loader
Picha

Magufuli- Watanzania tukiamua tunaweza

RAIS John Magufuli ameweka jiwe la msingi katika mradi wa daraja la Kigongo-Busisi wilaya ya Misungwi na kusema ujenzi wake ni uthibitisho mwingine kwamba nchi si masikini bali watanzania wakiamua wanaweza.

Alisema Sh bilioni 699.2 za mradi huo ni kodi za wananchi zinazoimarisha uhuru wa nchi na kufanya iheshimike duniani kutokana na kufanya uamuzi wake yenyewe.

Magufuli ambaye alieleza alivyonusurika kufa maji katika eneo hilo katika miaka ya 1990, alisema wapo watu waliopoteza maisha kwa kuzama majini kutokana na ajali za mitumbwi wakivuka baada ya feri kuharibika.

Aidha, katika uzinduzi huo uliofanyika eneo la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza, Rais Magufuli amehimiza Watanzania kutunza amani akisema maendeleo yaliyopo ni matokeo ya kushikamana.

Tanzania tajiri

“Kwangu ujenzi wa daraja hili ni uthibitisho mwingine kwamba nchi yetu si masikini na watanzania tukiamua tunaweza,” alisema Rais Magufuli akisisitiza Watanzania kutembelea kifua mbele kwa kuwa fedha zinazotumika ni kodi zao.

Alisisitiza, “Sh bilioni 699.2 ni fedha nyingi na zote zimetolewa na serikali yenu, hatujaomba mkopo, hatujaomba msaada, hatujampigia magoti mtu, hatujamlilia mtu, ni fedha zenu Watanzania.”

Rais alisema kodi zinazokusanywa ndizo zinatumika kujenga reli, kutoa elimu bure, zilizojenga zaidi ya vituo 352 vya afya, bwawa kubwa la Nyerere litakalozalisha megawati za umeme 2,115.

“Ndiyo maana nimekuwa nikiwaambia tutembee kifua mbele, sisi Watanzania ni matajiri siyo masikini,” alisema.

Alihimiza wananchi kulipa kodi na kusisitiza kwamba licha ya kuwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo na kijamii, pia zinaimarisha uhuru wa nchi na kufanya iheshimike duniani.

“Kutokana na kodi zetu, tunafanya maamuzi sisi wenyewe.”

Magufuli alivyonusurika Akizungumzia umuhimu wa daraja hilo la Busisi- Kigongo, Rais Magufuli alirejelea tukio la miaka ya 1990 ambalo watu 12 wa familia moja walikufa maji wakati wakivuka kwa mitumbwi baada ya kivuko kilichokuwapo kupata matatizo.

“Siku feri ilipokuwa ikiharibika ni lazima upande mitumbwi,” alisema. Akisimulia alivyonusurika, Magufuli alisema alipofika Busisi, aliambiwa feri ya MV Geita iliyokuwa ikitoa huduma katika eneo hilo imeharibika na kushauriwa apande mtumbwi umvushe hadi ng’ambo (Kigongo).

Kwa mujibu wa Rais, alizingatia kwamba hana uzoefu wa kuogelea, asingeweza kuvuka kwa mtumbwi hivyo aliamua kuzunguka kwa kupita kivuko cha Kamanga.

Alisema alipofika Mwanza mjini, aliambiwa miongoni mwa watu waliopanda mitumbwi siku hiyo, watu zaidi ya 12 walifariki wakati wakivuka. Licha ya vifo vya ajali mitumbwi, Rais alisema wapo wengine (wagonjwa) kutoka maeneo mbalimbali kwenda Hospitali ya Bugando, Mwanza walipoteza maisha wakisubiri feri kabla ya kuvuka baada ya kukuta ama haipo au imeharibika.

Waliodhani haiwezekani

Akieleza uamuzi wa kujenga daraja hilo, Magufuli alisema unatokana na ahadi alizotoa mwaka 2015 wakati akiomba kura.

Alisema, “nikiwa uwanja wa Kirumba (Mwanza) nikiomba kura, nilisema nitajenga daraja na wapo ambao walisema hili haliwezekani.”

“Wapo watu ambao hawakuamini hiki,” alisema na kusisitiza kuwa alitoa ahadi hiyo akiamini kwamba itawezekana kwa kuwa tayari kulikuwa na madaraja makubwa 77 yaliyokwishajengwa nchini na isitoshe, walioshiriki walikuwapo miongoni mwao akiwa ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mfugale aliyeandaa michoro ya madaraja mbalimbali.

Akimshukuru Mfugale kwa kuandaa mchoro wa daraja hilo la Busisi-Kigongo haraka baada ya kutakiwa kufanya hivyo, Magufuli alisema, “nashukuru kwa kutangaza haraka zabuni hii kwa sababu wangechelewa wakasubiri urais wangu ukaisha, ajeye angeweza kufuta huu mradi.”

Alipongeza pia Bunge chini ya Spika Job Ndugai akisema lilipopelekewa mapendekezo, mradi ulipitishwa.

Akieleza furaha ya mradi huo, Magufuli alisema mafanikio yanatokana na kuminya fedha za mafisadi. Rais Magufuli alisisitiza kuwa ni mtumishi wa Watanzania na ataendelea kutumika kadri wanavyoona anafaa.

Alisema miradi mbalimbali inayotekelezwa ni matokeo ya ushirikiano wa pamoja. Tutunze amani “Maendeleo tunayoona yanaendana kwa sababu tumeamua kushikana pamoja, vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi,” alisema na kuhimiza Watanzania kutunza amani kwa kuepuka kubaguana kwa misingi ya dini, sura au hali.

Alisema wakati nchi ikijiandaa kusherehekea miaka 58 ya uhuru (wa Tanganyika) kesho, wananchi hawana budi kudumisha amani na upendo maendeleo yaendelee kuonekana.

“Penye amani pana maendeleo.” Ataka kasi ya ujenzi Alimtaka wakandarasi , Kampuni ya CCECC kutoka China na China na China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) kujenga usiku na mchana ukamilike mapema.

“Naomba makandarsi wasimamie vizuri mradi huu, hizi ni fedha za Watanzania masikini. Fedha yao waliyokusanya wameamua kuweka uwekezaji hapa ndiyo maana nawaomba wakishaanza, kwa sababu fedha ya kulipa asilimia 50 tayari ipo imewekwa.

Fedha ya kulipa fidia nayo ipo,” alisema. Fidia kupisha mradi Rais Magufuli alisisitiza kwamba wote watakaoguswa na mradi huo watalipwa fidia na kusema zaidi ya Sh bilioni 3.145 zimetengwa kwa ajili hiyo ya wanaostahili; ambao ni waliofuatwa na barabara.

Mradi huo ni kiungo muhimu cha usafiri kati ya Mwanza na mikoa mingine ya kanda ya ziwa pamoja na nchi jirani ikiwamo Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda. Utakapokamilika utachochea shughuli za uzalishaji hususani kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara na utalii.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

1 Comments

  • avatar
    Hassani mussa
    08/12/2019

    tunakuombea kwa mungu rais wetu jpm akuepushe nawanao kusema vibaya, ili uitengeneze nhi yetu. AMINA

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi