loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nafasi ya kilimo hai katika usalama wa chakula

“UGAIDI mkubwa kwa sasa si mashambulizi, lakini ni katika chakula kwani watu wengi wanaweza kuangamia ikiwa haitazingatiwa usalama wa chakula kwa afya za Watanzania.”

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema hayo akisisitiza nchi kuzingatia kilimo hai ili kulinda afya za walaji. Alikuwa anazungumza katika mkutano wa kitaifa wa masuala ya kilimo hai uliofanyika jijini Dodoma na kukutanisha wadau wapatao 300. Anasema ili kuleta mabadiliko chanya katika kilimo hai kwa serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, ni muhimu kuungana kuweka msisitizo wa kilimo hai nchini.

Katika mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu isemayo: “Kufikia Uhakika wa Chakula, Uboreshaji Maisha, Viwanda na Utayari wa Kuyakabili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Ubunifu wa Kilimo Hai,” kulikuwa na maonesho ya bidhaa za kilimo hai, ubora wake, mbegu na jinsi ya kukabili wadudu waharibifu bila kutumia kemikali.

SHERIA /KURUGENZI

Katika ufunguzi wa mkutano (semina) huo, Waziri Hasunga anasema katika sheria mpya ya kilimo, watazingatia masuala ya kilimo hai ikiwemo kuanzisha kurugenzi inayojitegemea kwa ajili ya kusimamia kilimo hicho endelevu.

Anasema mbegu za asili zitalindwa katika sheria hiyo mpya kwa ajili ya usalama wa chakula na afya na sheria hiyo mpya inatarajiwa kukamilika mwakani. Anasema kupitia mabadiliko ya Sera ya Mwaka 2013 na sheria ya kilimo, watazingatia masuala ya kilimo hai ili kukabiliana na ongezeko la watu.

Kwa mujibu wa Hasunga, Serikali inaandaa wananchi wake kuepuka matumizi ya kemikali za dawa na mbolea na kugeuzia katika viuatilifu, kwani duniani kuna uhitaji mkubwa wa chakula kisicho na kemikali.

“Hii inawezekana kwani kwani imebainika kuwa dawa ya asili zinazotengenezwa kuepuka wadudu waharibifu zinatumia zao la pareto ambalo Tanzania ni ya pili kwa kuzalisha zao hilo duniani,” alisema.

Hasunga anasema ugaidi mkubwa kwa sasa siyo milipuko ya silaha, bali kutumia chakula chenye kemikali kuangamiza watu, hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wa chakula ili kudumisha afya kwa Watanzania.

Anabainisha kuwa Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo hai. Nyingine ni Uganda, Ethiopia, Kenya na DRC, hivyo katika kuongeza nguvu, sheria ya ushirika itakapotungwa kilimo hai kitawekwa ili kuwa endelevu na kuondokana na magonjwa yanayogharimu serikali. Anasema mpaka sasa Tanzania ina hekta milioni 44, lakini zinazotumika ni hekta milioni 10 pekee hivyo kuna nafasi kubwa kutekeleza kilimo hai katika maeneo yaliyobaki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa anasema sera ya kilimo hai ipo, lakini haijafanyiwa kazi kwa kiwango kinachostahili. Mgimwa anasema katika mabadiliko ya sheria na sera,ni vema kanuni zifanyiwe kazi haraka ili kuwalinda na kuwawezesha wakulima katika kilimo hai. Anasema nchini kuna wakulima 270,000 katika hekta 150,000 wanaolima kilimo hai.

WATAALAMU WA KILIMO HAI

Ilibainishwa kuwa, hivi karibuni nchini kutaanza kupata wataalamu wa kilimo hai katika ngazi mbalimbali ili kupata maofisa ugani kwenye kilimo hai. Vyuo mbalimbali vitaanza kutoa vyeti, diploma na shahada ya uzamivu kwa wataalamu wa kilimo hai nchini kwa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) kufanya marekebisho ya mitaala na kuruhusu utoaji wa cheti na astashahada ya kilimo hai huku Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kikiwa kimeanza kutoa shahada ya uzamivu katika kilimo hicho.

Hatua hiyo itasaidia nchi kuongeza uzalishaji wa mazao hai yenye ubora, hivyo kukamata soko nje ya nchi pamoja na nchi kupunguza matatizo ya magonjwa mbalimbali yanayosababisha na uzalishaji mazao kwa kutumia kemikali.

Meneja wa Mradi nchini kutoka Shirika la Lutheran World Relief, Moses Kabogo anasema kuhakikisha wanapatikana maofisa ugani wa kutosha katika kilimo hai, Nacte imefanya mabadiliko katika utoaji elimu na kuanza kuruhusu utoaji wa elimu hiyo. Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Kalunde Sibuga anasema katika mwaka huu wa masomo, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imepitisha wanafunzi kusoma shahada ya uzamivu katika kilimo hai. Anasema shahada hiyo itasaidia kupata wataalamu zaidi huku wakiendelea na utafiti unazosaidia katika kilimo endelevu huku wakirutibisha ardhi.

“Katika kuhakikisha elimu itapatikana inavyostahili, tuna kitivo cha kilimo cha ekolojia ili kufanya kazi na wakulima na tayari tumeanza na wilaya za Masasi, Morogoro na Bagamoyo,” anasema.

Katika hili, Waziri Hasunga anasema: “Ipo haja taasisi zote kubadili mitaala ili wanafunzi kabla ya kuhitimu elimu, waende vijijini kufanya kazi kwa vitendo ndipo wapate vyeti.”

UTAFITI

Profesa Sibuga anasema pesa zinazoelekezwa katika utafiti wa kilimo cha ekolojia ni kidogo tofauti na kilimo cha kemikali kutokana na nchi kutokuwa na sera madhubuti katika kilimo hicho. Ametaka serikali kuwa na sera ya kilimo hai pekee ili kubainisha malengo yake na kuwezesha utafiti katika kilimo hicho kupewa kipaumbele na taasisi za kimataifa kutoa fedha za utafiti.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Agness Nyomoro anasema utafiti unaendelea katika maeneo mbalimbali ili kupata dawa za asili kutibu haraka magonjwa katika mboga kukabiliana na changamoto ya wadudu katika mazao hayo.

MAZAO YA KIPAUMBELE

Wizara ya Kilimo imetaka wadau wa kilimo kubainisha mazao ya kipaumbele katika utekelezaji wa kilimo hai yatakayokuwa na miongozo ya kufuata kwa kila zao kuanzia kupanda mpaka kuvuna.

Hatua hiyo itasaidia mazao hayo kusimamiwa kwa mapana na kuwa endelevu huku ikikidhi viwango stahili kulingana na uwezo wa nchi huku kukiwa na waratibu watakaosaidiana na serikali kufanya maamuzi kuhusu kilimo hai. Pia, itatoa fursa ya utekelezaji wa mazao ya kipaumbele kati ya mazao zaidi ya 80 yaliyopo nchini kuliko kutekeleza mazao yote kwa pamoja.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo, Enock Nyasebo anasema serikali inatambua juhudi za wadau katika kuendeleza kilimo hai. Anasema kilimo hai kinapaswa kuwa agenda ya kitaifa kwa kuchagua mazao ya kipaumbele kwa kuunda timu ya uratibu itakayoendeleza kilimo hicho kwani serikali ipo tayari kwa mijadala ya kuimarisha.

Katika kuimarisha agenda hiyo, ni vema kutoa elimu kwa wadau wote ikiwemo serikalini ili kuleta uelewa wa pamoja hususan katika sheria na sera. Anasema soko la dunia kwa kilimo hai lina thamani ya dola bilioni 90 hivyo mazao ya kilimo hai kuwa na fursa kubwa kibiashara na kuboresha afya kwani wizara haipingi taratibu za kilimo cha kisasa, bali inatakiwa kuhakikisha wanasimamia matumizi ya kemikali hasa kudhibiti wadudu kwani kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi.

WADAU WA MAENDELEO

Mwakilishi mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), Fred Kafeero anasema ili kupambana na njaa, lazima kutekeleza agenda ya mwaka 1930 ya kilimo endelevu. Anasema utashi wa kisiasa ni umuhimu katika mapinduzi ya aina hiyo na wako tayari kutoa mchango wao katika kuchukua hatua zinazofaa na endelevu.

Mwakilishi wa Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Cecile Frobert anasema serikali ya Ufaransa imeongeza ufadhili katika kusaidia sekta hiyo hadi kufikia Euro milioni 20, ikiwa ni mara mbili kwa mwaka jana ili kusaidia nchi kufikia kipato cha kati mwaka 2025.

Anasema wamesaidia kuandaa mkutano huo ili kuunga mkono katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ili kuzingatia lazima kuangalia viuatilifu kuathiri mazingira, ardhi, udongo na maji pamoja na kiwango kikubwa mazao na athari za baadaye.

“Tanzania kwa sehemu kubwa haijaathirika na viuatilifu hivyo inabidi kuokoa ardhi isizidi kuharibika kwani nusu ya wakulima wamepata vyeti vya kilimo hai huku mahitaji ya mazao ya kilimo hai yakiwa makubwa katika nchi za Marekani, Ulaya na Asia,” anasisitiza.

Anasema kitakwimu, mahitaji ya mazao hayo yanaongezeka kila mwaka kwa asilimia 20 hivyo Ufaransa inasaidia Tanzania katika miradi miwili ya dola milioni mbili katika nchi tatu za Afrika zikiwamo Tanzania na Uganda. Anasema pia wametoa dola bilioni moja kusaidia mashirika mbalimbali duniani kuimarisha kilimo hai na kulinda mazingira. Aliwakaribisha Watanzania katika Mkutano wa 20 wa Kimataifa katika Kilimo Hai utakaofanyika mwaka 2020 na kushirikisha nchi 50.

Mkurugenzi wa Taasisi ya kuendeleza Kilimo Hai nchini na Afrika, Jordan Gama anasema makubaliano yatapelekwa serikalini ili maoni ya wadau yaingizwe kwenye mabadiliko ya sheria na sera ya kilimo.

Ametangaza mkutano wa kimataifa utakaofanyika Ufaransa mwakani na maonesho ya kilimo hai yatakaofanyika mwaka 2021 nchini Morocco na kutaka wakulima na wafanyabiashara kutumia fursa hizo kupata masoko duniani huku Februari mwakani kukiwa na uzinduzi wa programu maalumu inayofadhiliwa na Ufaransa katika kuboresha kilimo hicho nchini.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi