loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bilioni 2/- kujenga Chuo cha Mipango Mwanza

SERIKALI imetoa Sh bilioni 2.1 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Dodoma, Kampasi ya Mwanza, ambacho kitajengwa Kijiji cha Katumba Kata ya Kisesa wilayani Magu.

Hayo yamesemwa jana wilayani hapa na Kamishina Msaidizi wa Bajeti, Pius Mponzi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James wakati wa hafla ya kukabidhi rasmi kiwanja Namba 1 chenye ukubwa wa hekta 8.3 sawa na ekari 21 kitalu “C’ na Kitumba ‘A’. Kiwanja hicho kimetolewa bure na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Filemoni Sengati, Mkurugenzi Mtendaji Lutengano Mwalibwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elisha Hilali walikabidhi kiwanja hicho kwa uongozi wa chuo hicho.

Hafla hiyo ilishuhudiwa na viongozi wa Kijiji cha Katumba, wa Kata ya Kisasa na wakazi wa maeneo hayo. Mponzi alisema tayari serikali imetoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo katika kijiji hicho cha Katumba, ambacho kitachochea mwamko wa jamii wa kusomesha watoto wao kuanzia elimu ya msingi hadi ya chuo kikuu na pia kitaongeza fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi na taifa.

“Naupongeza sana uongozi wa wilaya ya Magu kwa kutoa eneo hili bure kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki, kama wangekuwa watu wenye mawazo finyu wangekataa,” alisema.

Fedha hizo zilizotolewa na serikali zitatumika kujenga kumbi mbili za mihadhara ya chuo katika mwaka huu wa fedha 2019/20, zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 610 kila moja, jengo moja lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 430, darasa lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 180, ofisi 10 na vyoo vinne. Alisema uongozi wa wilaya ya Magu, umeithibitishia serikali kuwa ina maono mapana ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

“Mmetambua hilo kwa sababu chuo hiki si mali ya Chuo cha Mipango peke yao, ni mali yenu, kitakuwa hapa milele na kitanufaisha watoto wenu,” aliongeza.

Aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kutoa ekari 21 bure kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na kusisitiza kuwa ujenzi utaanza mara moja. Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Hozen Mayaya aliishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho, ambacho manufaa yake ni makubwa kwa nchi.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk Filemoni Sengati aliishukuru serikali kwa kutoa fedha na kuwezesha kufanyika kwa uwekezaji huo mkubwa kwenye sekta ya elimu ya juu wilayani kwake.

Alisema yeye kwa kushirikiana na viongozi wenzake, watahakikisha chuo hicho kinakamilika kujengwa na kutoa fursa kwa vijana wengi kupata elimu. Alisema chuo hicho kitachochea ongezeko la uchumi.

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Mwanza

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi