loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ubidhaishaji wa lugha ya Kiswahili

MAKALA haya yatazungumzia mbinu zinazoweza kutumika katika ubidhaishaji wa Kiswahili. Ubidhaishaji wa Kiswahili ni kitendo cha kutangaza lugha ili ipate wajifunzaji wengi na hatimaye kukuza pato la taifa na jamii kwa ujumla.

Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha nne duniani zenye watumiaji wengi na zinazokua kwa kasi kubwa. Maendeleo ya lugha ya Kiswahili yamechangiwa na matumizi yake katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vya kimataifa kama vile BBC, Deutsche Well, Sauti ya Amerika na vituo vingine vya habari ulimwenguni.

Kiswahili ni lugha inayozungumzwa katika nchi za Afrika Mashariki mathalani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Pia Kiswahili ni lugha inayofundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali ulimwenguni katika nchi kama Marekani, China, Urusi na nchi nyingine.

Mchakato wa ubidhaishaji wa Kiswahili ni kitendo cha kutangaza lugha ya Kiswahili ulimwenguni ili wajifunzaji wa lugha waweze kununua maarifa ya lugha kama bidhaa nyingine. Ubidhaishaji wa lugha una faida nyingi sana. Makala haya yanazigawa faida hizo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Kiuchumi, lugha ya Kiswahili ina mchango mkubwa katika sekta ya uchumi. Ubidhaishaji wa Kiswahili unatengeneza ajira kwa mtu binafsi, taasisi na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.

Ubidhaishaji unaweza kuongeza ajira kwa mtu binafsi kama vile Ualimu wa kufundisha wageni, kufanya tafsiri na ukalimani katika mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Aidha, lugha ya Kiswahili ina mchango katika kuwaunganisha wafanyabiashara wa nchini na nje ya nchi, vilevile, utangazaji wa lugha ulimwenguni hukuza sekta ya utalii nchini.

Mfano nchini Tanzania lugha ya Kiswahili huwavutia wageni wengi kuja kujifunza na kutalii katika vivutio mbalimbali kama vile mbuga za wanyama, maporomoko na makumbusho ya kihistoria, jambo ambalo huongeza pato la taifa na jamii. Kiutamaduni, kutangaza lugha ulimwenguni kama bidhaa kuna faida kubwa sababu hutambulisha utamaduni wa lugha hiyo. Ubidhaishaji wa Kiswahili utachochea kusambaza utamaduni wa Waswahili ulimwenguni. Utamaduni huo ni pamoja na mavazi, chakula, mila na desturi n.k.

Hivyo kuitangaza vema lugha ya Kiswahili kutawavutia watu kujifunza lugha hiyo pamoja na utamaduni wake. Kijamii, ubidhaishaji wa Kiswahili una faida kubwa kwa jamii kwa sababu utatengeneza fursa kwa wanajamii. Mfano, kutengeneza fursa za ajira na kujiajiri kwa kuanzisha vituo binafsi vya ufundishaji lugha kwa wageni waingiapo nchini Tanzania.

Pia tunaweza kupunguza umaskini katika jamii kwa kuwa baadhi ya wanajamii baada ya kuajiriwa na kujiajiri watakuwa na uwezo wa kumudu mahitaji muhimu katika jamii. Mahitaji hayo ni chakula, malazi na mavazi. Baada ya kuangalia faida za ubidhaishaji wa Kiswahili, tunaweza kuona mbinu au njia ambazo zina mchango mkubwa katika kuitangaza lugha ya Kiswahili ulimwenguni.

Kwa ujumla, ubidhaishaji wa lugha ni mchakato wa kuitangaza lugha ulimwenguni ili watu wa mataifa mbalimbali wajitokeze kujifunza lugha hiyo; jambo hilo linafanyika kama biashara ya kubadilishana maarifa ya lugha na fedha. Njia hizo ni kama zifuatazo.

Mosi ni matumizi ya Kiswahili katika vikao vya kitaifa na kimataifa. Matumizi ya Kiswahili katika vikao na makongamano ya ndani ya nchi na nje ya nchi ni njia nzuri ya kuitangaza lugha ulimwenguni kwa sababu vikao na makongamano hayo huhusisha watu wa mataifa mbalimbali, jambo ambalo linaweza kuwavutia au kupata shauku ya kujifunza lugha hiyo na hata kuitangaza pale wanaporudi kwao.

Matumizi ya Kiswahili katika vikao vya kimataifa kama vile katika vikao vya Umoja wa Afrika (AU), vikao vya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) huweza kuwa chachu ya viongozi wa nchi mbalimbali kuhitaji kujua lugha hiyo, jambo ambalo linatengeneza ajira kwa wazawa kuuza maarifa ya lugha katika nchi za kigeni.

Pili, ni matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi. Matumizi katika vyombo au mashirika ya habari ya ndani na nje ya nchi yana mchango mkubwa katika kuitangaza lugha ulimwenguni.

Mfano ni katika mashirika ya habari kama vile BBC Swahili, Deutsche Welle, Sauti ya Amerika na mashirika mengineyo ulimwenguni ambayo hutumia lugha ya Kiswahili katika kuendesha vipindi na matangazo. Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuitangaza lugha ulimwenguni kwa kuwa wasikilizaji wake ni wengi, jambo ambalo huwavutia wengi kujifunza lugha hii ili wapate habari kwa ufasaha zaidi. Utangazaji huu hutengeneza fursa ya kufundisha lugha kwa wanaoihitaji. Njia nyingine ni kuitangaza lugha kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamerahisisha njia za kupashana habari juu ya masuala mbalimbali ulimwenguni. Wanajamii hupashana habari kuhusu masuala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Katika mawasiliano baina ya mtu mmoja na mwingine kila mtu yuko huru kutumia lugha yake anayoipenda. Hivyo katika harakati za ubidhaishaji wa lugha yetu ya Kiswahili ni muhimu kutumia lugha yetu ya Kiswahili ili kuwavutia watu wa mataifa mengine kupata shauku ya kujifunza.

Tunaweza kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram na Twitter katika kuitangaza lugha yetu ya Kiswahili ili kupata wahitaji wengi ambao wataongeza kipato kwa taifa na jamii kwa ujumla.

Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika uga wa sayansi na teknolojia ni eneo jingine muhimu. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamechangia katika ugunduzi wa vifaa mbalimbali vya kisayansi ambavyo hutumika kurahisisha mawasiliano na kazi katika jamii zetu. Mfano, ugunduzi wa vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta na simu za mkononi na vifaa vingine vimerahisisha sana mawasiliano. Lakini vifaa hivyo vingi hutumia lugha ya Kiingereza ilhali watumiaji wake wanatumia lugha ya Kiswahili na lugha nyingine tofauti.

Ili kuitangaza lugha yetu ya Kiswahili ni muhimu kuingiza lugha ya Kiswahili katika maelekezo ya matumizi ya vifaa hivyo ili kuwawezesha watumiaji kujua matumizi ya vifaa hivyo na kuwavutia wasiotumia Kiswahili kujifunza lugha ili wamudu kutumia vifaa hivyo. Baada ya kuangalia baadhi ya faida na mbinu au njia za ubidhaishaji wa Kiswahili ulimwenguni, ninahitimisha kwa kusema kwamba licha ya kuwa na vivutio vingi nchini kama vile mbuga za wanyama, maeneo ya kihistoria, malikale, milima, mabonde na vivutio vingine, Watanzania tuna kitu cha pekee cha kujivunia ambacho ni lugha yetu ya Kiswahili.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Alfred Leonard

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi