loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

UDSM kutahini ujuzi lugha ya Kiswahili

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema kitaanza kutoa mitihani ya kimataifa ya ujuzi wa Lugha ya Kiswahili kuanzia mwezi huu.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye, amesema hayo katika Mahafali ya 49 ya UDSM yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Katika mahafali hayo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ambaye pia ni Mkuu wa chuo hicho, Jakaya Kikwete aliwatunuku shahada za uzamivu, uzamili, shahada ya awali, stashahada na vyeti wahitimu wa fani mbalimbali.

Wahitimu 8,313 wakiwemo wanawake 3,201 sawa na asilimia 38.5 wamefuzu na kuhitimu mwaka huu.

Kikwete alimtunuku cheti mwanafunzi bora wa jumla kitaaluma aliyehitimu kwa ufaulu wa kiwango cha ufaulu (GPA) 4.8 wa shahada ya awali katika elektroniki na mawasiliano, Anold Matemu. Profesa Anangisye alisema:

“Kitakuwa chuo kikuu cha kwanza duniani kutunga mitihani hii, kusimamia utahini na usahihishaji wake na mwishowe kutoa cheti cha kimataifa kinachoonesha kiwango cha ujuzi wa mtahiniwa.”

Akaongeza: “Hii ni kutokana na ukweli kuwa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni chuo pekee chenye taasisi ya kale zaidi katika masuala ya Kiswahili; Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika taaluma za Kiswahili, na kina uhusiano mzuri wa kitaaluma na vyuo vingi vinavyojihushughulisha na ufundishaji wa Kiswahili.”

Makamu Mkuu wa chuo huyo alisema UDSM inajivunia mafanikio mbalimbali yakiwamo ya Chuo cha Madini Dodoma kuwa sehemu ya chuo kikuu hicho baada ya kukabidhiwa na Wizara ya Madini ili kiwe Chuo kishiriki kuanzia Mwaka wa Masomo wa 2019/2020.

Mwenyekiti wa Baraza la UDSM, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema wanamuahidi Rais John Magufuli kusimamia na kukuza ubora wa elimu kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazingatiwa. Rais Magufuli hakuwepo katika mahafali hayo.

“Pia, tutasimamia kwa ukamilifu fedha zote zinazotolewa na serikali na zitokanazo na vyanzo vya ndani vya mapato ya chuo,” amesema.

Mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (Phd) katika Jiografia, Mary Mtumwa Khatib, alisema atatumia elimu aliyoipata kufanya utafiti utakaoleta majawabu katika jamii dhidi ya changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchi.

WATOTO 84,625 waliokuwa na utapiamlo mkali, wametibiwa kuanzia mwanzoni mwa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi