loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wenye ulemavu watengeneza bidhaa bora wateja wachache

“WATEJA wetu bado ni watu binafsi; mtu mmoja mmoja; na hao japo ni wachache, wengi wao wanapenda na kuvutiwa na ubora wa viatu tunavyotengeneza hapa, lakini uwezo wao kifedha ni mdogo, hivyo wanataka kupunguziwa bei hadi kiwango ambacho hakina maslahi kwetu…”

“Ili kuwapata wateja kama hao, inabidi tukubaliane na ombi lao la ‘kubandika’ (yaani kulipia kwa kuweka pesa kidogo kidogo) hadi wanapokamilisha malipo na kuchukua bidhaa.”

Ndivyo anavyosema Mwenyekiti wa kikundi cha mafundi viatu wenye ulemavu wa Buza Disabled Partnership, Amir Salim, wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu kiwanda chao cha kutengeneza viatu, mikoba na bidhaa nyingine za ngozi kilichopo wilayani Temeke, eneo la Njiapanda ya Kitunda, Buza kuelekea Mwanagati.

Katika mazungumzo hayo yaliyowashirikisha mafundi wenzake wenye ulemavu wakiwamo Amanzi Likwata, Hashimu Hussein, Amidu Ally, Twaha Mohammed, Nassoro Tayari, Michael Masanja (Mweka Hazina) na Anderson Gwemarika (Katibu wa Kikundi), wanasema wamejikita kuzalisha viatu, pochi na huduma nyingine, kwa kutumia ngozi halisi ili kuepusha hasara kwa wateja wao na kwamba, hilo watalisimamia hadi mwisho.

“Katika kiwanda hiki, kila kitu tunachozalisha au kutengeneza, ni original (halisi); tunatumia ngozi orijino, soli orijino, gundi orijino; hatutumii plastiki wala vitu vya ‘magumashi’ kwa tamaa ya pesa; hapana… kiwanda hiki ni cha kikundi cha watu wanaojali wateja, utu na thamani ya pesa ya mteja,” anasema Amanzi.

Wanasema kiwanda chao kinazalisha viatu vya kike na vya kiume kwa kutumia ngozi halisi vikiwa katika aina, mitindo na saizi mbalimbali kutegemea mahitaji ya wateja.

“Bei inategemea muundo wa kiatu; na ukubwa wa kiatu,” anasema Mwenyekiti (Salim) huku Katibu akifafanua: “Unajua, kiatu cha mtoto kinatumia ngozi ndogo hivyo, bei yake pia itakuwa ndogo tofauti na kiatu cha mkubwa au ‘travota’, au buti ambacho hutumia ngozi kubwa, gundi nyingi na soli kubwa pia.”

Kutokana na namna walivyoamua kutumia vipaji vyao kujitafutia vipato na riziki halali, wanasema wanamwomba Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, vijana , Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mahagama, Naibu Waziri wake, Stella Ikupa, na viongozi wengine mbalimbali kutembelea kiwanda chao ili kuona namna mafundi hao wenye ulemavu wanavyochapa kazi bila kusingizia maumbile yao ili kukaa barabarani na kuishi kwa kuombaomba.

“Tunamwomba Rais atutembelee; aje ashuhudie namna tusivyotaka kumwangusha na tulivyoitikia mwito wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda; na tunamshukuru sana na watendaji wake akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi, na Ofisi ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa nasi bega kwa bega,” anasema Nassoro Tayari ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Usalama Barabarani kwa wenye Ulemavu Tanzania.

WALIVYOANZA

Kwa mujibu wa Mwenyekiti na Katibu, kikundi cha Buza Disabled Partnership kilianza Juni, 2019, kisha kikaomba mkopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kupitia ushonaji wa viatu kwa vile ni wataalamu ambao wamekuwa wakifanya kazi hiyo ingawa kila mmoja alikuwa kivyake.

Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 20, Kifungu 37A (4) iliyotungiwa kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo ya vikundi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019, halmashauri zote nchini zinapaswa kutenga asilimia mbili ya mapato ya ndani kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

“Tuliomba vifaa, lakini wale kwa utu na utaalamu wao, wakatulipia pango kwa miezi 6 Sh milioni 1.2 ambayo ni sehemu ya mkopo. Kisha wakatuletea vifaa yaani cherehani 3 za umeme, mashine ya kisasa ya kukatia ngozi, mashine ya msasa, ngozi yenye thamani ya Sh milioni 1.5, jozi 200 za soli za viatu na gundi vyote vikiwa na thamani ya Sh 46,387,200,” anasema Katibu wa Kikundi, Gwemarika.

Mafundi hao wanasema waliamua kujiunga kwani wanaamini umoja ni nguvu maana mkiwa wengi, mnachangia ujuzi na karama na pia kwamba, kufanyia kazi katika kuta za nyumba zao au katika viambaza vya maduka hakuna mwisho mzuri.

Wanasema hawafurahi kuona watu wengine wenye ulemavu wakizungukazunguka barabarani wakifanya kazi za kuombaomba, badala ya kutumia vipaji vyao kuzalisha mali na kujipatia riziki. Wanaomba serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma mintarafu namna ya kujiajiri kwani wengine wanakuwa ombamba kwa kukosa elimu namna ya kujiunga na kufanya ujasiriamali, kwa kadiri ya uwezo na maumbile yao.

SHUKRANI

Wanasema wanaishukuru serikali kwa kutekeleza mpango huo wenye manufaa kwa wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na jamii kwa jumla.

MAFANIKIO

Wanasema wamefanikiwa kujiunga pamoja na wanatamani wengine wenye ulemavu wajiunge kwani umoja na nguvu na penye wengi hapaharibiki kitu.

“Kitendo cha kujiunga, kutembelewa na kufanyiwa ukaguzi hadi kuaminika na kupewa mkopo wa vifaa vya mamilioni ya pesa, ni imani ya jamii kwetu na ni mafanikio makubwa pamoja na namna wateja wanavyozidi kutufahamu na kuja kutuunga mkono,” anasema Mwenyekiti.

MATARAJIO

Katika mazungumzo ya pamoja, mafundi hao wenye ulemavu wa miguu wanasema wanatamani kiwanda chao kifahamike zaidi kwa ubora wa huduma na bidhaa. Wanapenda pia kuhamasisha zaidi watu wenye ulemavu kujiajiri na wao kuwa mfano katika kuendesha uchumi wa familia zao na kuchangia katika pato la taifa kupitia kazi wanazofanya.

CHANGAMOTO

Mwenyekiti anasema awali mafundi wanachama walikuwa wakifanya shughuli zao za ufundi sehemu mbalimbali kila mmoja katika eneo lake wakitumia sindano za mkono, hivyo mashine za kisasa wanazotumia katika kiwanda chao, hawajazizoea na kuzitumia ipasavyo. Kutokana na hilo, Gwemarika anasema ili kulinda ubora wa huduma na bidhaa zao kwa wateja, pale wanapoona utaalamu wao hautakidhi kiu ya wateja ipasavyo wanakodi wataalamu wenye uzoefu wa kutumia mashine zaoi za kisasa kwa kuwalipa Sh 2,500 kwa kukata na kushona.

“Kadhalika katika kupandisha (kuunda sura ya kiatu) tunamlipa mtaalamu Sh 2,500 kwa hiyo kila jozi tunamlipa Sh 5,000. Idadi ya jozi hutegemea mahitaji na kiasi cha pesa tulicho nacho,” anasema Gwemarika.

Changamoto nyingine kwa mujibu wa Mweka Hazina wa kikundi, Masanja, ni ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa ajili ya kusafirisha viatu kutafuta soko hali ninayowalazimu kukodi bajaji.

“Ugumu uko hivi, unaweza kukodi hata hiyo bajaj, ukapeleka mzigo sokoni, lakini usiuze ingawa utakuwa umetangaza biashara… Tunatamani kupata usafiri wetu wa uhakika wa kutafutia masoko katika maeneo mbalimbali,” anasema Masanja.

Anaongeza: “Mtaji bado shida, hivyo hata mahitaji ya kawaida ya kibinadamu hasa katika hatua hizi za mwanzo ambazo bado tunajijenga na kujiimarisha na hatujaanza kunufaika kiuchumi na kifamilia maana licha ya kazi nzuri hizi tunazofanya hapa, tuna miezi minne tu tangu tuanzishe kiwanda hiki.”

Anasema kwa sasa biashara ni ngumu kwani watu hawajawafahamu wala kuwazoea. Kutokana na hali hiyo, anasema mara nyingi hutokea siku wakazalisha viatu, lakini wasiuze hata jozi moja.

“Soko ni gumu sana, hatujapta order (maombi) kamili na kubwa ndiyo maana tunataka wateja; watu binafsi na taasisi waje watujaribu maana tunaamini hawatajuta na hao ndio watakuwa mabalozi wetu,” anasema Masanja.

Wanasema ukosefu wa soko unawafanya wauone ugumu wa kufanya marejesho ya mkopo ili unufaishe na wengine. Ili kukabili changamoto ya uhaba wa wateja na soko la uhakika, Gwemarika anasema: “Tunaomba Serikali na hasahasa halmashauri itusaidie kupata soko la uhakika na njia mojawapo ya kufanya hili, ni kuzihimiza taasisi kama shule zilizo chini yao kununua viatu kiwandani hapa ili wanafunzi wote wawe na viatu vinavyofanana ambavyo ni ngozi halisi.”

Gwemarika anaongeza kwamba watu wanaofanya shughuli za ujenzi, wafanyakazi katika vituo vya mafuta, kampuni za ulinzi na hata vyombo vingine vya usalama wanaweza kuona namna ya kununua bidhaa kwao, “kwani sisi tunatengeneza hata mabuti.”

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi