loader
Picha

Serikali yalipa mil 703/- kwa wazabuni Moro

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imewalipa wazabuni wa mkoa wa Morogoro waliokuwa wametoa huduma za chakula kwenye shule za serikali, Sh milioni 703.1 baada ya madeni yao kufanyiwa uhakiki na kuthibitishwa ni halali.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema hayo akijibu hoja za fedha na kodi katika mkutano wa mashauriano kati ya serikali, wafanyabiashara na wawekezaji mkoa wa Morogoro juzi, chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angellah Kairuki.

Alitoa maelezo ya serikali kutokana na Mwenyekiti wa wazabuni mkoa wa Morogoro, Juma Yahaya kudai kwenye mkutano huo kumekuwa na changamoto ya kutolipwa fedha zao bali ahadi ya kulipwa inayotolewa na serikali na haitekelezwi hadi wengine wanafariki, kuumwa na wengine kufilisiwa biashara.

Ashatu alisema serikali kuanzia mwaka 2016/2017 ilianza kulipa madeni ya watoa huduma baada ya kufanyika kwa uhakiki na kuthibitshwa ni halali.

“Serikali imelipa madeni ya wazabuni wakiwemo wa mkoa wa Morogoro baada ya Tamisemi kufanya uhakiki wa madeni yote ambayo waliwasilishwa na wizara ya fedha nayo kuendeleza ukaguzi kupitia mkaguzi mkuu kuupitia tena uhakiki huo kabla ya kulipwa na serikali,” alisema Dk Kijaji.

Alisema baada ya uhakiki, wazabuni wa mkoa wa Morogoro waliosambaza vyakula shule za serikali mwaka 2016/2017 walilipwa Sh milioni 291. 8. Alisema mwaka 2017/2018 serikali ilitenga Sh trilioni moja kulipa madeni na wazabuni wa mkoa wa Morogoro wa vyakula walilipwa Sh milioni 291.8. Alisema mwaka 2018/2019, serikali pia ilitenga Sh trilioni moja kulipa madeni na wazabuni wa mkoa wa Morogoro wa vyakula walilipwa Sh 119,482,037.

“Wazabuni wa mkoa wa Morogoro tangu 2016 wamelipwa na ambaye hajalipwa anaipiga serikali,” alisema.

Alisema serikali itaendelea kulipa madeni ya wazabuni halali ambayo wanafunzi wa shule za serikali walipewa huduma ya chakula shuleni. Alisema serikali imekuwa ikifanya jambo la ushirikishaji wa masuala ya kodi kwa uwazi na wataalamu wapo tayari kupokea maoni ya wadau wa kodi. Aliziomba mamlaka za serikali kabla ya kuweka sheria au kanuni za tozo, kwanza kuwasiliana na Waziri wa Fedha na Mipango ili kupata idhini.

Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege akizungumzia wazabuni alisema kulikuwa na changamoto ya madeni ya nyuma kurudi mwaka 2014 , lakini tangu serikali hii iingie madarakani hakuna madai mapya ya wazabuni.

ELIMU ya Awali ni sehemu muhimu sana ya dhana nzima ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi