loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba, Yanga viwango tofauti, tabu ileile

MSIMU wa 2019/2020 unaweza kusema ni furaha kwa wekundu wa Msimbazi, Simba kwa sababu wametimiza baadhi ya mambo yao huku Yanga ikiendelea kutaabika kwa kila kitu.

Ukiachilia mbali kuongoza katika msimamo wa ligi, Simba imemaliza ujenzi wa awamu ya kwanza ya uwanja wao wa mazoezi uliopo Bunju unaofahamika kwa jina la Mo Simba Arena.

Hilo ni jambo zuri na la kupongezwa baada ya kukaa miaka 83 bila kuwa na uwanja wake. Simba ya sasa si ile ya zamani, inajivunia uwekezaji wake chini ya Mohamed Dewji ambapo kwa sasa huwezi kusikia wachezaji wanalia njaa au ucheleweshaji wa mishahara kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Pia, timu hiyo wanajaribu kujiendesha kisasa baada ya kubadilisha mfumo na kuingia kwenye kampuni. Hilo linajionesha wazi kutokana na namna wanavyopangilia mambo yao kuanzia kwenye kuajiri.

Kwa sasa huwezi kulinganisha Simba na Yanga zimetofautiana kuanzia ubora, uwekezaji na mfumo. Simba ya sasa ina uwezo wa kusajili mchezaji yeyote wanayemtaka, changamoto iliyopo kwao ni namna wanavyosajili na kushindwa kupata wachezaji wanaostahili. Kingine uswahili mwingi kila mtu ana mchezaji wake wa kumsajili kwa ajili ya kupata ile asilimia 10 na hayo yanaweza kuwa hatari kwao.

Sababu kubwa iliyonifanya nione kuna uswahili ni namna Kocha aliyetimuliwa Patrick Aussems aliwahi kusema kuwa kuna wachezaji aliwapendekeza kwa ajili ya kusajiliwa kabla ya kuanza kwa msimu huu lakini alivyorudi kutoka likizo alikuta mambo tofauti.

Kati ya wachezaji sita au saba aliowahitaji alimkuta mmoja tu. Sasa inaonesha ni kwa namna gani mambo hayakuwa sawa. Matokeo yake ya sasa timu yao ikashindwa kufanya kile kitu ambacho walikitarajia kisha mzigo wa lawama wakamwachia kocha wao.

Inawezekana kabisa kocha huyo alikuwa na makosa mengine kama ya nidhamu lakini kwa upande wa kiwango cha timu hakika wanaweza kulaumiana wote. Bado licha ya wekundu hao kuonekana hawachezi katika kiwango kinachohitajika, unaweza kusema ni miongoni mwa timu zilizoonesha jitihada katika mechi zao kadhaa zilizopita za ligi.

Ukilinganisha na Yanga, kiwango ni tofauti. Simba ina wachezaji wengi wazuri na kikosi kipana tofauti na watani zao kuna baadhi ya wazuri lakini kuna muda wakifanya mabadiliko mambo yanazidi kuwa magumu badala ya kuwa mazuri.

Utofauti wa Yanga kwa Simba ni kwamba, Yanga bado wanaendelea kulia njaa, kwa sababu wanakabiliwa na ukata. Si kwamba umeanza sasa hata kidogo bali tangu kuondoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wao wa zamani, Yusuf Manji. Yanga ina madeni kibao na kuna wakati wachezaji wanaliamsha wakiwa hawajalipwa mishahara. Ushahidi ni taarifa za hivi karibuni kuwa baadhi ya wachezaji kama Sadney Urikhob, Lamine Moro na Juma Balinya kuandika barua na kuomba kuvunja mkataba kwa sababu hawakulipwa mishahara ya miezi miwili.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla anathibitisha ni kweli wanaelemewa na mzigo wa madeni na kutaja zaidi ya Sh bilioni mbili huku akisema madeni mengine aliyakuta. Hayo yote yanadhihirisha ni namna gani timu hizi mbili kwa sasa zinazungumza habari tofauti. Mwingine anacheka na mwingine analia hapo ndipo utofauti ulipo. Tabu ile ile Simba ilikuwa inataabika kupata matokeo mazuri katika baadhi ya mechi sawa na Yanga, licha ya wote kutamba kuwa walisajili wachezaji wazuri. Kingine fukuza ya makocha.

Yanga ilianza kumtimua Kocha aliyekuwepo Mwinyi Zahera kisha Simba wakafuata na kuachana na Patrick Aussems. Isipokuwa sababu za kuwatimua makocha zinatofautiana kiasi lakini mengi ni yale yale tu na zaidi wakigusia kiwango cha uwanjani. Wekundu hao licha ya wachezaji wake kulipwa vizuri na kwa wakati tabu ipo kwenye suala la nidhamu.

Wachezaji, baadhi yao hulewa, kuchelewa mazoezini, limekuwa likiwasumbua labda ni kutokana na jinsi walivyokuwa wanalelewa. Tabu nyingine iliyopo kwa timu hizi. Ni viongozi kuwaingilia benchi la ufundi na kuwapangia.

Tatizo lililopo kwenye timu hizo kila mtu anajua na ni Kocha, akiona mchezaji fulani hajapangwa au ni mchezaji wake wanaingilia na kumpangia kocha ambaye hukaa na wachezaji mazoezini. Kwa mfano, Zahera wakati anaondoka Yanga alikiri kuingiliwa kwenye maamuzi yake na hata kwa upande wa Simba, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alikiri kuwa kuna muda walikuwa wanamshauri kocha apange wachezaji fulani.

Kwa kauli hizo inaonesha dhahiri bado benchi la ufundi linaingiliwa, kitendo ambacho ni lazima kitaleta mgongano kwa sababu kocha ana wachezaji wake na viongozi wana wachezaji wao. Jambo lingine ni namna mashabiki wa klabu hizo wanavyokosa uvumilivu. Yaani wanataka kuona Simba au Yanga inashinda mechi zote kitu ambacho kinaweza kuwezekana au kisiwezekane.

Mashabiki wa timu hizo ni wa ajabu wanadhani wao ni bora kuliko wengine. Timu zao zikifungwa na klabu ndogo basi wanalalamika kana kwamba wameonewa wakati mchezo unachezwa uwanjani dakika 90.

Ni watu wa kwanza kuwanyooshea vidole makocha na viongozi wao kwa sababu wamepoteza mechi moja na kupata sare moja pengine. Hawaamini mpira ni mchezo wa makosa ukikosea mwenzako anakuadhibu.

Halafu imani yao kubwa mmoja akifungwa ndio furaha yao mwaka mzima, baada ya hapo mengine ndio yaendelee. Kama timu hizi zimeamua kujiendesha kisasa, basi ni lazima wakubali kuacha mambo mengine na kukubali mabadiliko ya kweli ili kuleta ushindani mkubwa sio tu kwenye ligi bali michuano ya kimataifa.

MGOMBEA ubunge katika jimbo la Ilemela, Dk Angelina Mabula amesema ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi