loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Shein afanya mageuzi makubwa ya Tehama Z’bar

MIAKA tisa ya uongozi wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein imeleta mageuzi makubwa katika nyanja za Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuleta matokeo chanya ambapo wakazi visiwani Zanzibar wanaweza kupata vitambulisho vya ukazi, vyeti vya uzazi na vifo katika ngazi ya wilaya.

Mafanikio ya Tehama visiwani hapa yamechochea maendeleo na ustawi sekta mbalimbali za uchumi na kijamii ambapo hilo limewezekana kutokana na ubia na mashirika mbalimbali ikiwamo kampuni kubwa ya Kichina ya mawasiliano ya ZTE Corporation iliyotoa mchango mkubwa.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Ali Mohammed Shein, imefanikisha upatikanaji wa huduma za kimtandao na hivyo zote kuweza kuunganishwa katika Mkongo wa Taifa na kuimarisha utoaji wa huduma,” Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Zanzibar, Shukuru Awadhi Suleiman.

Suleiman alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka Tanzania Bara waliotembelea Zanzibar kujifunza namna miradi mbalimbali ya Tehama ilivyotekelezwa na kuchochea maendeleo ya kijamii.

Alisema serikali kupitia Wakala wa Mkonga wa Taifa wa Mawasiliano Zanzibar imefanikiwa kuziunganisha ofisi 11 za wilaya za Wakala wa Usajili wa Vitambulisho vya Ukazi, Uzazi na Vifo.

“Haya yote yamewezekana kupitia maendeleo ya Tehama ambapo huduma zote hizi zinatolewa ikiwemo vyeti ya ndoa, talaka, kuzaliwa na vitambulisho vya ukazi vinatolewa moja kwa moja katika ngazi ya wilaya,” alisema.

Alisema hapo awali kabla ya awamu ya Rais Shein, huduma hizo zilikuwa zinamlazimu mtu kusafiri mbali hadi makao makuu kwaajili ya kupata huduma hiyo na kwa sasa imebakia historia tu.

“Katika kuhakikisha watu wanapata huduma bora ya mawasiliano, serikali chini ya Rais Shein imewekeza katika mkonga wa mawasiliano uliolazwa baharini kutoka Dar es Salaam hadi Unguja na mwingine kutoka Tanga hadi Pemba,” alisema mhandisi huyo.

Kwa mujibu wa Suleiman, Mkonga wa Taifa umewasaidia sana watoaji wa huduma za intaneti kupitisha kiwango kikubwa cha intaneti kutoka Tanzania Bara kwenda visiwani vya Zanzibar.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi