loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ni vita ya England, Hispania Uefa

HATUA ya makundi ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imekamilika katikati ya wiki hii kwa timu 16 kutoka katika makundi manane kupenya hatua inayofuata. Kati ya timu hizo England imeingiza timu zake zote nne Liverpool, Chelsea, Manchester City na Tottenham.

Mbali na England, Hispania pia nayo imeingiza timu zake zote nne ambazo ni Real Madrid, Athletico Madrid, Valencia na FC Barcelona. Mabingwa wa Ligi Kuu Ufaransa, PSG waliokuwa kundi A wametinga hatua hii baada ya kushinda mechi tano na sare moja huku wakiwa wamefunga mabao 17 na kuruhusu kufungwa mawili.

Real Madrid waliokuwa kundi hili nao wamepita baada ya kushika nafasi ya pili. Mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich waliokuwa Kundi B, wakipata ushindi katika mechi zao zote sita, wakifunga mabao 24 na kuwafanya kuwa timu pekee iliyopata matokeo mazuri kwenye hatua ya makundi, imetinga 16 bora sambamba na Tottenham ambao msimu uliopita walishindwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kukubali kufungwa na Liverpool katika fainali.

Mabingwa wa Ligi Kuu England Manchester City, waliokuwa Kundi C baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wao wa mwisho na Shakhtar Donetsk imewafanya waingie hatua hii wakiwa vinara wa kundi wakifuatiwa na Atlanta waliopata ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Shakhtar katika mchezo wa mwisho. Kundi D limepitisha mabingwa wa Ligi Kuu Italia Juventus na Atletico Madrid, ambapo Kundi E mabingwa watetezi Liverpool na Napoli wakipenya.

FC Barcelona mabingwa wa Ligi Kuu Hispania wamefuzu baada ya kuwa vinara wa Kundi F ikiwa hii ni mara yao ya 13 mfululizo, wameambatana na Borussia Dortmund. Kundi hili limeshuhudia vigogo kutoka Italia, Inter Milan wakishindwa kufuzu hatua ya 16 baada ya kumaliza nafasi ya tatu na kujikuta wakiangukia Europa League. Kundi G timu ya RB Leipzig na Lyon ndizo zilizosonga mbele huku Benfica pamoja na Zenit St Petersburg zikigonga mwamba.

Vinara wa Kundi H, Valencia ambao kwenye mchezo wao wa mwisho waliibuka na ushindi wa 1-0 mbele ya Ajax, Chelsea walioshika nafasi ya pili walioshinda 2-1 mbele ya Lille ndio waliosonga mbele. Baada ya timu 16 kupatikana kinachosubiriwa ni upangwaji wa ratiba na kujua ni timu gani zitakutana ili kupata timu nane zitakazoingia robo fainali kisha nne kucheza nusu fainali na mbili kucheza fainali ili kumpata bingwa.

Michuano ya mwaka huu ni ya 65 tangu ilipoanzishwa lakini ni ya 28 tangu ilipobadilishwa mfumo na jina kutoka kuitwa European Champion Clubs’ Cup (Kombe la klabu bingwa Ulaya) na kuitwa UEFA Champions League (Ligia ya Mabingwa Ulaya).

Mchezo wa fainali unatarajiwa kupigwa katika uwanja wa Ataturk Olympic, Istanbul Uturuki. Ratiba ya hatua ya 16 bora inatarajiwa kupangwa keshokutwa mjini Nyon, Uswisi saa 8 mchana kwa saa za Afrika Mashariki na kuna uwezekano mkubwa wa timu za England kukutana na za Hisapnaia.

Kuna uwezekano mkubwa Chelsea kupangwa na Barcelona, hii inakuja kutokana na kwamba wakati wa upangwaji timu zilizoingia 16 bora hugawanywa katika makundi mawili ambapo timu zilizoongoza makundi zitakutana na timu zilizoshika nafasi ya pili. Utaratibu mwingine uliopangwa na Uefa ni kwamba timu za nchi moja na zilizokuwa katika kundi moja hazipangwi kukutana.

Hesabu zinaonesha Chelsea kuwa na asilimia kubwa ya kupangwa na Barcelona mbali ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi lakini pia hawawezi kukutana na Valencia kwasababu walikuwa kundi moja na pia hawawezi kukutana na Liverpool au Man City kwakuwa wanatoka nchi moja. Mabingwa watetezi Liverpool na Manchester City mmoja wao anatarajiwa kupangiwa na kama si Real Madrid basi Atletico Madrid.

Man City ambao vinara wa kundi lao hawawezi kukutana na Tottenham, Chelsea au Atalanta, hivyo kunawafanya nao wawe na uwezekano wa kukutana na Real Madrid au Atletico Madrid. Hali kama hiyo itawakuta Liverpool ambao kuna uwezekano mkubwa wa kwenda Madrid na hawawezi kukutana na Tottenham, Chelsea au Napoli. Msimu wa mwaka 2017/18 Barcelona waliwafunga Chelsea katika hatua kama hii kwa jumla ya mabao 4-1, lakini Chelsea nao wana kumbukumbu nzuri ya kuwatoa Barcelona katika nusu fainali mwaka 2012.

Tottenham, kama watanusurika kupangwa na Barcelona, Juventus, PSG basi itaangukia kwa Valencia. Kwakuwa Tottenham ilikuwa kundi moja na Bayern hivyo haiwezi kukutana nayo wala Man City kwakuwa zinatoka nchi moja hivyo inaweza kukutana na Valencia au Barcelona. Huu ndio msimu pekee katika historia ya michuano hii kupitisha timu pekee kutoka mataifa ya England, Ufaransa, Hispania, Italia na Ujerumani. Kuna timu nne kutoka England, nne zingine Hispania, tatu Ujerumani, tatu Italia na mbili Ufaransa.

NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania rasmi ametolewa kwa mkopo ...

foto
Mwandishi: NYON, Switzerland

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi