loader
Tanzania kutibu saratani kwa nyuklia

Tanzania kutibu saratani kwa nyuklia

TANZANIA itaandika historia ya kuwa nchi ya kwanza kwenye Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara (ukitoa Afrika Kusini), kuwa na huduma bora za tiba na uchunguzi wa saratani kwa kutumia mashine za kisasa za PET/CT Scan na tiba za dawa za nyuklia.

Kwa sasa nchi za Afrika zinazokuja Tanzania kufuata huduma za tiba ya saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ni Kenya, Comoro, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.

Aidha, rufani zilizokuwa zikitolewa kwa wagonjwa wa saratani kwenda nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi, huenda sasa zisitolewe baada ya mashine na dawa hizo kuanza kutolewa Aprili mwakani.

Akizungumzia maboresho hayo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage alisema serikali imetoa Sh bilioni 14.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo maalumu, ununuzi na kusimika mashine mpya mbili na za kisasa za Cyclotron na Pet/ CT Scan.

Alisema mashine hizo ndizo zinatumika duniani kote hivi sasa kutibu na kufanya uchunguzi wa saratani hususan kwa saratani ya damu ili kumpa mgonjwa tiba stahiki kulingana na kiwango cha ugonjwa wake.

Alisema awali tatizo lililokuwepo ni ukosefu wa mashine hizo na ndiyo ilikuwa moja ya sababu ya kuwapeleka wagonjwa wa saratani ya damu nje kwa ajili ya kufanya vipimo hivyo kwenye mashine hizo, na kwamba Tanzania itaandika historia baada ya kuzinunua kwasababu katika ukanda tajwa mashine hizo hazipo.

“Tutaandika historia na hiyo itaongeza idadi ya wagonjwa tunaopokea kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matibabu katika taasisi yetu, ukitoa Afrika Kusini na nchi za Afrika ya Kaskazini, nchi nyingine zilizobaki mashine hiyo na dawa za nyuklia hazipo, Tanzania tutakuwa wa kwanza,” alisema Dk Mwaiselage.

Akizungumzia kuanza kwa huduma hizo, alisema miradi hiyo imeshaanza na inategemewa kukamilika Aprili mwakani na hivyo serikali itaokoa fedha za kugharamia matibabu ya rufani za wagonjwa wa saratani nje ya nchi.

Alisema mwaka 2015 wagonjwa 164 wa rufani walipelekwa nje ya nchi kutibiwa saratani lakini baada ya kuanza kuboreshwa kwa huduma katika miaka minne ya awamu ya tano, rufani hizo zimepungua na mwaka 2019 wagonjwa 14 tu wa saratani ya damu ndio walipewa rufani na hivyo serikali ikaokoa Sh bilioni tano.

Alisema rufani hizo za kwenda nje kutibiwa zilitokana na nchi kukosa mashine za PET CT Scan na dawa za nyuklia lakini baada ya miezi mitano kuanzia sasa mashine hizo zitakuwa zimeshafungwa na kuanza kutoa huduma.

Akizungumzia ujenzi wa kiwanda cha dawa za saratani za nyuklia kwa wagonjwa wa saratani ya damu, Dk Mwaiselage alisema ujenzi wake umeshaanza na dawa zitakazotengenezwa ni za nyuklia (rasio-isotopes) zinazotumika kwa wagonjwa wa saratani wakati wa kupima kipimo cha PET/ CTScan.

Amesema baada ya kiwanda cha kuzalisha dawa hiyo kitakapokamilika na kuanza uzalishaji Aprili mwakani, dawa hizo pia zitaweza kuuzwa kwenye hospitali nyingine nchini zitakazofungwa mashine hizo za PET/CT scan ili kuhakikisha hakuna mgonjwa wa saratani anayekwenda nje kufuata huduma.

“Tutakuwa tumejitosheleza kwani mashine hizo za PET/CT scan na hiyo cyclotron ndizo zinatumika kwenye hospitali zote duniani, ukienda Marekani ndiyo inatumika sasa kutibu wagonjwa, nenda India utaikuta, nenda popote ndio hizo na sisi tunazileta ili turahisishe huduma na tiba,” amesema Dk Mwaiselage.

Akizungumzia utoaji huduma katika taasisi hiyo ndani ya miaka minne ya awamu ya tano, Dk Mwaiselage alisema serikali imefanya maboresho kwenye taasisi ya saratani ambapo kwa sasa bajeti ya dawa kila mwaka ni Sh bilioni 10 kutoka Sh milioni 790 mwaka 2015/16.

Aidha, huduma za tiba ya saratani zimeboreka ambazo ni tiba ya upasuaji, mionzi na dawa na kwamba upatikanaji wa dawa kwa sasa ni asilimia 95 ukilinganisha na miaka minne ya awali iliyokuwa asilimia nne tu.

Mbali na uboreshaji wa dawa na huduma za saratani ambazo hutolewa bure kwa serikali kugharamia, pia ununuzi wa vifaa tiba mionzi umeboreka kwani hivi sasa wagonjwa wagonjwa 70 hufanyiwa vipimo kwa wiki ukilinganisha na awali ambapo wagonjwa 30 tu kwa wiki ndio walifanyiwa vipimo.

Aidha, ujenzi wa wodi mpya kwa ajili ya wagonjwa binafsi na wale wanaotoka nje ya nchi uko kwenye maandalizi ili kuboresha huduma na kuongeza mapato ya hospitali hiyo yatokanayo na wagonjwa binafsi na wale wanaotumia bima.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6dd518afb7a7ef867fc9efeca0196586.jpg

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mradi wa ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi