loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maandalizi Daftari la Kura yapamba moto

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanikiwa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa zaidi ya asilimia 50 ya mikoa ya Tanzania Bara mpaka kufi kia Desemba 9, mwaka huu.

Uboreshaji huu ulioanza rasmi Julai 18, mwaka huu mkoani Kilimanjaro, unahusisha marekebisho ya taarifa za wapiga kura waliohama makazi, kuandikisha wapiga kura wapya waliofikisha miaka 18 na wale watakaofikisha umri huo siku ya kupiga kura mwaka 2020 pamoja kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa ikiwemo waliofariki dunia.

Taarifa hii ilithibitishwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage alipozungumza kwenye mkutano na wadau wa uchaguzi jijini Mbeya. Jaji Kaijage alisema tayari tume imeshaboresha taarifa za wapiga kura katika mikoa 16 ya Tanzania Bara na kazi inaendelea kwa mujibu wa ratiba na mgawanyo wa kikanda katika mikoa.

“Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ulikwishaanza na tayari mikoa 16 imekamilisha zoezi hili tangu kuzinduliwa kwake Julai 18, mwaka huu mkoani Kilimanjaro,” alisema Jaji Kaijage.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Dk Wilson Charles alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, wakati wa uboreshaji katika mikoa ya Dodoma na Mbeya, alisema lengo la tume ni kuandikisha wapiga kura milioni 30, ikiwa ni ongezeko la watu takribani milioni saba kutoka watu milioni 23 walioandikishwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.

“Lengo la tume ni kuandikisha takribani zaidi ya watu milioni 30, mwaka 2015 tulikuwa na watu milioni 23 na tunawashukuru Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hili kwani tulikuwa tunatazamia asilimia kumi na tisa mpaka sasa tumefikia asilimia 29,” alisema Dk Charles.

Aliongeza kuwa kazi ya tume ni kuhakikisha kuwa kazi hiyo, inafanyika kwa usahihi na pia kuhakikisha wananchi wanajitokeza kukamilisha zoezi. Kazi hiyo ya uboreshaji ambayo hufanyika kwa kipindi cha siku saba katika kila eneo, inaendelea katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani na inatarajiwa kufungwa rasmi Februari 16, mwaka 2020 katika mikoa ya Dar es Salaam na pwani na baadaye Machi 31 daftari litawekwa wazi.

Mikoa inayofuata katika uboreshaji huo ni Dodoma (Wilaya ya Mpwapwa), Mbeya (Chunya, Mbarali na Rungwe) na Iringa kuanzia Desemba 17 hadi 23, mwaka huu. Kuanzia Desemba 30 uboreshaji utafanyika katika mikoa ya Njombe, Ruvuma na Zanzibar, ikifuatiwa na Lindi na Mtwara ambako uboreshaji utafanyika kuanzia Januari 18, mwakani.

Mikoa mingine ni Tanga na Morogoro katika Halmashauri ya Ifakara na wilaya za Malinyi na Ulanga kuanzia Januari 23 huku Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Wilaya za Gairo, Kilombero, Kilosa, Morogoro na Mvomero zikitarajiwa kuanza kazi hiyo Februari 3, mwaka 2020. Pazia la uboreshaji linatarajiwa kufungwa na mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kuanzia Februari 10 hadi 19, 2020.

TAKRIBANI mifugo 12,000 katika vijiji ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi