loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali kumsomesha yatima hadi chuo kikuu

SERIKALI imesema itamgharamia masomo yake hadi elimu ya juu Anna Zambi aliyefiwa na wazazi wake na wadogo zake watatu kwenye ajali ya gari Oktoba 26 mwaka huu wilayani Handeni mkoani Tanga.

Mbali na kumsomesha, Serikali pia itahakikisha mtoto huyo anaendelea kupatiwa msaada wa kisaikolojia pamoja na kuhakikisha kuwa haki zake zote zinalindwa.

Wakati Serikali inatoa ahadi hiyo, kuanzia sasa Anna atakuwa anaishi na mama yake mdogo mkoani Arusha.

Anna ambaye amemaliza mitihani ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mother Theresa of Calcutta mwishoni mwa wiki, amejikuta yatima baada ya Baba yake, Lingston Zambi, Mama yake, Winfrida Lyimo pamoja na wadogo zake, Lulu, Andrew na Grace kupoteza maisha baada ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda kwenye mahafali yake kusombwa na maji.

Hayo yalibainishwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk John Jingu alipofika kumfariji na kumpa pole mtoto huyo nyumbani kwa wazazi wake Goba jijini Dar es Salaam.

Dk Jingu ambaye aliongozana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu na Maofisa Ustawi Jamii, alisema serikali haitamwacha Anna bali itahakikisha inampatia msaada wote wa kisaikolojia na kimasomo mpaka hapo atakapofikia ndoto zake za kimaisha.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya, aliitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto kuhakikisha haki zote za mtoto huyo hazipotei. Alisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha maendeleo na ustawi wa mtoto huyo yanalindwa.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Lissu, alisema kwa kuwa ndoto ya Anna ni kuwa Mwanasheria, hivyo serikali itahakikisha inamtafutia shule nzuri ya bweni yenye mchepuo wa masomo ya Historia, Kiswahili na Kiingereza (HKL) ambayo yatamfaa kwa ajili ya kusoma masomo ya sheria atakapofika chuo kikuu.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kunenge, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema Serikali ya Mkoa itahakikisha inakuwa karibu na mtoto huyo ili kuhakikisha hakuna changamoto yoyote inayoweza kumtikisa.

Baada ya maelezo hayo, Anna aliishukuru serikali kwa kuahidi kumsaidia, naye alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa atasoma kwa bidii ili aweze kufikia ndoto yake ya kimaisha.

Aenda kuishi

Arusha Katika hatua nyingine, Mama Mdogo wa Anna, Isabela Lyimo amekubali kubeba jukumu la kumlea mtoto huyo mpaka hapo atakapokuwa mtu mzima na kujitegemea.

Isabela ambaye anaishi Arusha, ataondoka na Anna kesho kwa ajili ya kuanza rasmi jukumu la kumlea.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Ibrahim Zambi ambaye ni Wakili kitaaluma, alisema familia ilimpa Anna uhuru wa kuchagua nani amlee, ndipo alipoamua kumchagua mama yake mdogo.

Anna atarudi Dar es Salaam mwisho mwa mwezi huu kushiriki Ibada ya Misa ya kuwaombea Marehemu Wazazi wake na ndugu zake ambapo wanafunzi na uongozi wa shule aliyosoma watashiriki pia.

WAANDAAJI wa Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) Kanda ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi