loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Safari za treni Dar-Moshi kuwa 6 kuanzia Jumatatu

KUTOKANA na kuongezeka kwa abiria katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema kuanzia Jumatatu wiki ijayo, litaongeza safari za Dar es Salaam-Moshi kutoka nne kwa wiki (mbili kwenda na mbili kurudi) hadi sita.

Hatua hiyo inatokana na mahitaji makubwa yaliopo tangu treni ya abiria irejee kufanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi Ijumaa Desemba 6, mwaka huu baada ya miaka 25 ya kusitishwa, ambapo kwa safari moja zaidi ya abiria 500 walisafiri.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema jana kuwa mahitaji yameongezeka tangu kuanza kwa safari hizo, hasa kutokana na sherehe za mwisho wa mwaka, hivyo wanaangalia namna ya kuongeza safari ili kukidhi mahitaji.

“Mpangilio wetu tangu turejeshe safari za abiria ni kwenda Moshi mara mbili na Dar es Salaam mara mbili, inayofanya safari nne kwa wiki. Sasa tunataka iwe mara sita, ‘discussion’ (majadiliano) inaendelea hivi sasa,” alisema Kadogosa.

Kaimu Mkurugenzi Uendeshaji wa TRC, Focus Sahani alipoulizwa, alifafanua kuwa wanasubiri idhini ya mkurugenzi mkuu waongeze safari hizo Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kwa kuwa mahitaji yameongezeka na kufanya lazima ya ruti tatu kwenda na tatu kurudi kutoka mbili kwenda na mbili kurudi za awali.

“Mahitaji yapo mpaka Kigoma na Mpanda katika sherehe hizi za mwisho wa mwaka. Lakini kwa hii ya kaskazini, tumepanga kuongeza ruti tatu badala mbili na mabehewa mawili kutoka tisa na tunasubiri idhini ya DG (mkurugenzi) malengo yetu ni kuanza next week (wiki ijayo) Jumatatu,” alisema Sahani.

Sahani alifafanua kuwa ruti moja ya kulala inabeba abiria 72, na daraja la pili kukaa ni mabehewa mawili yanayobeba abiria 120 huku daraja la tatu likiwa na mabehewa matatu yanayobeba abiria 240 na kufanya idadi ya abiria 432.

Alisema kuna behewa moja ambalo ni hoteli na baa. Hata hivyo, alisema abiria hupanda na kushuka njiani na abiria wa Moshi hawapendi kusongamana, hivyo abiria wengi hupenda kukaa na wachache wanaopanda njiani kwa safari fupi kama Pugu, Korogwe, Kidomole baadhi husimama na kufanya idadi kufikia kati ya 550 hadi 600 kwa ruti moja.

Kuhusu mapato, Sahani alisema wanashirikiana na maofisa wa TRC wa Moshi na Dar es Salaam kuweka sawa hesabu. Aliahidi ataeleza mapato hayo tangu kuanza kwa safari leo.

Alisema nauli ya kukaa ni Sh 16,500 ikilinganishwa na mabasi Sh 32,000 na daraja la kulala ni Sh 39,000 na daraja la tatu ni Sh 10,700. Usafiri wa treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, ulisitishwa mwaka 1994 na treni ya mizigo ya Dar es Salaam- Arusha ilisitishwa 2007 na kurejea Julai mwaka huu huku ya abiria ikirejeshwa Desemba 6, mwaka huu.

TAKRIBANI mifugo 12,000 katika vijiji ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi