loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

CCM yapita bila kupingwa mikoa 3

NAIBU Waziri wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara ametangaza rasmi kuwa wagombea wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepita bila kupingwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika mikoa mitatu nchini ya Tanga, Katavi na Ruvuma.

Kwa mantiki hiyo, chama hicho tawala hakitafanya kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizoanza juzi. Waitara alibainisha hayo katika mahojiano maalumu, yaliyorushwa mbashara jana na Shirika la Utanganzaji Tanzania(TBC) kupitia kipindi chake Jambo Tanzania.

"Mikoa 23 kati ya 26 iliyopo Tanzania Bara itaendelea na kampeni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hadi Novemba 23 mwaka huu, taarifa zilizopo ni kwamba mikoa mitatu wagombea wote wa CCM kuanzia vitongoji, mitaa na vijiji wametangazwa washindi baada ya kupita bila kupingwa katika maeneo yao,"alieleza na kuongeza: "Katika mikoa hiyo mitatu walikuwepo wagombea wa vyama vingine vya siasa lakini baadaye wakajitoa kwenye kinyang'anyiro" alisema.

Aidha alisema kuwa kati ya halmashauri 185, wagombea katika halmashauri 94 nchini wamepita bila kupingwa, huku kati ya vijiji 12,319 wagombewa wa vijiji 1,000 wamepita bila kupingwa, ambapo kati ya mitaa 4,000 wagombea wa mitaa 188 wamepita bila kupingwa. Mkoani Shinyanga, wagombea kupitia CCM wameonekana kuanza kampeni, huku vyama vya upinzani vikiendelea kususia.

Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Shinyanga, Rebeka Magoma alianza kampeni hizo kwa kuwataka vijana kuacha tabia ya kufanya fujo kwenye kipindi cha kampeni pamoja na siku ya upigaji kura Novemba 24 mwaka huu.

Magoma alibainisha hayo juzi wakati akizindua kampeni ya uchaguzi huo kwa wagombea wa CCM kwenye Kata ya Kambarage Shinyanga Mjini. Mkutano huo ulifanyika katika Mtaa wa Jomu mjini humo.

Diwani wa Kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga, Hassani Mwendapole aliwataka wananchi kuwapuuza watu ambao wamekuwa wakizusha kuwa wagombea wa CCM wamependelewa, na kubainisha kuwa wao walifuata maelekezo ya namna ya kujaza fomu na ndio maana hawa kukatwa majina yao.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo mkoani Shinyanga, Siri Yasin alisema kuwa wao hawatashiriki kwenye kampeni wala kupiga kura katika uchaguzi huo, kama msimamo wao unavyowataka. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Shinyanga, Emanuel Ntobi alisema wao kama walivyoazimia, hawashiriki katika kampeni wala upigaji kura.

Mkoani Mbeya, CCM imesema utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi, utakuwa ndiyo mizani itakayotumika kuwapima viongozi wa serikali za mitaa waliopita bila kupingwa. Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mashango alipokuwa akifungua kampeni kuwatambulisha wateule wa Kata ya Itezi jijini Mbeya.

Alisema ushindi ambao Chama cha Mapinduzi kimepata ni ishara kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwakani, hivyo aliwataka wenyeviti na wajumbe kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri ili mkoa wa Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, viweze kuchukuliwa na CCM. Kwa Halmashauri ya jiji la Dodoma, wagombea wa CCM katika mitaa 219 wamepita bila kupingwa.

Kwa upande wake, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) kimesema kinashangazwa na uwepo wa washiriki kutoka chama hicho, ilihali walishajitoa. Kimesema labda wanaodaiwa kushiriki katika kampeni kwa ajili ya uchaguzi, wanatokea katika chama kipya.

Katika Manispaa ya Sumbawanga, imedaiwa wagombea wa chama hicho hawajajitoa, hivyo kushiriki katika uchaguzi, wakati chama hicho kilishadai kujitoa na kutoshiriki katika uchaguzi. Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mamboya Nje wa Chadema, John Mrema alisema hayo jana jijini Dar es Salaam. Alisema tayari wamemwandikia barua Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo kuhusu kujitoa kushiriki uchaguzi.

Alisema katika Manispaa ya Sumbawanga walikuwa na wagombea 182, ambao wote walienguliwa wakati wa kurejesha fomu, jambo linalowashangaza uwepo wa wanaoshiriki uchaguzi hivi sasa. Nacho Chama cha Demokrasia Makini kimesema kinatarajia kuzindua rasmi kampeni zake za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kimeahidi kuwa kitaibuka na ushindi wa ‘kisulisuli’ katika maeneo yote ambayo kimesimamisha wagombea. Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mohammed Abdullah wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kampeni hizo.

Alisema chama hicho hakina mpango wa kususia uchaguzi, badala yake kimeamua kuelekeza nguvu zake kuwapigia kampeni kabambe wagombea wake zaidi ya 80 waliopo nchi nzima ili waweze kuibuka na ushindi. Alitaja mikoa ambayo chama hicho kimesimamisha wagombea kuwa ni Morogoro, Mara, Tabora, Kigoma na Dar es Salaam.

MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania anayefanya shughuli zake Marekani, Flaviana ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi