loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mimba shuleni zinavyogeuzwa ATM za watu Kishapu

“KUMEKUWA na mchezo unaofanyika upande wa wazazi, polisi, watendaji wa kata na vijiji na walimu kutafuta fedha kwa kupitia matukio ya mimba kwa wanafunzi… baadhi ya watu hawa wanapobaini tatizo la mimba kwa watoto na wanafunzi, hufurahi maana hupewa fedha na mwanafunzi kuendelea kuteseka akiwa katika umri mdogo.”

Ndivyo anavyosema Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba, akikemea tabia ya baadhi ya watu wakiwamo wazazi na watendaji katika taasisi za serikali, wanaogeuza tatizo la mimba shuleni kama mradi na mashine zao za kuchukulia pesa (ATM).

Anasema wanaofanya hivyo hushirikiana na waathirika na ndugu zao, kuficha tatizo hilo lisionekane huku watoto wakiendelea kuteseka na mimba kuendelea kuwepo. Hii inatokana na taarifa za vituo vya taarifa na maarifa vilivyojengewa uwezo na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wilayani Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga kuwa, mimba shuleni bado ni tishio kutokana na kutodhibitiwa kikamilifu.

Mkuu wa Wilaya anasema: “Kwa wazazi wengine, mtoto wa kike anakwenda kuogeshwa dawa za kienyeji wakimaanisha ‘nyota ing’ae’ ili akipita barabarani aitwe na wanaume na asipoitwa, wanaona dawa hizo hazifai na kuendelea kutafuta mganga mwingine; hili nalo linachangia kuwepo mimba za utotoni.”

Talaba anasema, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaombea ruhusa watoto wao shuleni wanapobaini wanafunzi hao wana mimba ili waendelee na mikakati ya kutoa mimba, jambo ambalo pia ni hatari kwa maisha ya watoto hao na uvunjaji wa sheria za nchi.

Anasema hadi sasa anayo majina ya watoto kadhaa ambao baadhi ya wazazi wao wamekimbilia ofisini kwake kuomba msaada baada ya kuzungushwa na jeshi la polisi. Anasema kwa mwaka 2019 wamebaini mimba 56 shuleni na zilizofikishwa mahakamani ni 30 huku 26 zikiwa bado zinafanyiwa upelelezi.

Katibu wa vituo hivyo wilayani Kishapu, Peter Nestory anasema TGNP imekuwa na utekelezaji wake katika kata 13 za wilaya hii ikiwemo Kata ya Ukenyenge ambayo imekuwa ikipewa elimu juu ya kupinga ukatili wa aina yoyote ndani ya jamii.

Anazitaja sababu kadhaa za kuwapo na kushamiri mimba za utotoni, Nestory anasema baadhi ya wazazi na watendaji wa serikali wameshindwa kuwajibika kuona vichocheo vya mimba shuleni, likiwamo suala la wanafunzi kutembea umbali mrefu wa takriban kilomita kumi kwenda na kutoka shuleni hali inayowafanya wengi wakiwamo wanafunzi wa kike, kupanga na kuishi ‘gheto’ mitaani kutokana na ukosefu wa hosteli.

“Kukosekana huduma za maji, wanafunzi hao wanatumwa kufanya kazi za kijamii na wazazi wao mfano kufuata maji umbali; tena unakutana nao nyakati za usiku wakiwa wameambatana na wanaume hujui kinachofanyika hapo matokeo yake mimba za utotoni,” anasema.

Aidha anasema siku zisizo za masomo watoto wa kike huenda kuchunga mifugo wao porini wanakumbana na vishawishi vya kubakwa na kuishia katika mimba za mapema shuleni.

Anasema TGNP imekuwa ikitekeleza miradi wilayani Kishapu kwa utoaji elimu dhidi ya vitendo vya ukatili na kuibua changamoto na mbalimbali katika katika kata za Songwa, Kishapu, Idukilo, Mwadui, Lohumbo, Kiloleli, Mondo, Maganzo, Bunambiyu, Mwaweja na Ukenyenge.

Kwa mujibu wa Peter, lengo la vituo hivi ni kuleta uhusiano mzuri kati ya jamii, serikali na familia katika kukuza maadili sambamba na kuondoa kasumba kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ni vya kawaida. Baadhi ya wazazi katika Kijiji cha Bulimba, Kata ya Ukenyenge Angelina Madaha na Suzan Kulwa, wanasema wapo wazazi ambao hawajapata elimu mintarafu kumlinda mtoto wa kike kwani nao wameonesha kufurahia mimba kwa wanafunzi.

“Tukio la binti ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Sekondari ya Ukenyenge kudaiwa kupewa mimba na baba yake mzazi hilo limeonekana katika familia kulikubali bila kuona madhara yake na kumueleza afiche ukweli, lakini sasa amejifungua hana msaada wowote baadhi ya ndugu wamemtenga,” anasema Suzana.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ukenyenge, Juma Maganga anasema baadhi ya wazazi wanachangia uwepo wa mimba kwa watoto wakidhani ni jambo la kawaida. Anasema kwa mwaka huu (hadi Novemba) wanafunzi saba wamepata mimba.

Mwenyeki wa Bodi ya Shule ya Ukenyenge, Shehe Othman Mohammed anataka itungwe sheria inayotaka yeyote anayempa mimba mwanafunzi, kulipa gharama zote zikiwamo alizogharamia mwanafunzi huyo katika masomo yake, malipo ya mishahara ambayo angelipwa baada ya masomo na kuajiriwa, pamoja na malipo ya kustaafu ili liwe fundisho.

Diwani wa Viti Maalumu, Josephine Malima anasema miongoni mwa njia za wanafunzi kukataa vishawishi vinavyowasababishia mimba ni kukaa nyumbani au shuleni pamoja na kurudi nyumbani mapema, badala ya kupita mitaani na kufika nyumbani usiku, hali itakayowaepushia ubakaji.

“Wanafunzi mtambue mnayo thamani kubwa katika jamii; mkisoma mtaisaidia taifa, epukeni vishawishi vinavyowafanya mjipeleke wenyewe maana mkivikataa vishawishi hakuna wa kuwalazimisha,” anasema Diwani Malima.

Diwani wa Kata ya Ukenyenge, Anderson Mandia anasema moja ya mikakati waliyoipanga katika mikutano ya hadhara kama njia ya kudhibiti uwepo wa mimba kwa wanafunzi, ni wanafunzi wa kike kushinda na sare za shule ili wanaowarubuni wawatambue na kuwaogopa.

Msimamizi wa Dawati la Jinsia katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Tarafa ya Negezi, Kata ya Ukenyenge, Clement Mgaya anasema: “Wazazi nao wamekuwa hawaripoti matukio ya mimba kwa watoto wao; wababaki kulalamika chini chini na hata wakiripoti, hawatoi ushirikiano wanapohitajika kutoka ushahidi mahakamani. Matokeo yake, kesi yake ni kufutwa, lakini wakitoa ushahidi wengi watatiwa hatiani.” Mgaya anasema licha ya kuwepo kwa sheria, jamii yenyewe inapaswa kutia mkazo katika kukataa ukatili wa aina yoyote kwa watoto ukiwamo wa ubakaji na mimba za utotoni na kwamba, jambo hilo linawezekana.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Kishapu, Ndola Masunga anasema baadhi ya wazazi hawatekelezi majukumu yao kwa kuruhusu watoto wao kumiliki vitu vya thamani, bila kujulikana vimepatikanaje.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Boniface Butondo anasema ni muhimu kuwa na upimaji wa wanafunzi kila baada ya miezi mitatu, badala ya wazazi na walimu kusubiri fununu ya mwanafunzi mwenye mimba.

“Upimaji wa watoto shuleni haufanyiki kisheria, hivyo sheria iliyopo isisitizwe kwa walimu wote kila baada ya miezi mitatu wanafunzi wapimwe… Isichukue muda mrefu bila kuwapima, mpaka mwanafunzi anakaribia kujifungua walimu wakiwa hawajui,” anasema Butondo.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Kahundi, anasema mwaka jana kulikuwa na mimba 66 kwa wanafunzi na kati ya hizo, mimba 6 zilitoka katika shule za msingi. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Claud Kanyorota anasema shida kubwa iliyopo katika suala la mimba ni viongozi kushindwa kulisimamia kikamilifu huku jamii na baadhi ya wazazi wakiendelea kuficha ukweli. “… unapokea kesi vizuri, binti anapimwa ushahidi unakamilika, lakini mwishowe shahidi anageuka,” anasema.

Mwakilishi kutoka Kitengo cha Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Shinyanga, Alphonce Kasenyi, anasema wanafunzi ni sawa na nyara za serikali hivyo, lazima zitungwe sheria ndogondogo kuwalinda. Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela anase maazimio yaliyofikiwa na wadau wa elimu ni kutoa muongozo kwa halmashauri kuhusu mimba shuleni ili tatizo hili likomeshwe.

Mwanaidi Bilali, mkazi wa kijiji cha Matandu, wilayani ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi