loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkapa: Mawaziri hawa waliniumiza kichwa

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa ameelezea namna alivyoendesha baraza lake la kwanza la mawaziri tangu achaguliwe kuwa rais mwaka 1995, aliloliita askari wa miavuli na namna alivyojikuta akiwataka mawaziri wanne, wajiuzulu kutokana na makosa mbalimbali.

Pia, Mkapa aliyeapishwa kwa mara ya kwanza urais Novemba 23, mwaka huo 1995, alieleza namna anavyojivunia marais wawili wa Tanzania, ambao ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli waliokuwa ndani ya baraza lake la kwanza la mawaziri.

Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Mkapa, wakati Magufuli alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye Waziri wa Ujenzi katika Serikali hiyo ya Mkapa.

Hayo yalielezwa na Mkapa kupitia kitabu chake cha “My Life My Purpose”(Maisha Yangu, Kusudi Langu), ambacho kinaelezea historia ya maisha yake, kuanzia alivyozaliwa hadi historia yake ya siasa.

Alieleza namna alivyowataka mawaziri wanne wajiuzulu, watatu katika awamu yake ya kwanza, ambapo hata hivyo baadaye alimtaka aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Juma Ngasongwa kuendelea na uwaziri wake baada ya uchunguzi dhidi yake kumsafisha.

“Nilimtaka Waziri wangu wa Fedha, Simon Mbilinyi na Naibu wake Kilontsi Mporogomi kuondoka kwa kuwa kila mara walikuwa wakigombana, jambo ambalo sikuweza kuliruhusu,” alibainisha.

Alisema Waziri wa Viwanda na Biashara, Idd Simba wakati huo naye alijiuzuli katika kipindi cha awamu ya pili, kwa kuwa alishindwa kutofautisha ukuzaji wa biashara ya serikali na mambo yake binafsi.

Aidha, alieleza kuwa Waziri wa Nchi, Dk Hassy Kitine naye aliondoka madarakani, baada ya kubainika kuwa mkewe alitoa maelezo ya uongo katika madai yake ya malipo ya tiba akiwa Amerika ya Kaskazini.

Alisema “Kiongozi ukionekana ni mtu unayeweza kufikiwa kiurahisi ni muhimu, lakini pia kuna changamoto kuweza kufikia mipango yako ya maendeleo kwani kuna wengine wanaweza kutumia mwanya huo kukukandamiza.

“Unaweza kusikiliza ushauri wa mtu, halafu akiondoka anakwenda kuwaambia wengine Oooh unajua nimemwambia Rais… kwa hiyo nikajifunza kuwa makini na watu ninaojihusisha nao na ninaowaomba ushauri. Lakini pia nikajifunza kuwa wengine unaweza kuwauliza kitu ili wakuridhishe wanakujibu kile unachotaka kusikia, jambo ambalo halimsaidii kiongozi,”alisema.

Alisisitiza kuwa “Ukweli ni kwamba sikuwa na mtu yeyote ninayempendelea katika baraza langu. Wote niliwaita askari wa miavuli, niliwapa maelekezo na waliyatekeleza.

“Pia nilikuwa na manaibu wazuri sana katika timu yangu ya mawaziri, walikuwa wanafanya kazi nyingi na nzito sana kama punda. Baadhi yao wamepiga hatua kubwa leo hii akiwemo Rais John Magufuli ambaye ni Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano na Rais mstaafu Kikwete,” alieleza.

Alisema Rais Magufuli katika serikali yake hiyo, alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye akawa waziri kamili katika wizara hiyo. Rais Kikwete ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa vipindi vyote viwili vya utawala wake, baadaye ndiye aliyemrithi kiti chake cha Urais, na kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Pamoja na hayo, kiongozi huyo pia alibainisha kuwa katika uongozi wake, alikuwa wazi kwa mawaziri wake, kuhakikisha wanatambua mipaka ya mamlaka zao, wapi pa kutumia mamlaka hizo na wapi pa kutozitumia. Alisema alikuwa muwazi kwa mawaziri wake, jambo ambalo anashukuru pia kuwa hata marais waliomfuatia, Kikwete na Magufuli, wamelitekeleza.

“Nilijifunza kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere jinsi ya kusikiliza na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanyia kazi,” alisema.

Aidha, katika kitabu hicho Mkapa alieleza namna alivyokuwa akiendesha serikali yake hiyo, ambapo kila asubuhi ilikuwa lazima asome magazeti yote na endapo atakutana na jambo linalomkwaza, huwasiliana na waziri husika kujieleza.

“Mawaziri kwa haraka walijifunza namna ya kujiandaa kupokea simu zangu kila siku. Pia walijifunza kuwa siwezi kukubali taarifa inayowasilishwa kwenye baraza mpaka iwe imeandaliwa vizuri. Nilitegemea kila waziri atakutana na katibu wake mkuu na wafanyakazi wake waandamizi kuandaa taarifa hiyo kikamilifu,” alisisitiza.

Aidha, alibainisha kuwa pia alipenda akiwa ofisini kwake Ikulu, kuingia kwenye ofisi mbalimbali muda wowote, jambo lililowaweka wafanyakazi kuwa makini muda wote. Kwa sasa Rais Magufuli amekuwa na mtindo wa kufanya ziara za kushtukiza kwenye ofisi mbalimbali za serikali yakiwemo mashirika ya umma.

Tayari alishashtukiza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Vilevile Mkapa alielezea namna alivyonusurika kifo katika kampeni zake za uchaguzi wa kuwania nafasi ya urais mwaka 1995, baada ya kukumbana na hali mbaya ya hewa wakati ndege waliyopanda ilipotaka kutua Ifakara, mkoani Morogoro.

“Pamoja na jitihada na ujasiri wa rubani kuituliza ndege, kadiri tulivyokuwa tunashuka ndivyo ndege hiyo ilionekana kukataa kutoa ushirikiano.

“Kwa kweli ilikuwa inaogopesha pale tulipokuwa bado angani, lakini hata ndege ilipotua ardhini hali ilikuwa mbaya zaidi. Ardhi ilikuwa inateleza, hivyo ilikuwa ni vigumu kuidhibiti ndege hiyo. Tukiwa katika hali hiyo iliyoonekana kuwa haidhibitiki hatimaye ndege ilisimama,” alieleza.

Alisema baadaye wakati wakijiandaa kupaa na kuondoka eneo hilo, rubani aliwatahadharisha na kuwaambia kuwa wajiandae, kwani hali ya kupaa inaweza kuwa mbaya kuliko waliyokutana nayo wakati wa kutua.

“Tulipokuwa angani rubani wetu alituambia kuwa wakati wakijiandaa kupaa kulikua na shimo katika njia ya ndege, hivyo ilibidi ainyanyue ndege mapema zaidi kulikwepa shimo hilo, kwani lingeweza kuipindua ndege. Kwa kweli siku ile tulikuwa na bahati sana,” alisema.

Alisema waliendelea na kampeni kama kawaida hadi pale Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposikia kuwa menejimenti ya kampeni imepanga kukodisha helikopta ili kuyafikia maeneo mengi zaidi. Alisema Mwalimu Nyerere alikasirika na kumpigia simu Meneja wa Kampeni, Ferdinand Ruhinda ambaye wakati huo alikuwa ametoka, lakini aliwasilisha maoni yake kwa msaidizi wake.

UZALISHAJI wa chakula umeimarika na hivyo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi