loader
Picha

Sumaye aibua mjadala mzito

KUONDOKA kwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumeibua watu mbalimbali waliowahi kuwa wanachama hicho, baadhi yao wakisema alichelewa kuchukua uamuzi huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanasiasa hao ambao baadhi walikuwa na nyadhifa ndani ya Chadema, wamesisitiza umuhimu wa vyama vyote vya siasa kumulikwa mifumo yake ya demokrasia, ifahamike umma usidanganywe na maneno ya majukwaani.

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili jana ni Hamisi Mngeja aliyehamia Chadema mwaka 2015 na kisha kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka jana. Mngeja alimpongeza na kumsihi Sumaye kutafakari juu ya kurudi ‘nyumbani’ akimaanisha kwenye chama tawala alichokihama.

“Itakuwa ni busara akirudi nyumbani. Acha kwanza atafakari. Inatosha tu leo (jana) kumpongeza kwa hatua ya awali,” alisema Mngeja akizungumzia kitendo hicho cha Sumaye kutangaza uamuzi wa kuondoka kwenye chama hicho jana.

Alisisitiza kuwa hatajiunga na chama chochote, bali atabaki kuwa huru kutumika kwa ushauri na watakaomhitaji.

Yaliyomkuta Sumaye

Akitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam kwa kuanika kasoro mbalimbali za Chadema, Sumaye alisema ndani ya chama hicho hakuna demokrasia na nafasi ya Mwenyekiti wa taifa inayoshikiliwa na Freeman Mbowe haiguswi. Alisisitiza kwamba amesitisha uanachama kwa usalama wake, wanachama na chama kwa ujumla.

Alieleza alivyofanyiwa figisu wakati wa uchaguzi wa Kanda ya Pwani, ikiwamo wajumbe kupewa fedha na kuwekwa hotelini kwa lengo la kumuangusha.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Sumaye aliongozana na Katibu wa Kanda ya Pwani, Casimir Mabina ambaye pia alitangaza kujivua wadhifa huo, akisema mazingira yaliyopo yamemfanya achukue uamuzi huo na atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa Chadema.

Sumaye alisema nongwa dhidi yake, ilitokana na uamuzi wake wa kutaka kugombea uenyekiti wa taifa. Alishachukua fomu ambayo aliilipia Sh milioni moja na kuiwasilisha kabla ya kuamua jana kujiondoa ndani ya chama.

Kwa mujibu wa Sumaye, wanachama walimtaka agombee uenyekiti wa Kanda ya Pwani akawakubalia, lakini siku ya uchaguzi, baadhi ya wajumbe walifungiwa hotelini na wakapewa fedha kwa lengo la kumuangusha, jambo lililofanikiwa kwa kupigiwa kura nyingi za ‘hapana’.

Uchaguzi huo ulifanyika Novemba 28, mwaka huu na Sumaye alikuwa mgombea pekee, ambapo alipigiwa kura 28 za ‘Ndiyo’ na kura 48 za ‘Hapana’. “Nilifanyiwa figisu uchaguzi wa kanda ya Pwani, kwani wajumbe walifichwa hotelini na kulipwa posho ili nishindwe,” alisema Sumaye.

Alisisitiza kuwa ndani ya Chadema, hakuna demokrasia.

Akisisitiza kuwa hakuhamia Chadema kusakacheo, Sumaye alieleza namna kuhamia kwake upinzani kulivyomuathiri, ikiwamo kulaumiwa na familia yake na kukosa haki kama wanazopata wastaafu wengine katika ngazi ya uwaziri mkuu.

Alisema kutokana na uamuzi wake wa kuondoka Chadema, mkewe na watoto wake watamvisha taji la kuondokana na adha katika chama hicho cha upinzani.

Alisema awali hakuamini yaliyokuwa yakisemwa kwamba ndani ya Chadema hakuna demokrasia na kwamba kiti cha Mbowe hakisogelewi.

Alisema uamuzi wake wa kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti wa taifa, ulilenga kuondoa hisia hizo na kukisafisha chama.

Sumaye alisema baada ya kuwasilisha fomu, uchunguzi wake ulionesha siyo muafaka kuendelea na safari hiyo ya kugombea, kwa kile alichosisitiza kwamba amesitisha uanachama kwa usalama wake, haoni sababu ya kuonja sumu kwa ulimi, kama ambavyo Mbowe aliwahi kuwahadharisha wakiwa kwenye kikao mkoani Arusha.

Alitaja mambo yanayoitafuna Chadema ni makundi kutokana na kuwapo mgawanyiko kati ya wafuasi wa Mbowe na wasio. Sumaye ambaye alisema anategemea kupokea matusi, alisisitiza kuwa pamoja na nchi kuhitaji upinzani imara, hilo haliwezekani kutokana na hali halisi ya chama hicho kikubwa.

Alisema fedheha hizo alizopata ikiwa ni malipo ya kutaka kugombea uenyekiti wa taifa, zimeamsha tena hasira ya familia, hivyo isingekuwa rahisi kwake kukaza shingo na kuendelea kubaki ndani ya chama hicho.

“Nilipotafakari ustaarabu ukasema “toka Sumaye huhitajiki”. Akifafanua kuhusu wanaomuona kwamba hapendi ‘kukatwa’ wala kushindwa na ndiyo maana alihama CCM mwaka 2015, Sumaye alisisitiza kuwa hakuhama kwa sababu ya jina lake kukatwa kwenye kugombea urais, bali alikwenda kwa lengo la kuupa nguvu upinzani.

Sumaye ambaye alisisitiza kwamba anakwenda kupumzika na hana mazungumzo aliyofanya na ACT Wazalendo kama ilivyosambazwa jana kwenye mitandao ya kijamii, kuhamia chama kingine si kosa, isipokuwa dhamira yake imemuelekeza aachane na vyama.

Wamchambua Sumaye, Chadema

Akizungumza na gazeti hili, Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Bara, Shaaban Mambo aliunga mkono hatua ya Sumaye kuanika kasoro za Chadema, akisema ni njia sahihi kuwezesha umma wakiwamo wanaotaka kujiunga, kufahamu matatizo yaliyopo kabla ya kuingia.

Mambo aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Meya wa Manispaa ya Kigoma na Mwenyekiti wa Madiwani wa Chadema kabla ya kukihama mwaka 2013/14, alisema Sumaye alipokwenda Chadema alitakiwa kufahamu utamaduni wa chama hicho.

“Haya yasiishie Chadema, bali pia ACT na vyama vyote kikiwamo chama tawala… vyombo vya habari msaidie kuanika haya yote ili tujenge nchi yenye demokrasia,” alisema. Mambo alikanusha kwamba Sumaye ana mpango kuhamia ACT, akisema hawajawahi kuzungumza naye juu ya hilo.

“Sisi kwa wakati huu hatuna shida kwenda kumshawishi mtu aje kwetu, Watanzania bado ni wengi,” alisema.

Akizungumzia uzoefu ndani ya chama hicho, alisema kila inapofika uchaguzi mkuu, Chadema hukumbwa na kelele kama ilivyotokea uchaguzi wa mwaka 2014 na kusababisha Kabwe Zitto kukihama. “Ni mambo ambayo unapokwenda, unatakiwa kufahamu itatokea hivi,” alisema.

Alisema katika Chadema hakuna anayeweza kusimama, akasema ukweli na ikitokea hivyo ni lazima ahame chama na kuwaacha wanaosalimu amri.

“Mzee sumaye alikuja kwa moyo mkunjufu kuweka nguvu zaidi kwenye upinzani. Kwa sababu alikwenda kugombea uongozi wa ngazi ya juu, angefanya subira kidogo. Hakujua utamaduni wa Chadema,” alisema.

Alitaka Chadema kijitathimini katika suala zima la demokrasia, kwa kuachia wanachama kuwa na uhuru wa kuchagua mtu wanayemtaka. Alisema ACT Wazalendo ni waathirika wa matatizo ya kwenye vyama, hivyo wanajihadhari yasitokee yaliyowakimbiza kwenye vyama husika.

Wafurahia kusafishwa

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba aliliambia gazeti hili kwamba kuondoka kwa Sumaye na kuanika kasoro za chama ni faraja kwao, kwani umma unazidi kuelewa kwamba walikuwa sahihi kukihama. Mwigamba ambaye pia alikuwa Mhasibu wa chama hicho makao makuu na sasa ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kadri siku zinavyokwenda, watatokea watu wengi zaidi watakaoelezea hali halisi ndani ya Chadema.

“Walipojitokeza watu na sisi tukajitokeza kueleza haya, hatukueleweka. Huu ni ushahidi kwamba yanayofanyika ndani tuliyosema yalikuwa kweli. Kuna watu hawataki demokrasia ya nchi hii iendelee, lakini kwa kuwa mtu alikuwa akidanganya watu, aendelee kuanikwa na wanachama wafahamu kwamba chama kinapelekwa kwenye bwawa la mamba,” alisema Mwigamba.

Mngeja: Sumaye alichelewa

“Nampongeza Sumaye kwa kutumia uamuzi wa busara… hizo kasoro sisi tuliziona siku nyingi sana na ndiyo maana tukawahi kuchomoka mapema mimi na Lowassa (Edward-Waziri Mkuu mstaafu).

Alisema walibaini kwamba hao wanaosema wanapigania demokrasia, ndiyo wanaoikandamiza ndani ya chama chao.

“Tukaona acha turudi kwenye chama chetu cha CCM,” alisema Mngeja na kumshauri Sumaye baada ya kutafakari arudi.

Aliendelea, “alikuwa amechelewa; Angechukua uamuzi zamani kama tulivyoona. Lakini pamoja na kuchelewa, tunampa hongera zake. Alikuwa akiruka na ndege ambao alikuwa hafanani nao.Bata huwezi kumchanganya na kunguru. Sisi tulipoliona kwamba haturuki pamoja na hawa, tukaona bora turudi kwenye asili yetu CCM mbako tukiruka tunaruka pamoja.”

Akiendelea kuainisha kasoro, Mngeja alisema walikuwa wakitoa ushauri lakini haupokewi. Miongoni mwa ushauri ilikuwa ni kukiondoa chama kutoka kwenye uhanaharakati kuwa chama kamili cha siasa.

“Kuna giza nene sana ndani ya Chadema. Na hilo litaendelea kuwatafuna hawatabaki salama, ni vizuri wakajitathimini sana. Nashukuru kwamba watu sasa wameanza kuwashutukia,” alisema.

Alisisitiza kuwa hakuna matumaini ya vyama vya upinzani kushika dola sasa.

“Wanajifanya wao wana demokrasia wakati wao ni wauaji wakubwa wa demokrasia,” alisema Mngeja.

CCM haina mbadala Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni miongoni mwa wanasiasa waliofukuzwa Chadema mwaka 2013, alisema kinachoendelea kinathibitisha kuwa chama hicho hakina uhalali wa kupigania demokrasia, unapokuja uchaguzi wa mwenyekiti wa taifa.

Mkumbo akiwa Chadema alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu. Mwaka 2014 ndipo alihama chama hicho na kujiunga ACT – Wazalendo, ambacho alijiuzulu mwaka 2017 baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu.

“Kuna msemo kwamba ‘muda ndiyo jibu la kila kitu’. Sisi tulifukuzwa Chadema mwaka 2013, tuliambiwa sisi ni wasaliti lakini miaka sita baadaye (mwaka huu) yamejirudia. Waliotuita wahaini, hao hao wanaondoka,” alisema.

Alisema imefika wakati, chama kibadilishe nafasi ya uenyekiti kuwa ya kifalme. Alisema pamoja na vyama hivi kuanzishwa viwe mbadala wa CCM, mpaka sasa hakuna chama mbadala, kwani vingi vimebaki kuwepo kwa sababu sheria inaruhusu. Alivyojiengua CCM Sumaye alikuwa waziri mkuu wa pili nchini, kujiengua CCM kwenda Chadema mwaka 2015.

Mwingine ni Edward Lowassa aliyehamia huko mwezi Julai mwaka huo 2015.

Akizungumza na waandishi Agosti 22, 2015, Sumaye alisema ameamua kuhama CCM, kutokana na kukithiri kwa rushwa ndani ya CCM wakati huo na kuvurugwa kwa uchaguzi, kulikochangia wananchi kukata tamaa, hali iliyofanya baadhi ya watu kuunga mkono upinzani.

Sumaye alieleza kuwa ameamua kujiunga na upinzani, ili kushirikiana na viongozi wa kambi hiyo, kuwatumikia Watanzania na alikuwa na imani wapinzani wangeshinda uchaguzi.

“Sitoki CCM kwa sababu nina hasira na CCM au sikuchaguliwa au sikuteuliwa kugombea; na wala sitoki CCM ili kudhoofisha Chama Cha Mapinduzi badala yake nakiimarisha” alieleza Sumaye siku hiyo alipojiengua CCM.

Sumaye ni nani? Sumaye ambaye alizaliwa Mei 29, 1950 mkoani Arusha, ni Waziri Mkuu wa saba tangu Tanzania ipate Uhuru mwaka 1961. Alishika madaraka Novemba 28 , 1995 hadi Desemba 30, 2005.

Mtangulizi wake ni Cleopa Msuya. Aliwahi kuwa Mbunge wa Hanang kuanzia mwaka 1983 hadi 2005 kisha jimbo hilo kuongozwa na Mary Nagu (CCM) mpaka sasa.

Aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Ushirika kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Alikuwa mwana CCM hadi Agosti 22, 2015 alipotangaza mbele ya waandishi wa habari kuhamia Chadema.

Waliowahi kujiengua Mbali na Sumaye, wanasiasa wengine ambao wamewahi kuwepo Chadema na kisha kujiengua ni Edward Lowassa, Profesa Kitila Mkumbo, Dk Wilbrod Slaa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema na Said Arfi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.

Wengine ni Dk Amani Walid Kabourou aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti Bara na Chacha Wangwe, ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho. Wengine ni Shaibu Akwilombe aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara na Kabwe Zitto aliyewahi pia kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara.

MISIKITI ya Zanzibar imeanza kutekeleza agizo la Mufti wa Zanzibar ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi