loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wizara- REA msiruke kijiji

WIZARA ya Nishati imelitaka Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kuhakikisha haiachi wala kukiruka kijiji katika kuviunganishia umeme, kwani awamu ya sasa ndiyo ya mwisho ijulikanayo kama ‘baba lao’.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kwenye kitongoji cha Migude kata ya Kiromo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati akizindua uwashaji umeme.

Pia alizindua kisima cha maji ya kunywa kinachotumia mashine ya kuvuta maji inayotumia umeme kwenye kitongoji hicho.

Mgalu amesema awamu hiyo ndiyo ya mwisho ya REA awamu ya tatu mzunguko wa pili wa kusambaza miundombinu ya umeme kwenye vijiji ili ifikapo Juni 31 mwaka 2021 inapaswa kuvifikia vijiji vyote kabla ya kuhamia kwenye vitongoji.

“Awamu hii ndiyo ya mwisho ya kuvipelekea umeme vijiji kabla hatujahamia vitongoji hivyo, nawasihi Tanesco na REA kupitia vijiji vilivyobaki ili tukamilishe hili kwa vijiji kama alivyoagiza Rais John Magufuli kuwa ifikapo kipindi hicho vijiji vyote vipate umeme,” alisema.

Hadi sasa wamevifikia vijiji 8,115 kati ya vijiji 12,000 kote nchini ambapo bado vijiji 4,000 na hadi kufikia Juni 2020 vijiji 10,336 vitakuwa vimefikiwa na umeme na lengo litatimia Juni 2021.

“Pia naomba kuwashauri kuwa kuna haja ya kuwakopesha wateja hasa kwa wale wateja wa mijini ambao gharama zao ni tofauti kwani wao wanalipia kuanzia Sh 320,000 hadi Sh 500,000 tofauti na wale wa vijijini ambao wanaunganishiwa kwa Sh 27,000,” amesema Mgalu.

Aidha amesema kuwa kuna haja ya kuwakopesha umeme halafu walipe kidogo kidogo kupitia ankara zao za umeme kwani serikali inatumia gharama kubwa kuweka miundombinu ya umeme.

“Suala la gharama ya kuunganisha umeme kwenye manispaa na majiji hauwezi kuunganishwa kwa Sh 27,000 kwani Tanesco inajiendesha kwa mapato yake, hata hivyo serikali imesikia hoja ya kutaka bei hiyo iwe maeneo yote,” amesema.

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa amesema umeme umesambazwa vijiji vingi lakini baadhi havijafikiwa.

Kawambwa alivitaja baadhi ya vijiji ni pamoja na Mataya, Magole, Baikani, Goba Kimelemeta, Kitopeni A na B, Mtowanyanza, Ukani A na baadhi ya vijiji vya kata ya Fukayosi.

Diwani wa Kata ya Magomeni, Mwanaharusi Jarufu alisema jambo kubwa katika maendeleo ni umeme na barabara pamoja na maji.

foto
Mwandishi: John Gagarini, Bagamoyo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi