loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ligi Kuu ya wanawake yarejea

LIGI Kuu ya soka ya wanawake inatarajiwa kuendelea leo baada ya kusimama kwa mwezi mmoja kupisha michuano ya kombe la Chalenji iliyofanyika nchini mwezi uliopita. Ligi hiyo ambayo inaingia katika mzunguko wa tatu leo itachezwa michezo sita katika viwanja vya miji tofauti.

Bingwa mtetezi JKT Queens itacheza na Simba Queens kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam. Mchezo huo unatarajiwa kuwa na upinzani kwani Simba Queens itahitaji kufuta uteja kwa JKT Queens kwa sababu katika michezo minne waliyokutana tangu msimu wa mwaka 2017 hadi 2018 Simba Queens imefungwa mechi zote.

JKT Queens inaongoza msimamo ikiwa na pointi sita walizopata katika mechi za ugenini wakati Simba Queens ina pointi nne ilizozipata katika uwanja wake wa nyumbani, Karume. Endapo Simba Queens itashinda mechi hiyo itakuwa timu ya pili kuifunga JKT kwani Mlandizi Queens iliwahi kufanya hivyo msimu wa mwaka 2016/2017 walipotwaa ubingwa ligi ilipoanza lakini kama JKT Queens haitafungwa itaendeleza rekodi ya kutofungwa kwa msimu wa tatu.

Mchezo mwingine utazikutanisha Yanga Princess ambayo itaialika Mlandizi Queens katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Yanga Princess msimu huu imeanza vyema kwa kushinda mechi zote mbili ilizocheza na kujikusanyia pointi sita huku Mlandizi Queens ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza michezo miwili ikiifunga Panama Queens na kufungwa na Ruvuma Queens katika uwanja wa nyumbani Mabatini, Pwani.

Mji wa Songea utakuwa unaandika historia kwa mara ya kwanza tangu Ligi Kuu ya wanawake Tanzania Bara ianzishwe msimu wa mwaka 2016/2017 kwani hawakuwa na timu ya wanawake lakini safari hii Ruvuma Queens itamenyana na TSC Queens katika Uwanja wa Majimaji Ruvuma Queens yenye pointi nne, mechi za mwanzo mbili ilicheza ugenini hivyo haijawahi kutumia uwanja huo kwa mechi za Ligi Kuu zaidi ya zile za kirafiki.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwasababu timu zote zimepanda daraja msimu huu lakini Ruvuma Queens inaonekana kuwa vizuri zaidi kutokana na kuwa na wachezaji wazoefu zaidi kwenye ligi ukilinganisha na TSC Queens yenye pointi tatu.

Panama Queens ya Iringa ambayo haina pointi itaialika Alliance Girls ya Mwanza yenye pointi sita katika Uwanja wa Samora Iringa, Sisterz ya Kigoma yenye pointi tatu itacheza na vibonde Tanzanite Queens ambayo inashika mkia katika msimamo kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Marsh Queens ya Mwanza itacheza na Baobab Queens ya Dodoma katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani kwani hakuna timu iliyoshinda mchezo wake katika ligi ya msimu huu.

Katika kuwania kiatu cha ufungaji bora Fatuma Mustafa wa JKT Queens ana mabao sita akifuatiwa mchezaji mwenzake wa JKT Asha Rashid mwenye mabao matano na Mwapewa Mtumwa wa Yanga Princess ana mabao manne.

Mwanahamisi Omar wa Simba Queens ana mabao mawili sawa na Philomena Daniel na Jamila Hassan wa Mlandizi Queens na Janeth Matulanga wa Alliance Girls.

TIMU ya Ruvu Shooting imeboresha kikosi ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi