loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali katika safari ya kuongeza uzalishaji sukari

MWAKA jana, Rais John Magufuli alipozungumza na wafanyabiashara jijini Dar es Salaam, pamoja na masuala mengine, aliwataka kuwekeza katika viwanda vya sukari kuziba nakisi inayosababisha kuagizwa kwa sukari kutoka nje ya nchi.

Vile vile Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hivi karibuni kilitaja sekta ya sukari kwamba ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji kuongezwa kasi ya uwekezaji kwa kusema yapo mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo ikilinganishwa na inayozalishwa.

Hivi karibuni, gazeti hili limefanya mahojiano na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Profesa Joseph Buchwashaija kufahamu mikakati inayoendelea kuhakikisha sukari inazalishwa kwa wingi ili Tanzania iondokane na utegemezi wa sukari ya ziada kutoka nje.

Swali: Kuna viwanda vingapi vya sukari nchini kwa sasa?

Jibu: Tasnia ya sukari nchini ina viwanda vitano vinavyozalisha sukari; Vikubwa vinne na cha kati kimoja. Viwanda hivyo ni Kilombero na Mtibwa vilivyopo Morogoro, Kagera kilichopo Kagera, TPC Ltd kilichopo Kilimanjaro na Manyara Sugar Company kilichopo mkoani Manyara.

Swali: Mahitaji na uzalishaji wa sukari nchini ukoje?

Jibu: Mahitaji ya sukari yamekuwa yakibadilika mwaka hadi mwaka kulingana na hali halisi ya mahitaji kwa mwaka husika. Mathalani, kwa mwaka 2019/20 mahitaji ya sukari yanakadiriwa kuwa tani 710,000. Kati ya hizo, tani 545,000 ni sukari ya matumizi ya nyumbani na tani 165,000 ni kwa matumizi ya viwandani. Makadirio ya uzalishaji wa sukari kwa viwanda vyote kwa mwaka 2019/20 ni tani 378,449 sawa na asilimia 67.7 ya sukari inayokadiriwa kwa matumizi ya nyumbani.

Swali: Uzalishaji wa sukari ukoje katika kila kiwanda?

Jibu: Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kinaendeshwa na Kampuni ya Sukari Kilombero inayomilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Sukari ya Illovo kwa asilimia 75 na serikali asilimia 25. Mwaka 2017/2018, kiwanda kilizalisha tani 118,511 za sukari.

Kina shamba lenye ukubwa wa ekari 10,000 na pia kimeingia mikataba na wakulima wa nje 6,500 wanaomiliki ekari 13,000 za mashamba. Kwa mwaka 2018/19 kiwanda kilizalisha tani 134,035 za sukari na kimepanga kuongeza mitambo yenye uwezo wa kuchakata miwa kutoka tani za miwa 110 hadi 310 kwa saa.

Vile vile kitaongeza idadi ya wakulima wadogo kutoka 6,500 hadi 12,000 ambao watachangia ongezeko la uzalishaji wa tani 130,000 za sukari hadi tani 265,000. Kiwanda cha Tanganyika Planting Co. Ltd (TPC Ltd) kinamilikiwa kwa ubia kati ya Sukari Investment Co. Ltd (SIL) ya Mauritius inayomiliki asilimia 75 na serikali ni asilimia 25.

Kina eneo la hekta 16,000 na kati ya hizo, hekta 8,000 hulimwa na huzalisha wastani wa tani 100,000 za sukari kwa mwaka. Mwaka 2018 kiliwekeza Sh bilioni 200 kwa ajili ya uboreshaji zaidi wa kiwanda ikiwamo miundombinu ya kisayansi ya kuondoa chumvi kwenye shamba la hekta 400 ili kuongeza eneo la uzalishaji. Uzalishaji katika mwaka 2017/18 ulikuwa tani 91,487 na umeendelea kuongezeka hadi tani 104, 399 katika msimu wa 2018/2019.

Kiwanda cha Sukari cha Kagera kina eneo la hekta 15,876 ambazo kati yake, hekta 13,869 zinamilikiwa na kiwanda na hekta 2007 ni za wakulima. Uzalishaji wa sukari umekuwa ukiongezeka kila mwaka katika kiwanda hiki kutoka tani 35,362 msimu wa 2011/12 hadi tani 75,569 msimu wa 2017/18. Hali hii ilitokana na kuimarishwa kwa uzalishaji wa kilimo cha miwa cha umwagiliaji na kuboresha uwezo wa kiwanda wa kuchakata miwa.

Kiwanda kinalenga kuzalisha tani 99,500 ifikapo mwaka 2020/21. Kiwanda cha Sukari Mtibwa kinamilikiwa na Kampuni ya Mtibwa Sugar Estates kwa asilimia 100. Kwa msimu wa 2018/19, kilizalisha tani 31,139 za sukari.

Kina mpango wa kuongeza eneo la uzalishaji wafikie tani 65,000 za sukari. Pia kipo kiwanda cha Sukari Manyara ambacho ni cha kati chenye uwezo wa kuzalisha tani takribani tani 5,000 . Katika msimu wa 2018/19, kiwanda kilizalisha tani 5,191.32 za sukari.

Kutokana na uwiano hasi kati ya uzalishaji na mahitaji ya sukari nchini, serikali imeweka utaratibu wa kuingiza sukari nchini baada ya mapitio ya uhitaji halisi na kutoa vibali vya kuingiza nchini. Swali: Mwenendo wa uingizaji wa sukari ukoje?

Jibu: Mwenendo wa uingizaji wa sukari kwa kipindi cha miaka mitano kwa sukari ya kawaida ni jumla ya tani 545,488.75. Mwaka 2014/15 ziliagizwa tani 100,000.75; mwaka 2015/16 tani 144,000; mwaka 2016/17 tani 130,000 na mwaka 2018/19 ni tani 38,000.

Kwa upande wa sukari ya viwandani, kiasi kilichoingizwa kwa mfululizo wa miaka hiyo ni jumla ya tani 561,212.36. Mwaka 2014/2015 ni tani 120,730.60; mwaka 2015/2016 ni tani 104,792.61; mwaka 2017/2018 tani 116,563.62; mwaka 2018/2019 ni 129,414.24 na tani 89,611.29 kwa mwaka 2018/2019.

Swali: Je, hali ya uzalishaji wa sukari katika msimu wa mwaka huu ikoje? Jibu: Viwanda vyote vitano vilivyopo nchini vimeanza uzalishaji sukari kwa msimu wa mwaka 2019/2020. Vilianza uzalishaji Juni.

Hadi Septemba, jumla ya tani 143, 148.49 za sukari zilikuwa zimezalishwa sawa na asilimia 39 ya malengo ya uzalishaji wa tani 378,449.

Swali: Ni mikakati gani serikali inafanya kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa uzalishaji wa sukari na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza sukari kutoka nje ya nchi?

Jibu: Kwa kuzingatia fursa zilizopo za kuzalisha sukari ikiwamo ardhi nzuri na soko, serikali imekuwa ikihamasisha uwekezaji wa mitaji katika tasnia ya sukari nchini. Jitihada zinajumuisha uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani. Miradi hiyo ni pamoja na wa Mkulazi I na II mkoani Morogoro; viwanda vya sukari vya Chamwino mkoani Dodoma; Geita; Kasulu; Rufiji mkoani Pwani; Songea mkoani Ruvuma; Manyara na Kilosa mkoani Morogoro

Swali: Je, ni nini hatma ya utoaji vibali vya kuingiza sukari nchini?

Jibu: Serikali imeelekeza viwanda vyote vinavyozalisha sukari nchini kuwa na mpango kazi wa kupanua na kuongeza uwezo wa uzalishaji. Uamuzi wa serikali kutoa vibali kwa viwanda kuingiza sukari nchini ni kuhakikisha kiasi cha sukari chenye upungufu pekee ndiyo inaingizwa ndani ya nchi na viwanda vinaendelea kutekeleza mipango yao ya uzalishaji kadri ya kiasi cha mahitaji ya sukari nchini. Hivyo, Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ili kufikia ukomo wa kuingiza sukari nchini.

Swali: Nani anasimamia biashara ya sukari na vibali vya kuagiza sukari vinatolewa kwa utaratibu gani?

Jibu: Biashara ya sukari inasimamiwa na wizara pamoja na taasisi mbali mbali zikiwamo Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Taasisi nyingine ni Bodi ya Sukari Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Wizara na taasisi hizi zinaunda kamati ambayo hufanya tathimini ya mahitaji ya sukari nchini kulinganisha na uzalishaji kupata kiasi halisi kinachopungua. Kutokana na tathmini hiyo, ndipo utaratibu wa kutoa vibali vya kuingiza sukari nchini hufanyika.

Swali? Unauelezaje umma wa Watanzania kuhusu bei ya sukari; Je, upo uwezekano wa bei kushuka?

Jibu: Kimsingi, bei ya bidhaa hutegemea hali ya ugavi na uhitaji wa bidhaa husika. Kwa kuzingatia mipango ya kuongeza uzalishaji iliyowekwa na viwanda hapa nchini na kuanzishwa kwa viwanda vipya, ugavi wa sukari sokoni utaongezeka hivyo kusababisha bei ya bidhaa kushuka.

“FISI ni mnyama muhimu sana katika hifadhi yetu (Hifadhi ya ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi