loader
Picha

Magufuli- Tutawashinda wenye hila

RAIS John Magufuli amesema Watanzania wataendelea kushinda hila na majaribio yote yanayolenga kukwamisha maendeleo yao, kama ilivyotokea kwa ndege mpya iliyokuwa inashikiliwa nchini Canada.

Amesema hila hizo zimeshindwa na kwamba watanzania wataendelea kuwa kidedea katika kutafuta haki na maslahi yao.

Rais amesema hayo jana jijini Mwanza wakati wa kupokea ndege mpya ya nane aina ya Bombardier Dash 8 Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 78 na tani 1.6 ya mizigo tofauti na ndege za awali aina hiyo hiyo zenye uwezo wa kubeba abiria 76 tu.

Ndege hiyo ilitua kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mwanza jana saa 1:15 usiku ikitokea nchini Canada. Kabla ya kutua Mwanza, ndege hiyo ilipotoka Toronto, Canada ilipitia kwenye nchi kadhaa ikiwemo Iceland, Jamhuri ya Czech, Misri na Addis Ababa nchini Ethiopia.

Rais Magufuli amesema ndege hiyo ilipangwa kuwasili hapa nchini mwezi uliopita lakini baadhi ya watu wenye nia mbaya na Tanzania walifungua kesi nchini Canada iliyosababisha ndege hiyo kuzuiwa.

Alisema jitihada zilizofanywa na serikali zilisaidia ndege hiyo kuachiwa na ujio wa ndege hiyo ni ishara kuwa Mungu yupo pamoja na watanzania na kila hila dhidi ya watanzania haitafanikiwa.

Kutokana na ushindi huo, aliwataka watanzania kutembea kifua mbele kutokana na kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya 11 kwa fedha zao wenyewe.

Alisema kwa muda mrefu watanzania walikuwa wanapuuzwa na kujiona wanyonge, lakini kwa sasa hawanabudi kutembea kifua mbele kwa kuwa nchi inaenda vizuri na uchumi unakua.

Magufuli alisema ununuaji wa ndege hizo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 ambayo pamoja na mambo mengine iliitaka serikali kuifufua Kampuni ya Ndege nchini (ATCL).

Aliwataka ATCL kuzitunza ndege hizo na wasizikwaruze, kuboresha huduma zao pamoja na kuwa macho dhidi ya hujuma kutoka ndani na nje kwani biashara ya usafiri wa anga ina ushindani mkubwa.

Aliwataka watumishi wa ATCL kutotetereka na vita wanayopigwa ikiwemo kuambiwa wana maumbile mabaya na sare zao za kazi ni mbaya.

“Tuliahidi kuimarisha usafiri wa anga kwa kuifufua ATCL, tumenunua ndege mpya kumi na moja zikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner mbili, Airbus A220-300 nne na Bombardier Dash 8 Q400 tano, ndege nane zimeshawasili hapa nchini, Bombardier nyingine itakuja Mwezi Juni mwakani na Airbus mbili zitakuja Juni na Julai 2021,” alieleza Rais Magufuli.

Aliwataka ATCL kuendelea kuimarisha kitengo cha rasilimali watu wakiwemo marubani, wahandisi na wahudumu na kuongeza kuwa ndege hiyo ya jana iliendeshwa na marubani wawili Watanzania kutoka Canada hadi Mwanza akiwemo Kepteni Komba na Kepteni Hamza jambo ambalo limesaidia kuokoa Dola za Marekani 40,000 sawa na Sh milioni 90 ambazo zingetumika kuwalipa marubani wa kigeni kuzileta ndege hizo.

Kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na marubani hao wawili na mhandisi mmoja, Rais Magufuli aliziagiza mamlaka husika kuwazawadia Sh milioni mbili kila mmoja, lakini pia akaipongeza ATCL kwa kuajiri jumla ya watumishi 521 katika vitengo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Rais, usafiri wa anga duniani ni muhimu na kwa takwimu za Benki ya Dunia mwaka 2018, watu bilioni 4.34 walisafiri kwa ndege, lakini pia ripoti zingine za kimataifa zinaonesha kuwa bidhaa za tani milioni 63.7 zenye thamani ya Dola za Marekani trilioni 6 sawa na asilimia 35 ya biashara yote duniani zilisafirishwa kwa usafiri wa anga.

Mbali na watu na bidhaa hizo, alisema kwa mujibu wa Shirika la Utalii Duniani, asilimia 70 ya watalii wanatumia usafiri wa anga.

Kwa kuwa asilimia 40 ya wateja wa ATCL wanatoka Kanda ya Ziwa, Magufuli alisema serikali inajenga jengo la kutunza baridi katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Songwe pamoja na kuliboresha jengo la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA).

Alisema mpango wa serikali kwa siku za hivi karibuni ni kununua ndege ya mizigo kwa ajili ya kusafirisha bidhaa mbalimbali yakiwemo maua, minofu ya samaki na nyama itakayokuwa inasafirishwa nje ya nchi.

Mbali na majengo hayo, pia alisema aliongea na Rais, Paul Kagame wa Rwanda ili ndege kutoka Kigali ziwe zinapitia Kiwanja cha Ndege cha Mwanza na kisha kwenda Ulaya na nchi zingine jambo ambalo litaondoa ulazima wa baadhi ya abiria kupitia Dar es Salaam kama ilivyo sasa.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alitoa ‘ofa’ kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM waliokuwepo Mwanza kusafiri na ndege hiyo bure kwenda Dar es Salaam ili wafurahie matunda ya utekelezaji wa Ilani yao ya Uchaguzi.

ATCL wazungumza

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema kuwa ATCL inasafirisha abiria 1,000 kwa siku kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza hivyo kufanya asilimia 40 ya wasafiri wa soko la ndani.

Matindi alisema mipango yao kwa sasa ni kuzifanya ndege za Airbus A220-300 kufanya safari za Mwanza mara nne kwa siku, Bombardier Dash 8 Q400 mara sita ili kukidhi mahitaji ya Mwanza.

Alisema kwa sasa ATCL inamiliki asilimia 73 ya soko la ndani lakini malengo yao ni kufikia asilimia 75 katika kipindi kifupi kijacho.

Alisema ATCL ilikuwa inasafirisha abiria 4,000 kwa mwezi mwaka 2016 lakini kwa sasa inasafirisha abiria 62,000 kwa mwezi, huku ikisafirisha tani tisa za mizigo mwaka 2016 lakini kwa sasa inasafirisha tani 177 za mizigo.

Kuhusu safiri za Guangzhou nchini China, alisema zitaanza mwezi Februari mwakani na zitafuatia safari za Kinshasa na Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa Matindi, ATCL imeajiri jumla ya wafanyakazi 521 wakiwemo marubani 94 ikilinganishwa na marubani 11 waliokuwepo mwaka 2016, wahindisi 127 na wahudumu wa ndani ya ndege 125. Balozi wa Canada Balozi wa Canada hapa nchini, Pamela O’Donnel, alisema uhusiano mzuri uliopo kati ya Canada na Tanzania tangu miaka ya 1970 unatokana na msukumo wa maendeleo ya watu na kupunguza umasikini.

Alisema Tanzania na Canada zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya uchukuzi kwa miaka 40 sasa na katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania imeweza kununua ndege sita zilizotengenezwa Canada.

Alisema anaamini ushirikiano huo wa Tanzania na Canada utaendelea kudumu.

Mawaziri Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema vitendo vya hujuma vya baadhi ya watu vya kutaka kuharibu maendeleo ya Tanzania vimeshindwa kutokana na ndege hiyo kuachiwa na kuwasili jana jijini Mwanza.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kitendo cha ndege hiyo kuwasili nchini jana kimewafanya wanyang’anyi kutapatapa kwa kitendo chao cha kuvizia ndege za Tanzania na kuzikamata nje ya nchi.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi