loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uvuvi wa kitalii wa samaki njege unavyopamba Morogoro

NJEGE ni aina ya samaki anayepatikana katika mito na maziwa. Samaki huyu kisayansi ameainishwa katika familia ya ‘alestidae’. Samaki huyu ambaye ni mwindaji, asili yake ni Bara la Afrika.

Watalii wengi huvutiwa kumvua kutokana na mwonekano na sifa yake kuwa mwindaji katili awapo majini. Hali hiyo imemfanya kuitwa jina la “tiger fish.” Anaweza kufika kilo 70 na ana meno marefu na makali kama chuimilia (tiger). Samaki huyu anapatikana katika mito yote inayozunguka Kanda ya Msolwa, Pori la Akiba la Selous.

Mito hiyo ni Kilombero, Ruaha na Ulanga. Uvuvi wa kitalii wa samaki huyu hufanyika kwa kumkamata kwa kutumia ndoano na kumrudisha majini baada ya kumtazama, kuchukua vipimo na kumpiga picha. Aina hii ya utalii haina madhara katika uhifadhi na ikolojia. Vipimo vya samaki huyu hutumika na wavuvi wa kitalii katika mashindano ya uvuvi wa samaki wa aina hii sehemu nyingine duniani.

Katika Kanda ya Msolwa, aina hii ya utalii ilianza mwaka 2007 na unaendelea mpaka sasa. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, idadi ya watalii imeendelea kuongezeka kwa kasi kila mwaka. Mathalani, kwa kipindi cha miaka ya 2007 hadi 2015 watalii walikuja kwa kundi moja mpaka mawili kwa mwaka tofauti na miaka ya 2016 hadi 2019 ambapo makundi ya watalii yameongezeka mpaka kufikia makundi kumi kwa mwaka.

Kuna kila dalili kuwa, utalii huu utaendeleaje kuongezeka zaidi miaka inayokuja. Aina hii ya uvuvi wa kitalii unaofanyika katika Mto Kilombero, Rwaha na Msolwa inayopita katika Pori la Akiba la Selous lililopo Kanda ya Kaskazini Magharibi linalosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa). Mkuu wa Kanda ya Msolwa, Augustino Ngimilanga, anaelezea aina hii ya utalii ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

Anasema taifa linaweza kujiingizia pesa nyingi za kigeni kutokana na aina hii ya utalii wa samaki aina ya ‘tiger fish.’

“Watalii wengi wa utalii wa aina hii wanatoka katika mataifa ya Afrika Kusini, Ufaransa, Ukraine na Uingereza,” anasema Ngimilanga na kuongeza: “Aina hii ya utalii imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza mapato ya fedha za kigeni mbali na utalii wa uwindaji na picha ambao umekuwa ukifanyika kwa kipindi kirefu.”

Anasema mtalii mmoja kwa siku analipa Dola za Marekani 103 pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT), lakini pia ni kivutio kikubwa ambacho kama kitatangazwa vizuri, kitaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni. Mkuu huyo wa Kanda anasema: “Kwa mwaka 2016, zilipatikana Dola za Marekani 60,000 na mwaka 2017, mapato yalishuka kidogo ambapo zilipatikana dola 48,000 tunategemea kwa mwaka huu mapato yataongezeka na tutafikia Dola 70,000 kutokana na watalii kuongezeka.”

Kwa mujibu wa Ngimilanga, utalii huu ukitangazwa vizuri na kupata wageni wengi, utakuwa chanzo kizuri cha mapato. Anakwenda mbali na kubainisha kuwa, aina hii ya utalii haisababishi uharibifu wa mazingira na wala kuathiri samaki hao kwa kuwa wanavuliwa tu na kurudishwa ndani ya maji baada ya kupimwa. Anasema kutokana na kuongezeka kwa watalii, juhudi za kuboresha maeneo ya uvuvi zinazidi kufanyika ili kuvutia wageni wengi zaidi.

“Utalii huu kupitia tiger fish ukitumika vizuri, utaisaidia serikali kuongeza mapato yake kwani watalii wataongezeka,” anasema.

Hata hivyo anasema, tofauti na uvuvi wa kitalii katika kanda hiyo, pia zipo shughuli nyingine za uwindaji wa kitalii. Kwamba, mwaka 2016 walipata wageni 57 waliowinda wanyama mbalimbali 377 na fedha zilizopatika zinazojumuisha malipo vibari, wanyama na malipo mbalimbali zilikuwa Dola za Marekani 435,170.

Mwaka 2017 walipata wageni 54 waliowinda wanyama 310. Fedha zilizopatikana ni Dola 348,970 na mwaka 2018 walipata wageni 46 waliowinda wanyama 355 na kupatikana Dola 380,330. Takwimu za mwaka 2019 bado zinaandaliwa. Mintarafu madai ya baadhi ya watu kuwa baadhi ya wageni wamekuwa wakiondoka na wanyama zaidi tofauti na idadi inayoruhusiwa katika vibali vyao, anasema upo utaratibu mzuri kuhakikisha hilo halifanyiki.

Anasema, katika uwindaji wa kitalii mgeni anapokuja kutoka Ulaya na Marekani au kwingine kokote, kampuni inayohusika na kuwinda ndiyo humpokea mgeni na kuhakikisha anakaguliwa vibali vyote na kama ana silaha na vibali kulipiwa kadiri ya mahitaji ya aina ya kibali.

“Wanapoenda kuwinda, wanakuwa wa watu maalumu ambao ni wataalamu wanaowaongoza. Kazi yao hao, ni kutambua aina ya mnyama na ‘size’ ya mnyama na maeneo ambayo mnyama anatakiwa kupigwa… Kila mnyama anayewindwa anarekodiwa,” anasema.

Anasema baada ya kuwinda wanyama, kampuni husika ndizo hutambua mahitaji mengine ya mwindaji na wawindaji hao hubeba jukumu la kumuandalia mgeni vibali na mahitaji mengine.

“Baada ya hapo zinapelekwa ofisini, zinakaguliwa na kuandikiwa kibali cha kumiliki. Kisha, zinasafiorishwa hadi makao makuu ya kampuni na wakaguzi kutoka mamlaka ya wanyama pori Tanzania inakwenda kukagua.”

“Baada ya kujiridhisha, taasisi nyingine za ukaguzi au udhibiti zikiwemo za uhamiaji, mamlaka ya anga, taasisi zinazohusika na haki za wanyama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Anga na taasisi nyingine nyingi ambapo anasema kuwa si rahisi mtu kusafirisha nyara zaidi ya kibali chake.

Changamoto katika pori hilo, Mkuu wa Kanda anasema, wakati mwingine matamko yasiyo ya kizalendo ya baadhi ya wanasiasa yanawafanya watalii kusita, lakini juhudi zinazofanywa na mamlaka mbalimbali kusema na kueleza ukweli, zinawafanya wageni kutambua hali halisi na hivyo, kuendelea kutembelea vivutio hivyo.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, changamoto nyingine ni pamoja na kuwapo kwa vijiji 11 vilivyo jirani sana na hifadhi hiyo, jambo linalosababisha kuwepo kwa ujangili. Ngimilanga anasema changamoto nyingine ni miundombinu ya barabara kwani wakati mwingine imekuwa haipitiki katika kipindi cha masika.

SEKTA ya ubunifu (sanaa) na uchumi ...

foto
Mwandishi: Agnes Haule

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi