loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mfanyabiashara Mufuruki kuagwa leo

MFANYABIASHARA maarufu nchini na Mwenyekiti Mwasisi wa Jukwaa la Maofi sa Watendaji Wakuu (CEOrt), Ali Mufuruki (61) anatarajiwa kuagwa leo jijini Dar es Salaam.

Mwili wa Mufuruki uliwasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA jana jioni ukitokea katika Hospitali ya Morningside, Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa Jumamosi, Desemba 7, mwaka huu na baadaye kufariki usiku wa siku hiyo. Simanzi na majonzi na vilio vilisikika viwanjani hapo wakati mwili huo uliposhushwa kutoka kwenye ndege binafsi iliyokuwa na mwili huo.

Baadaye ulipakiwa kwenye gari maalumu na kupelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo. Msemaji wa familia na rafiki wa karibu wa Mufuruki, Gilman Kasiga aliliambia gazeti hili jana kuwa leo saa 3:00 asubuhi mwili wa mpendwa wao utapelekwa kwenye moja ya kumbi za Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.

Mufuruki aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika taasisi za umma na binafsi, nje na ndani ya nchi ikiwamo Mwenyekiti Mwasisi wa CEOrt yenye kampuni zaidi ya 50 na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya InfoTech Investment Group Ltd, alijisikia homa wiki moja iliyopita na alipofanyiwa vipimo katika Hospitali ya Aga Khan aligundulika kuwa na homa ya mapafu.

“Baada ya uchunguzi wakabaini ana homa ya mapafu, madaktari wa Aga Khan na daktari wake kwa wiki hii moja walihangaika naye sana, wakashauriana na familia na kukubaliana apelekwe Afrika Kusini kwa matibabu zaidi,” alisema Kasiga.

Kwa mujibu wa Kasiga, Mufuruki alikodiwa ndege na kukimbizwa moja kwa moja katika Hospitali ya Morningside jijini Johannesburg jioni ya Jumamosi Desemba 7, mwaka huu, lakini usiku wa saa tisa za Afrika Kusini (saa 10 alfajiri ya Tanzania) alifariki dunia. Kasiga alisema Mufuruki alikuwa mtu wa watu, aliyependa jamii nzima ikombolewe kifikra hasa katika masuala ya kiuchumi ambako kudhihirisha hilo, mwaka 2017 waliandika pamoja kitabu kinachohusu masuala ya viwanda, sera, ujenzi, na alipigania mabadiliko katika sekta ya elimu kwa Watanzania.

Taasisi, mashirika, kampuni na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi akiwamo Rais John Magufuli, juzi kupitia akaunti zao za twitter walioeleza kushtushwa na kifo hicho na walimuelezea Mufuruki kuwa mtu makini, mzalendo, mchapakazi na aliyetumia sehemu kubwa ya maisha yake kuisaidia jamii. Mufuruki, mhandisi mwenye shahada ya ubunifu wa mitambo, ni mshauri katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na mazingira na amewahi kushika nyadhifa nyingi katika kampuni na taasisi za kiuchumi, biashara na uhandisi za nchini Tanzania, Kenya, Uganda, Marekani, Uholanzi, Ujerumani na Denmark.

Mfanyabiashara huyo mwenye utajiri wa Dola za Marekani milioni 110, sawa na zaidi ya Sh bilioni 250 amewahi kuwa mwenyekiti wa bodi nyingi za mashirika, taasisi, kampuni na amekuwa pia mkuu wa ubunifu katika Kampuni ya Uhandisi ya Taifa jijini Dar es Salaam. Ameacha mjane (Saada) na watoto wanne.

Pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Bodi za Kukuza Utalii Afrika Mashariki, Stanbic Bank Tanzania na Mfuko wa Jamii wa Kupambana na Ukimwi chini ya Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na Mjumbe wa Jukwaa la Rais la Wawekezaji (IIRT). Alihusika pia kuanzisha Kampuni ya EACP ya Kenya, mwekezaji katika Kampuni ya Chai Bora Tanzania, anamiliki maduka makubwa ya nguo ya Woolworths nchini na Uganda kama wakala na amekuwa Mjumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC).

Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Simu ya Vodacom kuanzia Novemba 2017, nafasi ambayo alitangaza kuwa angeachia ngazi kuanzia Desemba Mosi, mwaka huu.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi