loader
Picha

Wauza vinyago wahakikishiwa kutosumbuliwa

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imewatoa wasiwasi wafanyabiashara wa vinyago kuhusu utaratibu wa usafi rishaji wa bidhaa hiyo nje ya nchi kwa wageni wanapoondoka nchini.

Kwa muda mrefu wafanyabiashara hao wamekuwa wakilalamika wakala umekuwa kikwazo cha wao kuuza vinyago kutokana na usumbufu wanaokutana nao wageni wanapopita na vinyago katika kiwanja cha ndege.

Akizungumza jana wakati wa mkutano kati ya wafanyabiashara wa vinyago wa Mwenge na Meneja wa TFS wilaya ya Kinondoni, Dotto Ndumbikwa alisema kinachofanyika ni kuhakikisha rasilimali za misitu zinasimamiwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

“Tumekuja kuzungumza nanyi kuwapa ufafanuzi muelewe pale uwanja wa ndege kinyago chochote ambacho kitakuwa chini ya kilo 10, hakitatakiwa kukatiwa kibali ila kiasi hicho kikizidi utaratibu uliopo ni lazima kiwe na kibali,” alisema Ndumbikwa.

Alisema si lengo la TFS kuwakwamisha bali wanataka biashara hiyo ifanyike kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kuhusisha vibali kwa vinyago vinavyozidi kilogramu 10 vinaposafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Kurahisisha hilo tumefungua ofisi hapa Mwenge ili vibali na nyaraka zingine ziweze kupatikana hapa na kumuondolea usumbufu mgeni anapofika uwanja wa ndege na kukutana na maelekezo yanaweza kumsababishia kuacha vinyago alivyobeba,” aliongeza.

Pia alisema endapo mgeni aliyenunua kinyago na kupata vibali kutoka katika ofisi ya Mwenge hakuna ofisa wa TFS anaweza kumsumbua labda vishoka wanaofanya hivyo kwa maslahi yao binafsi.

Kwa upande wake Meneja wa TFS Ilala, Davis Mlowe aliwataka wanunuzi wa vinyago kutosita kutoa taarifa wanapotakiwa kulipia fedha kwa ajili ya vibali kwa vinyago vyenye uzito usiozidi kilo 10.

Awali Mwenyekiti wa wachonga vinyago wa Makonde Crafters, Hamis Mhando alisema wamekuwa wakipoteza wateja wa vinyago kutokana na wageni kushindwa kuhimili usumbufu wanaokutana nao uwanja wa ndege wakitakiwa kutozwa.

“Sasa hivi hatuna biashara wageni wameambizana wakija Tanzania hawanunui vinyago kutokana na usumbufu wanaopata kutoka kwa watu wa maliasili pale uwanja wa ndege na imekuwa changamoto kwetu tunatengeneza vinyago na kukaa navyo tunaomba serikali iliangalie suala hili,” alisema Mhando.

ELIMU ya Awali ni sehemu muhimu sana ya dhana nzima ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi