loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uhuru Tanganyika ulichochea Mapinduzi Zanzibar

KUPATIKANA kwa uhuru wa Tanganyika Desemba 9, mwaka 1961, kunatajwa kwamba kulichochea kwa kiasi kikubwa kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964, baada ya juhudi za kusaka uhuru kushindikana.

Hayo yamebainishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib (pichani) wakati akitoa salama za pongezi kwa Tanzania Bara kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru.

Alisema juhudi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kudai uhuru zilileta baraka kwa sababu ziliwafumbua macho wananchi wa Zanzibar na kusaka uhuru.

Khatib ambaye ni Waziri asiye na Wizara Maalumu amesema wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar walikuwa wakifanya harakati za pamoja za kudai uhuru kupitia Chama cha TANU pamoja na ASP kwa upande wa Zanzibar.

Kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) na Katibu wa Idara ya Uenezi ya Mkoa wa chama hicho, Baraka Shamte alisema uhuru wa Tanganyika kwa Zanzibar ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu ndicho kichocheo cha kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12 na baadaye kuzaliwa kwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema harakati za ukombozi wa Tanganyika chini ya Mwalimu Nyerere zilikuwa zikifanyika sambamba na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

“Wakati chama cha ASP kikizaliwa mwaka 1957, sherehe hizo zilihudhuriwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wakati huo akiwa kiongozi wa chama cha Tanu aliyepita Zanzibar kuelekea Tanga kwa ajili ya harakati za kuimarisha chama,” amesema.

Mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Fatma Karume amesema anaukumbuka uhuru wa Tanganyika wa mwaka 1961 ambao ndiyo uliowafumbua macho waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar kuuondoa utawala wa kisultani.

“Baada ya kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961...waasisi wakiongozwa na Abeid Karume waliingiwa na ushawishi mkubwa kuona Zanzibar nayo inakuwa huru kwa njia yoyote ile,” amesema.

Fatma amesema Karume na Nyerere walikuwa wakifahamiana kama wanaharakati wa kupigania Uhuru ambao walipata kukutana katika mikutano iliyofanyika Ghana pamoja na Lancaster, Uingereza.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi