakihusisha watafiti mbalimbali kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki. Anafafanua kwamba mbung’o ni mdudu anayeishi kwa kutegemea kufyonza damu pekee na ndipo kwa kufanya hivyo humwachia mnyama vimelea vya ugonjwa wa nagana na binadamu ugonjwa wa kusinzia wa malale.

“Mbung’o ni tatizo hasa katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara Tanzania ikiwemo,” anasema mtafiti huyo.

Malulu anasema inakadiriwa kwamba theluthi moja ya eneo la Tanzania ina mbung’o na hasa kwenye maeneo ya mapori yakiwemo ya akiba na hifadhi za taifa. Anasema ingawa ugonjwa wa malale umepungua hapa nchini lakini umekuwa ukiripotiwa zaidi kwenye mikoa ya Katavi na Tabora wakati ugonjwa wa nagana kwa mifugo umeendelea kuripitiwa karibu mikoa yote hasa maeneo yaliyohifadhiwa.

“Ndiyo maana tunashirikiana na wenzetu wa Kenya na nchi nyingine zenye kuathirika na ugonjwa huu katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo,” anabainisha Malulu.

Anasema utafiti wa maabara umeonesha kuwa kemikali zilizomo kwenye mnyama kuro zina uwezo wa kufukuza mbung’o kwa zaidi ya asilimia 60 ukilinganisha na vifukuzi vingine vinavyopatikana sokoni.

“Matokeo ya utafiti huu kwa sasa umetoa matumaini kwamba tunaweza kuzalisha kemikali hizo kwa ajili ya matumizi na kwa sasa hatua zinazoendelea ni za ujasiri,” anasema Malulu.

Anaongeza: “Pia hatua nyingine ni ya kutunza kemikali hizo. Tunashirikiana na Kampuni ya A to Z iliyopo Arusha inayojihusisha na teknolojia ya kupambana na mbu waenezao malaria kwa kuzalisha vyandarua na vifaa vingine katika kufanyia kazi hili,” anasema Malulu.

Anasema ili kufanikisha ugunduzi huo, wanakusudia kubuni kibebeo kitakachovaliwa na mnyama, iwe kwenye shingo, sikio au mkiani ili harufu itokayo ndani ya kibebeo hicho iwafukuze mbung’o. Anasema harufu hiyo watawekewa ng’ombe kwenye kifaa maalumu watakachofungwa nacho ili akijitikisa imsaidie kusambaza harufu ya kemikali hiyo inayofukuza mbung’o.

Naye Meneja wa Wakala wa Maabara za Veterinary (TVLA) mkoani Tanga, Dk Imna Malele anasema mdudu mbung’o amekuwa changamoto kubwa kwa wafugaji wengi mbali na watu wanaoishi maeneo ya hifadhi, hivyo ni wakati mwafaka kutumia mbinu za kisasa katika kumwangamiza. Dk Malele anasema ugonjwa utokanao na mbung’o kwa mifugo umekuwa ukipunguza mazao yatokanayo na mifugo. Anafafanua kwamba mifugo inapoathirika na ugonjwa huo hukosa raha na kwamba teknolojia waliogundua ya kufukuza mbung’o kwa kutumia kemikali ni njia ya kibayolojia inayotazamiwa kutokuwa na madhara na ya uhakika zaidi.

“Njia hii ya kibayolojia ni tofauti na njia inayotumika sasa ya viuatilifu katika kudhibiti mbung’o. Kwa kutumia njia ya viuatilifu wanyama huogeshwa dawa ili kudhibiti mbung’o lakini inaripotiwa kwamba hali hiyo inaleta usugu kwa mbung’o,” anasema.

Anasema, kwa kutumia njia hiyo ya kibayolojia, mifugo hasa ng’ombe hawataweza kupata maambukizi ya vimelea vya vitokanavyo na mbung’o na hivyo wataongezeka kwa kuzaliana kwa wingi na kuwafanya wafugaji wawe na pato zuri la mifugo na maziwa.

Dk Malele anafafanua kwamba dawa hiyo ambayo sasa inaelekea kwenye hatua ya usajili inaweza kuchukua mwaka mmoja hadi kuanza kuwafikia wafugaji lakini anasema hii kwa wafugaji ni habari njema kwa sababu maeneo mengi yaliyohifadhiwa yana tatizo hilo.

“Lakini pia ni habari njema kwa watalii wanaoenda kwenye hifadhi kujikinga na kuumwa na mbung’o,” anasema Dk Malele.

Naye Mtafiti wa Mifugo katika kitengo cha udhibiti wa mitego ya ndorobo (mbung’o), Eugen Lyaruu anasema mbung’o wamegawanyika katika makundi matatu. Analitaja kundi la kwanza kuwa ni mbung’o wa maeneo ya nyika (Morsitans) na kundi la pili ni mbung’o wa misitu mikubwa (Fusca), wakati kundi la tatu ni wale wanaopatikana kando ya mito na maziwa waitwao kwa jina la kitaalamu, Riverine.

Mtafiti huyo anasema, pamoja na matokeo mazuri ya utafiti wa kutumia kemikali inayozalisha harufu ya mnyama kuro, bado kituo kinaendeleza udhibiti wa mbung’o kwa kutengeneza mitego mbalimbali kulingana na aina ya makundi hayo matatu. Anasema malengo ni kuwasaidia wafugaji kuondokana na madhara ya mbung’o, wenye hoteli za kitalii yaliyopo kwenye hifadhi za taifa kuwadhibiti wadudu hao na kwa shughuli nyingine katika jamii.

“Madhara ya mbung’o si kwa wanyama pekee bali hata kwa binadamu kutokana na kueneza ugonjwa wa malale, hivyo ni vyema kuwa na mpango mkakati wa kuwadhibiti,” anasema.

Hata hivyo, anasema sampuli zilizochukuliwa na kituo chao zinaonesha kwamba mbung’o wanaopatikana maeneo la Pori la Akiba la Selous wameonesha kuwa hawawadhuru binadamu isipokuwa wanyamapori pekee. Anasema kituo kimetengeneza mitego ya kutosha kwa ajili ya kusambazwa maeneo yenye mbung’o kulingana na aina ya makundi yao katika harakati za kuwadhibiti wadudu hao hatari.

“WATU wengine wakiona mwanamke mwenye ulemavu ana mimba, wanashangaa na ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi