loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Finland kutoa bil 24/- mradi Panda Miti Kibiashara

SERIKALI ya Finland inatarajia kutoa Euro 9.5 sawa na Sh bilioni 24/- kwa ajili ya mradi wa awamu ya pili wa Panda Miti Kibiashara.

Mradi huo utakaodumu kwa miaka minne ni kwa ajili ya wakulima wadogo wa miti wa mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu aliagiza Idara ya Misitu na Nyuki ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa mradi huo kwa niaba ya Wizara, iweke utaratibu wa kusimamia na itoe taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo yake kwa wizara.

Aliwataka wataalamu wote watakaotekeleza mradi huo, wafanye kazi kwa weledi mkubwa, kwa kuzingatia thamani ya fedha hiyo .

Ametoa kauli hiyo  Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa alipokuwa akizindua awamu ya pili ya mradi huo.

Awali serikali hiyo ya Finland katika mradi wa awamu ya kwanza, kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2018, ilitoa Euro milioni 19.5 sawa na Sh billioni 40.

Kupitia uwezeshaji huo, hekta 12,000 za miti bora zimepandwa na zinamilikiwa na wananchi wapatao 9,030.

Katika awamu hiyo ya kwanza, fedha hizo zilitumika kuanzisha kituo cha mafunzo ya misitu na Kiwanda cha Misitu cha Mafinga.

Kituo hicho mpaka sasa kimeshatoa mafunzo kwa wakulima wapatao 8,555. Akizungumzia lengo la matumizi ya fedha hizo za awamu ya pili ya mradi, Kanyasu alisema fedha hizo zitatumika kuwajengea uwezo wakulima wa miti na wajasiriamali wadogo na wa kati

Alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kupambana na matukio ya moto na kuongeza ubora wa mazao ya misitu yaliyo kwenye mnyororo wa thamani.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo aliishukuru Finland kwa kufadhili mradi mwingine wa kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya misitu uitwao FORVAC, unaotekelezwa na wizara katika wilaya kumi za mikoa ya Tanga, Dodoma, Lindi na Ruvuma.

Alisema sekta ya misitu nchini isingefika hapa ilipo leo, kama hapangekuwepo msaada wa wananchi wa Finland. Balozi wa Finland nchini Tanzania, Riita Swan alisema nchi yake imeatoa fedha hizo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wadogo wa miti ili wajikwamue na umasikini.

Kwamba Finland inataka kuona wakulima wadogo wa miti, wanajengewa mazingira mazuri ya kushiriki katika shughuli za kuendeleza misitu kibiashara.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi