loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yasisitiza uchaguzi wa mitaa upo pale pale

IKIWA ni siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza kujitoa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Serikali imesisitiza kuwa uchaguzi huo uko palepale.

Pia, imewaonya viongozi wa vyama vya siasa na wananchi, wanaohamasisha fujo au kususia shughuli za maendeleo kwa njia ya mitandao, kuwa watachukuliwa hatua kali. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu na kampeni za uchaguzi zitaanza wiki moja kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara alitoa msimamo huo bungeni jana, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Singida Kaskazini, Justine Monko (CCM). Katika swali lake, Monko alisema Chadema kutangaza kujitoa, kunawakosesha wananchi haki yao kimsingi, hivyo alitaka kujua kauli ya serikali kutokana na kadhia hiyo.

Akijibu swali hilo, Waitara alisema taarifa ya Chadema kujiondoa kushiriki uchaguzi huo, wamezisikia kwenye mitandano na vyombo vya habari. Alisema hakuna tamko rasmi ambalo limefika ofisini kwake.

“Ni kweli na sisi kama ofisi tumesikia Chadema kujitoa, tumeona kwenye mitandao, huenda wakatoa tamko rasmi, lakini kauli ya serikali ni kwamba uchaguzi unaendelea kama ilivyopangwa kwenye ratiba, uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika Novemba 24 mwaka huu…wananchi ambao wamejiandikisha na vyama ambavyo vipo kwenye mchakato viendeleee na mchakato wao. Wametoa tamko jana (juzi) kwenye mitandao, lakini itakumbukwa kwamba kwenye taratibu zetu ni kwamba wale waliokuwa na malalamiko, wameandika mapingamizi yao na kesho (leo) ndio siku ya mwisho. Kama wamejiondoa hawana sababu yoyote ya kulalamika kwamba hawakutendewa haki,” alisema.

Aliongeza kuwa, “watu wenye sifa ya kutoa mapingamizi ni wagombea, wenzetu walitaka watoe kauli bungeni, kwenye mitandao ya kijamii, serikali inafanya kazi kwa karatasi kwa mawasiliano, hatuna document mezani hatuwezi kujadili.”

Aidha, Waitara alikemea maagizo yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na wananchi, ambao wanahamasisha wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo.

“Mwenye mamlaka ya kutoa maelekezo nchi hii ni Rais, na siyo kiongozi wa chama cha siasa, kiongozi wa chama cha siasa anatoa maelekezo kwenye chama chake na wanachama wake tu” alisema.

Waitara alitoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya, ambao ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama, kutafuta taarifa za watu wanaohamasisha fujo.

“Naomba nitoe maelekezo kwa wakuu wa wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama, tumepata taarifa kwenye mitandao wanahamasisha watu, wanaharibu mazao ya watu, wakuu wa wilaya popote mlipo kama kuna mtu anahisi hakutendewa haki kwenye uchaguzi huu na anafanya fujo mtaani, sheria stahiki zichukuliwe.

“Hatujawahi kutunga sheria katika Bunge hili inayosema ukigombea ukanyimwa nafasi au ukahisi umenyimwa haki ufanye fujo, ila zipo taratibu za kisheria mzifuate, msipozifuata vyombo vya usalama vinashughulika na wewe, tusilaumiane mbele ya safari” alisema.

Katika swali la msingi, Monko alitaka kujua kama serikali haioni umuhimu wa kuwepo uchaguzi mdogo, kama ilivyo kwa madiwani na wabunge. Akijibu swali hilo, Waitara alisema Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 (Kanuni ya 43 (1-4 na Kanuni ya 45), zinatoa fursa ya kufanya uchaguzi mdogo kujaza nafasi iliyoachwa wazi, endapo Mwenyekiti wa Kitongoji / Kijiji/Mtaa atafariki au kupoteza sifa za kuendelea kuwa katika nafasi hiyo kutokana na sababu zilizoainishwa kwenye Kanuni ya 44 (1 na 2). Alisema uchaguzi hautafanyika kama nafasi itakuwa imeachwa wazi, kabla ya miezi sita kabla ya uchaguzi.

Miongozo Baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge watatu walisimama kuomba mwongozo wa Spika kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa. Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) alitaka mwongozo wa kiti cha Spika, kuwa kanuni zinasemaje kwa chama kujitoa, hasa baada ya Chadema ambayo wabunge wake anawaamini na kuwaheshimu. Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) alitaka apewe ufafanuzi, endapo kama kuna chama kimejitoa, kanuni zinasemaje.

“Wakati Waziri wa Tamisemi akijibu swali namba 40 kuhusu suala la uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikajitokeza kwamba kwa sababu serikali ilitoa siku tatu kwa ajili ya kukata rufaa, kwa bahati mbaya chama ambacho nakiamini na kukiheshimu pamoja na wabunge wake, kimeamua kujitoa katika uchaguzi huo navishukuru vyama vingine kwa kuamua kusubiri siku ya mwisho ya rufaa kesho (leo)…Nilikuwa naomba kwa mujibu wa Kanuni za Serikali za Mitaa endapo kuna chama kimejitoa hata kwa kutokushemimu kikaamua kujitoa Kanuni inasemaje?” alisema Ndassa.

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM) alidai kwamba imekuwa kawaida kwa Chadema, kujitoa katika chaguzi mbalimbali, hivyo aliomba apatiwe ufafanuzi kuhusu chama hicho kujitoa.

“Mwongozo wangu unaotokana na swali namba 40, jana (juzi) Mwenyekiti wa Chadema ambaye tunamheshimu sana alitangaza kujitoa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hoja sio hiyo, kitendo cha kujitoa kinaendana na vurugu ambazo zinaendelea, Mheshimiwa Mwakagenda (Sophia) amesema amemfukuza mpangaji kutokana na hilo hilo.

“Jana (juzi) nimeona kwenye TV vijana wa Chadema Mbozi wameenda kufyeka shamba la msimamizi wa uchaguzi, vitendo hivyo vinaendelea nchi nzima. Mwenyekiti sisi wakongwe tuna historia ya chama hicho kugomea uchaguzi. Mwaka 2008 Chacha Wangwe alipotangaza kugombea uchaguzi Chadema nafasi ya mwenyejiti ilitokea tafrani.

“Mwaka 2015 Zitto Kabwe alipotaka kugombea uenyekiti wa taifa Chadema ilitokea tafrani mpaka wakamfukuza kwenye chama. Mwaka 2018 walipotakiwa kufanya uchaguzi wa mwenyekiti wa taifa waligomea mpaka sasa hivi wana barua nne za Msajili vya vyama vya siasa kutaka kugomea uchaguzi, kwahiyo tuna historia ya chama hiki kugomea chaguzi, kwahiyo naomba mwongozo wako Mheshimiwa Mwenyekiti,”alisema Mlinga.

Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonist (Chadema) alisema kwamba malalamiko yamezidi kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku Serikali ikiwa imekaa kimya. Alitaka apewe majibu kuhusu sekeseke hilo. Kauli ya Lugola Kutokana na miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge alitoa nafasi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alitoe ufafanuzi wa suala hilo, ambaye alisema Jeshi la Polisi limejipanga wakati wote wa kampeni hadi uchaguzi na limeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote nchini. Alisema polisi haitatoa mwanya kwa mtu yoyote, atakayejaribu kuvunja amani, ama kufanya vitendo vinavyoweza kuashiria kuvunjika kwa amani.

“Jeshi la Polisi limejipanga wakati wote, kuanzia kampeni hadi siku ya uchaguzi, hakuna mtanzania yoyote atakayefanya fujo ya kuzuru watu. Natoa onyo kwamba hakutakuwa na nafasi kwa chama chochote kitakachopanga kuvuruga amani, serikali tumejipanga kupambana na hali hiyo,” alisema.

Alisema atamuelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro aanze kuchukua hatua kwa wahusika, waliofyeka shamba la msimamizi wa uchaguzi wilayani Mbozi, pamoja na mbunge aliyemtimua askari katika nyumba yake aliyopanga. Wakati wa kipindi cha maswali, Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda alipopewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza alisimama na kusema: “Nimesimama kujibu swali la pili na nyongeza, nilikuwa na mpangaji ambaye ni askari nimemuondoa kwenye nyumba.”

Kwa upande wa Waitara aliongeza: “Kuna vyama 22 vyenye usajili, kwa hiyo kujitoa hakuzii kitu na nawapongeza waliobaki, na viongozi watakaopatikana watapelekwa kwenye mafunzo Chuo cha Hombolo.”

Mbunge wa Mtama, Nape Nnaye (CCM) alitaka kujua kama serikali haioni haja ya kuunganisha uchaguzi wa madiwani na vijiji, vitongoji na mitaa, ili uchaguzi wa wabunge na madiwani na rais uwe pamoja. Akijibu swali hilo, Waitara alisema jambo hilo ni la kisheria, hivyo wanapokea wazo hili ikiwezekana kufanya hivyo watafanya hivyo.

Vyama 11 kushiriki uchaguzi mitaa Katika hatua nyingine, Umoja wa Vyama 11 vya siasa visivyo na wawakilishi Bungeni, vimetangaza kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa na kuvikebehi vyama vilivyotangaza kuususia. Uamuzi huo ulitangazwa Dar es Salaam jana na Umoja huo unaoundwa na vyama vya DP, NRA, AFP, UDP, ADC, Demokrasia Makini, Ada-Tadea, Sauti ya Umma (SAU), TLP, CCK na UMB. Vyama hivyo vimesema vitashiriki uchaguzi huo, kwa kuwa ni wajibu wao wa kidemokrasia kufanya hivyo.

Vilisisitiza kuwa vyama vilivyosusia uchaguzi huo ‘vimeshiba’ “Vyama vilivyosusia vina mtaji wa wanachama, sisi katu hatuwezi kususia kwa sababu tunataka kutimiza matakwa ya demokrasia, waliosusia wana sababu zao za kufanya hivyo, kimsingi tunamuomba Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo aangalie mapungufu yaliyojitokeza kwa watendaji wake.

“Tunamuomba Waziri Jafo awarudishe katika mchakato wagombea wote ambao hakutendewa haki katika uteuzi ili tukapambane katika kura, tunaamini kufanya hivyo kutazidi kuinua demokrasi yetu hapa nchini,” alisema Mwenyekiti wa Umoja huo, Abdul Mluya.

Katibu wa Umoja huo, Hassan Almasi ambaye ni Katibu Mkuu wa NRA, alisema kimsingi chaguzi huendeshwa kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu, hivyo vyama vimetoa mapangamizi yao kuhusu kuenguliwa kwa majina ya wagombea na vinasubiri majibu ya rufaa ya wagombea wao.

“Vyama vimeundwa ili kushiriki uchaguzi, hatuwezi kususia kwa kuwa kushiriki chaguzi ndiyo hasa malengo ya kuanzishwa kwa vyama vya siasa, tunamuomba Waziri atoe maamuzi ya haraka ili tuweze kujua nini kifanyike,” alisema Almasi.

ACT–Wazalendo nayo yajitoa Wakati huo huo, Kamati ya Uongozi ya Chama cha ACT-Wazalendo iliyoketi jana, imeelekeza wanachama wake wote waliobakizwa katika uchaguzi huo wajiondoe. Taarifa ya Kiongozi wa Chama cha ACT –Wazalendo, Kabwe Zitto, ilieleza kuwa uenguaji wa wagombea kwa kutumia sababu zisizo na mantiki, umenyima wagombea haki yao kikatiba na pia umewanyima haki wananchi waliotimiza miaka 18 na zaidi.

Alisema haki hiyo ipo katika Ibara ya 5 ya Katiba. “Kwa kuwa CCM imeondoa wagombea wetu asilimia 96 na sisi tumewasaidia kuondoa asilimia nne ya waliobakia,” ilidai sehemu ya taarifa hiyo ya Zitto. Alisema chama cha ACT Wazalendo, kikiwa chama cha siasa makini chenye usajili wa kudumu nchini, kiliitikia wito wa kushiriki katika uchaguzi huo wa Mitaa, utakaofanyika Novemba 24, mwaka huu, kikiamini kuwa ni nafasi nyeti ya kuimarisha ushindani wa kisiasa nchini, lakini sasa kimeamua kujitoa.

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi