loader
Norway yaamini sekta ya  gesi itabadili Watanzania

Norway yaamini sekta ya gesi itabadili Watanzania

BALOZI wa Norway nchini, Elisabeth Jacobsen amesema anaamini kuwa sekta ya gesi itabadili maisha ya Watanzania, kwa kuwa serikali imeonesha utofauti mkubwa kwenye usimamizi wa rasilimali za Taifa.

“Serikali ya Tanzania inasimamia vyema rasilimali zake ikiwemo gesi asilia kwa kuwanufaisha watu wake. Haya yote yanatokana na maamuzi sahihi yanayokuwa yakifanywa na viongozi wanaosimamia na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo,” alieleza Balozi Jacobsen.

Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Utafiti wa Rasilimali Gesi na Mafuta, kilichoandaliwa na Taasisi ya Utafiti ya Sera ya Uchumi na Fedha (REPOA).

“Maamuzi mazuri yamekuwa yakifanywa na Serikali ya Tanzania yakilenga kunufaisha wananchi wake, tofauti na mataifa mengine ambayo yalipopata rasilimali kama za gesi wameshindwa kuisimamia na matokeo yake haijawanufaisha wananchi wake,” alisema balozi huyo.

Akielezea kilichopo kwenye kitabu hicho  ‘Usimamizi wa Rasilimali za Gesi na Mafuta’, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema utafiti huo unaeleza jinsi gani Tanzania itakavyoweza kusimamia vyema rasilimali ya gesi asilia na kusaidia kuinua uchumi wa nchi.

Dk Mmari alitaja maeneo makuu matano, ambayo yanalifanyiwa utafiti kuwa yalilenga kueleza nini kitarajiwe kwenye sekta ya gesi, namna bora ya usimamizi, ushirikishwaji wa wananchi, jinsi gani fedha za mauzo na uwazi wa matumizi ya fedha zitokanazo na sekya ya gesi.

“Tuna rasilimali ya gesi, tumetafiti na kupendekeza baadhi ya mambo ambayo yanaweza kufanywa na Serikali ili watanzania waweze kunufaika na rasilimali ya gesi. Watanzania wana matarajiao mengi hivyo tunatakiwa kuweka umakini kwenye usimamizi,” alisema Dk Mmari.

Aliongeza, “Pia tunatakiwa kuangalia ni jinsi gani fedha za mauzo ya gesi zitatumika kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo kama ya afya, elimu na miundombinu lakini pia kwenye utafiti wetu tunaeleza haya ya uwepo wa uwazi kwenye usimamizi wa fedha”.

Alisisitiza lengo la utafiti huo ni kushirikiana na serikali, kuhakikisha rasilimali gesi inabadili maisha ya Watanzania.

Kamishna Msaidizi wa Gesi katika Wizara ya Nishati, Sebastian Shana alipongeza Repoa kwa kuandaa kitabu chenye kuonesha mwelekeo wa sekta ya gesi nchini.

Shana alisema “Nchini Tanzania, tuligundua gesi mwaka 1974, tukaanza kuitumia mwaka 2004 na mpaka sasa ni sehemu ndogo ya rasilimali hiyo ambayo imeshatumika. Leo hii asilimia 54 ya umeme kwenye gridi ya taifa inatokana na gesi hii asilia.”

Aliongeza, “Leo hii tunasambaza gesi majumbani lakini pia inatumika kwenye magari imewekewa mifumo maalumu kama mbadala wa petroli. Hizi zote ni hatua nzuri.” Alieleza kuwa rasilimali hizo ni za wananchi na ziko kwa ajili ya maendeleo yao.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge waliohudhuria uzinduzi wa kitabu hicho, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) alisema kupitia utafiti uliofanywa na REPOA ni wakati sasa nchi ikaongeza kasi kwenye uvunaji wa gesi asilia.

Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, alisema kuwa ili uchumi wa nchi uweze kupiga hatua ni vyema rasilimali zake, zikatumika kwa usahihi.

Alisema, “Wenye maamuzi (Serikali) iangalie jinsi gani itafanyia kazi utafiti huu mzuri uliofanywa na REPOA kwa miaka mitano. Kuna juhudi kubwa zinazofanywa na Rais John Magufuli na wasaidizi wake lakini tunahitaji kuongeza kasi kwenye uvunaji wa gesi ili iweze kunufaisha taifa.

“Dunia haitusubiri, tuvune tulichonacho kwa ajili ya vizazi. Kama vitatumika vizuri tutafika mbali,” alisema Ngeleja.

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/a31f4aff2f2c7a0564600b56bef3c5bc.JPG

Mmoja kati ya vijana sita, ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi