loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mipango, bidii ya kazi vilivyopaisha maendeleo China

KUANZIA mwaka 1978 China ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, imekuwa ni nchi yenye maendeleo ya kasi ambayo pato lake la ndani GDP limekuwa likiongezeka kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka, imewaondoa wananchi wake milioni 850 kutoka kwenye lindi la umaskini, imetimiza Malengo yote ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), na sasa imekuwa nchi ya pili kwa nguvu ya uchumi duniani.

Pamoja na kuwa kwa sasa kasi ya ukuaji wa uchumi wa China imepungua hadi asilimia 7 hivi, bado ongezeko lake la uchumi ni kubwa kuliko nchi nyingi duniani, na imekuwa ni injini kubwa ya ongezeko la uchumi duniani.

Hakuna mjadala kuhusu muujiza wa kiuchumi uliofanywa na China katika kujiendeleza, kwani dunia nzima imetambua na inaona kuwa China ya sasa, ni tofauti kabisa na China ya mwaka 1978.

Ni nchi yenye kundi kubwa kabisa la watu wenye mapato ya kati duniani, ni nchi ambayo kiwango cha maisha ya watu wake katika maeneo ya elimu, afya, lishe, makazi, usafiri na huduma nyingine za jamii kimeinuka kwa kiasi kikubwa.

Kimsingi hayo ndio mambo ya kupima kama nchi inapata maendeleo au la. Lakini swali lililopo sasa ni vipi China imeweza kufanya muujiza huo, ambao mbali na kunufaisha watu wake, pia umekuwa ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya dunia.

Tuangalie baadhi ya sababu kubwa zilizofanya China iweze kuwa na maendeleo ya kasi.

Sababu kubwa ya kwanza ni kuwa China ni nchi ambayo imekuwa na uongozi madhubuti ambao umeleta utulivu mkubwa wa kisiasa. Tangu China mpya ilipoanzishwa mwaka 1949, na hasa tangu mwaka 1978 ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, kwa ujumla imekuwa ni nchi yenye utulivu mkubwa wa kisiasa.

Utulivu huu uliweka mazingira mazuri kwa chama cha kikomunisti kupanga na kutekeleza sera za maendeleo ya uchumi bila kusita au kuyumba.

Licha ya kuwa awamu za viongozi katika ngazi mbalimbali za chama cha kikomunisti zimekuwa zikibadilika, mwendelezo wa utekelezaji wa sera umeendelea kuwepo.

Kila awamu inafanya mapitio ya utekelezaji wa sera zilizoamulia, na kuhakikisha zinatekelezwa na kuwa na ufanisi.

Sababu ya pili ni utekelezaji wa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, ambayo iliamsha nguvu ya uchumi wa China iliyokuwa imelala.

Kupitia sera hiyo, China ambayo wakati inaanza kutekeleza sera hiyo ilikuwa na uchumi unaosimamiwa na dola ambao pato lake kwa mwaka (GDP) lilikuwa ni dola za kimarekani bilioni 150, ilianza kuruhusu polepole nafasi ya soko katika kupanga mgawanyo na matumizi ya raslimali.

Polepole ukiritimba wa dola kwenye baadhi ya sekta za uchumi ulianza kupungua, na mitaji binafsi ilianza kuruhusiwa kuingia kwenye uchumi.

Kwenye sekta ya viwanda, kwa sasa karibu nusu ya viwanda vya China vinaendeshwa na mitaji binafsi, na nusu vinaendeshwa na serikali.

Kwenye upande wa uwekezaji, wachina waliokuwa wanaishi nje ya nchi, wageni wenye asili ya China na hata wale wasio na asili ya China, walianza kuruhusiwa kufungua biashara zao. Hali hii ilianza kuleta ajira mpya, ujuzi mpya na kuiongezea serikali mapato yanayotokana na kodi.

Sera hii imekuwa inatekelezwa kwa umakini mkubwa, kwanza katika maeneo madogo na kupima ufanisi na manufaa yake kwa nchi na wananchi.

Miji ya Pwani iliyopo Kusini na Mashariki mwa China ilikuwa ni ya kwanza kutekeleza sera za mageuzi na kufungua mlango, na serikali ya China, ilianzisha maeneo maalum ya kiuchumi ili kuhimiza utekelezaji wa mageuzi. Sababu ya tatu ni uwekezaji mkubwa kwenye viwanda vya kimkakati.

Viwanda vya kimkakati ni vile vilivyotajwa kuwa ni msingi wa maendeleo ya viwanda vingine au sekta nyingine. Kwenye miaka ya 90, China ilianza kujenga msingi wa upatikanaji wa nishati ya kutosha, kwa kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme kwa nishati ya maji na nishati ya nyuklia.

Kinu cha kwanza cha kuzalisha umeme kwa nguvu ya nyuklia kilianza kuzalisha umeme mwaka 1991 na sasa kuna jumla ya vinu 39, mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa nishati ya maji wa magenge matatu (Three Gorges Dam) ulianza kujengwa mwaka 1994 na kuanza kuzalisha umeme mwaka 2009, na kulikuwa na miradi kadhaa ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Hata hivyo hatua hiyo sasa inawekwa pembeni polepole kutokana na sababu za uchafuzi wa mazingira. Uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya nishati, viwanda vingine vya kimkakati kama vile vya kemikali na dawa, na chuma na chuma cha pua, umekuwa ni msingi mkubwa wa maendeleo ya viwanda vikubwa, ambavyo mpaka vinaendelea kuchochea maendeleo ya sekta nyingine.

Sababu ya nne ni kuwa China iliweka mpango kamili na wa muda mrefu wa uwekezaji kwenye sekta ya miundombinu.

Kwanza iliweka mpango wa kuunganisha mikoa yote na miji yote kwa njia za ndege, reli na barabara. Mawasiliano hasa ya njia ya reli na barabara yanachukuliwa kuwa ni sawa na mishipa ya damu kwenye uchumi.

Kwa sasa China ni nchi yenye mtandao mkubwa wa reli za kasi, barabara za mwendo kasi, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya biashara.

Maeneo yaliyokuwa nyuma kiuchumi yalifunguka na kunufaika na fursa za kiuchumi za maeneo yaliyotangulia kiuchumi kutokana na mawasiliano kwa njia ya reli na barabara. China pia imewekeza sana kwenye sekta ya usafiri wa anga.

Na kwa upande wa usafiri wa majini kwa sasa China ina bandari tano kati ya bandari kumi kubwa duniani. Mbali na sababu hizo za kisera na kiuchumi, kuna mambo mengine ya kijamii na utamaduni ambayo hayatajwi sana, ambayo pia ni vigumu kwa watu wasiowahi kuishi China kuyaelewa.

Mafunzo ya mwanafalsafa wa kale wa China Confucius, yamekuwa ni msingi mkuu wa utamaduni wa jadi wa China ambao umechangia sana kuwepo kwa maendeleo ya kasi.

Maadili haya yanagusa karibu maeneo yote ya maisha, ikiwa ni pamoja na kuchapa kazi, nidhamu ya kazi, moyo wa kubana matumizi, utii, nidhamu, heshima, moyo wa kujiendeleza kielimu na kusoma kwa bidii, moyo wa kupenda familia na hata moyo wa kupenda taifa.

Mchanganyiko wa mambo yote haya madogo madogo, umekuwa na mchango mkubwa katika kuwafanya wachina wawe na namna ya kufikiri inayofanana, na kuweza kutekeleza kwa pamoja maagizo na sera zinazoamuliwa na serikali.

Hali hii ni tofauti na nchi nyingine hasa za Magharibi, ambapo mambo hayo yanatajwa kama ni mambo binafsi na si ya pamoja, na watu wanaweza kupinga, kukosa, kupuuza na hata kukataa maagizo ya serikali.

Sababu nyingine muhimu ya China kuwa na maendeleo ya kasi ya uchumi ni ushiriki mkubwa wa wanawake katika mambo ya uchumi, iwe ni uchumi wa familia au uchumi wa taifa.

Tangu Jamhuri ya Watu wa China ilipozaliwa mwaka 1949, hadhi ya wanawake katika jamii ya China iliinuka, baada ya kukombolewa kutoka kwenye mila za jadi kandamizi. Sehemu kubwa ya wanawake wa China wameweza kuwa na fursa sawa na wanaume, na kuweza kuonesha mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Utekelezaji wa Sera ya Mtoto mmoja (1979-2015), si kama tu ulisaidia familia kutokuwa na mzigo mzito wa kuugharamia kama familia zenye watoto wengi, bali uliwapa wanawake wa China muda zaidi wa kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi, na si kutunza watoto peke yake kama ilivyokuwa zamani.

Kuna sababu nyingine ambazo zimetokea katika miaka ya hivi karibuni baada ya China kuwa na maendeleo.

Wakati China inaanza kutekeleza sera ya mageuzi ilikuwa ni mpokeaji mkubwa wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI), lakini sasa uwekezaji unaoingia kutoka nje na uwekezaji inaoufanya China nje ya nchi unakaribia kuwa na uwiano.

Uchumi wa China pia umeanza kuwa na vyanzo vingi tofauti na zamani, ambapo ulitegemea zaidi uuzaji nje wa bidhaa za viwandani.

Sasa kuna maendeleo makubwa ya mambo ya utafiti (R&D), sekta ya mawasiliano ya habari, na hata mwelekeo wa vichocheo vya ongezeko la uchumi unaanza kulenga soko la ndani, hasa baada ya mazingira ya nje ya nchi kutokuwa na uhakika.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalum

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi