loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwalimu adai mimba nyingine zinapatikana kwenye makanisa

VIONGOZI wa dini wametakiwa kuangalia suala la kushirikisha wanafunzi kwenye kwaya kutokana na waimbaji na walimu wa kwaya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi ambao wengine hupata ujauzito.

Kauli hiyo ilitolewa juzi wakati wa mkutano wa majadiliano kwenye mradi wa Sauti Yangu unaotekelezwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Woman Wake Up (Wowap) kwa ufadhili wa Shirika la Child Fund Korea kupitia Jukwaa la Haki za watoto.

Mwalimu wa shule ya sekondari ya Mpwayungu Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Omar Amos alitaka kuangaliwa kwa suala la wanafunzi kushiriki kwenye kwaya za makanisani.

Alisema kumekuwa na kawaida ya kushirikisha wanafunzi kwenye makongamano, matamasha ya uimbaji na mikutano mbalimbali lakini mazingira mengi yamekuwa si salama kwao. Alisema kwenye kwaya wanafunzi wanapewa mimba na walimu wa kwaya na kuna mwanafunzi tayari amefukuzwa shule kwa kupewa mimba na mwalimu wa kwaya na sasa mwalimu huyo amekimbia na hajulikani alipo.

“Waacheni watoto waimbe kwaya za shuleni kama mnawahitaji kwenye kwaya zenu wasubirini wamalize masomo, kuna wakati wanafunzi walikuja kuombewa ruhusa wanakwenda kwenye uimbaji Singida tukajiuliza usalama wa wanafunzi ukoje, watakwenda kulala wapi? Na mazingira wanayofikia yakoje na kama ni salama kwao, hatukupata majibu,” alisema.

Aliwataka viongozi wa dini kupunguza kuwatumia wanafunzi walio shuleni kwa ajili ya uimbaji kwani baadhi ya kwaya wacheza shoo wote ni wanafunzi. “Viongozi wa dini wanatakiwa kwapunguzia wanafunzi majukumu ya kanisani, mimba nyingine zinapatikana makanisani kwenye kuimba kwaya” alisema. Kwa upande wake Mtendaji wa kijiji cha Mpwayungu, Selemani Kibakaya alisema kunatakiwa kuangaliwa chanzo cha tatizo. Alisema suala la mikesha ya kanisani kwa wanafunzi si changamoto au tatizo.

“Wanafunzi wengine wanaaga wanakwenda kwenye mikesha lakini hawafiki makanisan,i cha kufanya si kuzuia mikesha changamoto iko kwa wazazi, jamii ya Dodoma wazazi wengi hawakai na watoto wao na kuwaambia ukweli,” alisema.

Alisema kwenye baadhi ya familia watoto wana sauti kuliko wazazi hivyo hawawezi kuhoji chochote.

“Kwenye ndoa za Kigogo ngoma zinapigwa usiku kucha, viongozi wa dini waendelee kuhakikisha wanatoa elimu na kukemea masuala yasiyo ya maadili kwa watoto,” alisema.

Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Mpwayungu, Stella Yohana aliwataka wazazi kutoa mahitaji muhimu kwa watoto hasa chakula na mavazi.

Alisema watoto wengi wamekuwa wakiachwa bila msaada, hali ambayo imekuwa ikiwafanya waingie kwenye vitendo vya ngono. Mchungaji Jackline Munisi wa kanisa la Ufufuo na Uzima Mpwayungu alitaka viongozi wa dini kuwasaidia watoto wanaotoka mazingira magumu ili kupata mahitaji muhimu ya maisha kama vyakula, mavazi na vifaa vya shule.

SIKU moja baada ya pazia la uchukuaji fomu za Urais ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Chamwino

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi