loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Stars kuwapa raha Watanzania leo

BAADA ya wiki iliyopita timu ya taifa, Taifa Stars kufanikiwa kukonga nyoyo za Watanzania kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea ya Ikweta nyumbani, leo tena timu hiyo inajitupa dimbani nchini Tunisia kutafuta ushindi dhidi ya Libya.

Huo utakuwa ni mchezo wa pili kwa Stars katika Kundi J wakiwania kufuzu kushiriki michuano ya Afcon 2021 nchini Cameroon. Tayari Stars imetua Tunisia kwa ajili ya mchezo huo tangu juzi ikiwa imeshajifua kwa ajili ya kuondoa uchovu wa mchezo wao dhidi ya Guinea ya Ikweta na jana walifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa katika Jiji la Monastir. Libya inacheza mechi zake za nyumbani Tunisia kutokana na hali ya usalama kwa sasa nchini kwao.

Hali hiyo inazipa nafasi sawa Tanzania na Libya kwani zote ni timu ngeni nchini Tunisia na hivyo kutoa fursa na kupunguza presha ya mchezo kwa Stars, kitu ambacho kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije hakipi nafasi kubwa.

“Hata kama (Libya) hawapo kwenye ardhi yao haiwezi kufanya mchezo kuwa mwepesi au usio na mwenyewe. Maana wao wamekuwa wakikaa pale na kufanya kila kitu hapo, kwa hiyo kimazingira wao ndiyo wenyeji na wamezoea hapo, kikubwa ni kuendelea na maandalizi mazuri na kujipanga na mechi hiyo kikamilifu.

“Kuhusu maandalizi yapo sawa na wachezaji wapo kwenye ari kubwa, tunahitaji kuanza mechi hii kama tulivyomaliza iliyopita ili tuendelee kujiweka katika sehemu nzuri zaidi ya kwenda Afcon kwa mara nyingine,” alisema Etienne Ndayiragije.

Katika Kundi J, Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu, sawa na Tunisia inayoongoza kundi kutokana na kufunga mabao mengi. Guinea ni ya tatu na Libya ya mwisho.

Kama Stars itafanikiwa kufuzu Afcon, hii itakuwa mara ya pili mfululizo kushiriki michuano hiyo baada ya kufanya hivyo mwaka huu nchini Misri, Stars iliposhiriki mara ya kwanza Afcon baada ya miaka 39 kupita.

Mbali na nahodha wa Stars, Mbwana Samatta (pichani) kueleza kwamba wapo tayari kwa mapambano hii leo akiamini wachezaji wenzake kuwa kwenye hali nzuri ya kushindana lakini kipa wa timu hiyo pia, Juma Kaseja amesisitiza mashabiki wa timu hiyo kuwaombea waibuke na ushindi katika mchezo huo anaoamini utawaweka katika nafasi kubwa zaidi ya kwenda Afcon.

“Awali nilisema mitihani migumu tuliyonayo ni hizi mechi mbili za kwanza, ambazo moja tumeshinda na sasa tunaitazamia hii nyingine, cha msingi Watanzania watuombee dua, tufanikiwe pia na mechi hii ili tuzidi kukaa sawa kuelekea Afcon kwa mara nyingine,” alisema Kaseja.

foto
Mwandishi: Hans Mloli

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi