loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Man City, United shangwe muhimu leo

PAMOJA na kuwa kwenye nafasi tofauti katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, lakini mechi ya wapinzani wa Manchester, City na United inakuwa na mvuto wake. Miamba hiyo inakutana leo kwenye uwanja wa Etihad ambapo City itakuwa mwenyeji wa United.

Bingwa mtetezi City, inakwenda kwenye mechi hiyo ikionekana kupoteza matumaini ya kutetea taji lake, lakini United inaingia ikipambana walau isogee juu juu kwenye msimamo.

Inatia huruma, United ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo, ina kazi kubwa leo kuizuia City ambayo Jumanne ya wiki hii ilikuwa na shangwe za nguvu ilipoibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Burnley.

Shangwe zilitawala kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Manchester City kabla ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Burnley Jumanne ya wiki hii, lakini na wachezaji walipokuwa uwanjani walihakikisha wanaweka hai matumaini ya kutetea taji lao. Haitakuwa makosa kama utaamini presha bado ipo kwa kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola, licha ya kushinda mechi hiyo kwa mabao 4-1.

Hakukuwa na changamoto zaidi kwenye soka ya England usiku huo zaidi ya kuifunga Burnley, City ilicheza mechi hiyo ikitoka kutoka sare dhidi ya Newcastle na kuwa nyuma kwa pointi 11 dhidi ya vinara Liverpool.

Lakini katika kile kilichoonekana kujiamini zaidi, wageni walicheza bila wasiwasi wowote usiku huo wakionekana wenye nia ya dhati kutwaa taji la Ligi Kuu kwa mara nyingine, wakitawala vizuri kwenye kiungo.

Hata hivyo, matumaini ya City kutetea ubingwa bado yapo njia panda kutokana na kuandamwa na majeruhi. Itakuwa rahisi kwa Guardiola kulalamikia majeruhi aliyo nayo kuwa sababu ya kuburuzwa na Reds kwenye msimamo, lakini amekataa kufanya hivyo. Hata hivyo huwezi kuivunja rekodi ya Manchester City iliyoiweka zaidi ya misimu miwili iliyopita ikiwa na ubora mkubwa .

Gabriel Jesus, anayeonekana kuhaha kuvaa viatu vya Sergio Aguero, aliunyamazisha umati uliojaa Turf Moor kwa bao safi la kuongoza na kuleta tija kwa mchezaji huyo wa Brazil aliyesajiliwa mwaka 2017. Kisha akanogesha ushindi kwa timu yake kwa kuunganisha mpira safi ya krosi kutoka kwa Bernardo Silva na kuandika bao la pili.

Mchezaji aliyesajiliwa msimu huu Rodri alikuwa na wakati mgumu mwanzoni mwa maisha yake City, lakini hayo yote yalisahaulika alipofunga bao la tatu siku hiyo. Na bao la nne likitoka kwa Riyad Mahrez, labda akiwa mchezaji wa City anayejiamini zaidi. Baada ya mechi hiyo Guardiola katika kile kilichoonekana amefanya utani alisema mbio za ubingwa zimekwisha kutokana na yale aliyoyasoma kwenye vyombo vya habari.

Alionekana kukwepa kuzungumzia taji, akisema kuzungumzia jambo hilo ni wendawazimu na upuuzi kwani wameachwa kwa tofauti ya pointi nane na vinara Liverpool ambayo Jumatano ya wiki hii ilicheza na Everton. Lakini kiwango kilichooneshwa uwanjani, kilionesha wote yeye (Guardiola) na wachezaji wake hawajakata tamaa bado ya kutwaa taji. Kama ilivyokuwa msimu uliopita, walihitaji msaada kutoka mahali.

Miezi tisa iliyopita, walihitaji msaada kutoka Everton pale the Blues ilipoibana mbavu Liverpool kwa kutoka nayo suluhu. Leo mabingwa hao watetezi Man City wataikaribisha Manchester United, mechi inayosubiriwa kwa hamu, je shangwe za mechi ya Jumanne zitaendelea? Vipi kuhusu kiwango kilichooneshwa siku hiyo. Rodri ameonya kwamba Manchester City imekuwa yenye kujiamini na mechi hiyo itakayochezwa leo usiku.

Nyota huyo wa Hispania, Rodri alifunga bao kwenye ushindi wa katikati ya wiki hii. Guardiola baada ya mechi na Bunley alionekana kujiamini zaidi akisema anafurahia kikosi chake kwa namna kilivyocheza mechi hizo mbili. Ukweli ni kwamba mechi hiyo iliwafanya wachezaji kujiamini zaidi, na kupanga kubeba pointi nyingine tatu leo ili kujiweka vizuri kwenye kutetea taji lao. “Tunahitaji ushindi,” anasema Rodri.

“Wakati mwingine ushindi unakufanya kujiamini zaidi, ndivyo ilivyotokea mechi ya Jumanne, na Jumamosi (leo) tunataka kujiamini zaidi.” Rodri aliyekuwa mchezaji bora wa mechi hiyo alisema yupo imara kucheza mechi yake ya kwanza ya wapinzani.

“Nina furaha sana, itakuwa mechi nzuri dhidi ya Manchester United sijui itakavyokuwa lakini itakuwa nzuri kwenye uwanja wetu, kama hutokuwa uwanjani, huwezi kujua nini kitatokea.”

foto
Mwandishi: MANCHESTER, England

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi