loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

RIPOTI MAALUM-1: Watanzania wanavyozama biashara ya ukahaba India

MTAZAMO wa kurahisisha upatikanaji riziki na kipato kikubwa kwa muda mfupi, umewatumbukiza vijana wa kike wa Kitanzania kwenye biashara ya ukahaba katika miji mikubwa ya India, gazeti hili limebaini.

Taarifa za uhakika na ushuhuda mbalimbali, zinaonesha biashara hiyo kufanyika zaidi katika miji ya Delhi, Mumbai na Bangalore, wahusika hao wakielekeza soko lao zaidi katika maeneo ya starehe na klabu za usiku.

Ni sura nyingine ya kashfa ambayo gazeti hili linabaini, huku awali kulishatolewa taarifa mwaka 2016 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya kuwepo Watanzania wanaokadiriwa kuwa 500, wanaojihusisha na ukahaba India.

Baadaye 2017, taarifa nyingine ya wizara hiyo, ilionesha idadi hiyo ikipungua na kufikia 300.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo, Emmanuel Buholela, raia wa Tanzania wanaohusishwa na biashara hiyo, wanapatikana katika majiji makubwa ikiongozwa na New Delhi kisha kufuatiwa na majiji ya Bangalore, Mumbai, Hyderabad, Goa na Uttar Pradesh.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili nchini humo hivi karibuni, umebaini fikra kuu za wahusika wa biashara hiyo ni kupata utajiri wa haraka, lakini tofauti na matarajio yao, wamekuwa wakitumbukia katika biashara ya ukahaba na ukatili wa kijinsia.

Mabinti wa kitanzania waliozungumza na gazeti hili nchini India, wamedai kuwa walipelekwa katika nchi hiyo ya Bara la Asia, kwa ahadi ya kutafutiwa kazi nzuri, lakini walipofika walijikuta wakijiingiza katika biashara hiyo haramu kutokana na hali ngumu ya kimaisha.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini mabinti wengi waliopelekwa India kufanyishwa biashara hiyo, wanashindwa kurejea nchini kutokana na mabosi wao hao, kuwanyang’anya pasipoti ikiwa ni mbinu ya kuwadhibiti wasitoroke.

Gazeti hili pia limebaini kuwa mabinti hao hawapewi nafasi za kufanya mawasiliano na wananyimwa haki zao nyingine za msingi ikiwemo ya kuabudu.

Pia, imebainika viongozi wa biashara hiyo, huchukua mabinti wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 24 na wachache walio chini ya umri huo, wakiwalaghai kuna fursa katika sekta ya filamu na ajira kwenye hoteli, migahawa, maduka makubwa na kazi za nyumbani.

Viongozi wa makundi hayo, pia huwapa mabinti hao ofa za kuwatafutia pasipoti na tiketi za ndege ili kuwawezesha kufika India.

Amina (si jina halisi), mzaliwa wa Shinyanga, alizungumza na gazeti hili katika mji mdogo wa Chattarpur Aprili mwaka huu na kubainisha kuwa alianza kujihusisha na ukahaba akiwa kidato cha nne mjini Shinyanga miaka minne iliyopita.

“Maisha yangu yalikuwa magumu kipindi ninaishi na bibi yangu, nilianza kufanya shughuli hizi nikiwa kidato cha nne mwaka 2015.

“Nakumbuka nikiwa Geita Mjini, kaka mmoja aliyekuwa anatuunganishia wanaume wanaotoka kwenye mji huo, alitueleza kwamba kulikuwa na kazi India na kama tungekuwa tayari angetuunganisha na wahusika,” alisema Amina.

Aliendelea kusimulia kuwa baada ya kuipokea ofa hiyo kwa mikono miwili, wahusika waliwasaidia kupata hati za kusafiria na vibali vingine na safari ikaanza kuelekea Delhi, India kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

“Nilishawishika na kukubali lakini nilipofika India, nilikuta hali tofauti. Kwanza waliponipokea palepale uwanja wa ndege waliniambia niwape pasipoti yangu wakidai itawasaidia kukamilisha taratibu za mahali pa kufikia.

“Niliwapa na tukaanza safari kuelekea Chattarpur, si mbali na uwanja wa ndege. Tulipofika, kwa kweli mazingira sikuyaelewa, lakini nilijipa moyo kuwa pengine kuna maeneo mazuri wangenipeleka, nikiamini hawawezi kutumia gharama nyingi kunisafirisha kutoka Tanzania kisha kunipeleka kwenye eneo lisiloeleweka.

“Baada ya kukaa kwa saa mbili hivi, niliamua kuwauliza juu ya sehemu ambayo ningefikia, na ndipo nilipoambiwa habari mbaya kwamba hapa ndipo nimeshafika na hakuna sehemu nyingine.

“Sikujua kama ndiyo kwanza nimefika, niliwekwa kwenye eneo lenye harufu kali ya sigara, uchafu ndani ya nyumba, mandhari ambayo ni mabaya kuliko hata ya kule kwetu Shinyanga,” alieleza.

Aliongeza, “Baadaye nikawekwa chini na kuelezwa utaratibu mzima wa kile kilichonifikisha hapa India kwamba ni biashara hii. Na baadaye alikuja mtu na kunieleza kuwa ninadaiwa dola 2,000 (zaidi ya shilingi milioni nne) na kwamba nikizilipa watanirudishia pasipoti yangu, lakini sikuwa na fedha.

“Na kadri siku zilivyozidi kwenda, mtu yule yule alipandisha madai na kusema kuwa ninatakiwa kulipa dola 4,000 (zaidi ya shilingi milioni nane). Kwa kweli, sikutegemea na maisha yakawa ya taabu lakini nikajiuliza 'narudi vipi Tanzania, sina fedha?'.

“Nilipambana na mpaka sasa (Aprili mwaka huu) ni kama niko kizuizini kwani siwezi kuwasiliana na Mtanzania yeyote kwa simu na pia sipati huduma bora za afya ninapoumwa, hata chakula sipati kinachonitosheleza kwani ninapotoa huduma hizi huwa kuna mtu ambaye ndiyo anayepokea fedha, mimi huku ninatumika tu,” alisema.

Binti mwingine wa kitanzania aliyejitambulisha kwa jina moja la Gaudencia (33), aliliambia gazeti hili mjini Delhi kwamba amekuwa akifanya biashara ya ukahaba katika miji mbalimbali ya India tangu mwaka 2016, lakini hajafanikiwa kupata fedha nyingi kama alivyotarajia.

“Nilitoka Arusha mwaka 2016, nikaenda Mumbai, huko niliambiwa kuna mastaa wengi wanaopenda mabinti wenye asili ya kiafrika ili kucheza filamu.

“Aliyenipeleka ni kaka mmoja raia wa Nigeria ambaye alidai ana kampuni inayotafuta wacheza filamu kwenye maeneo mbalimbali duniani na kuwapeleka kwa kampuni mbalimbali zinazofanya shughuli za filamu hapa India.

“Walinilipia nauli na nilifikia jijini Mumbai kwenye hoteli nzuri siku ya kwanza, siku mbili baadaye alinihamishia kwenye nyumba ambayo nilikuta mabinti wengi wakiishi, sikujua kama biashara ni ya kujiuza lakini nililibaini suala hilo siku za mwanzo kabisa maana usiku ikiingia, baadhi ya mabinti hao waliondoka na wengine kutorudi usiku huo na ndipo nilipomuuliza mmoja wao akaniambia neno moja tu 'jiongeze’.

“Dada mmoja nilimuuliza na akanieleza kazi inayofanyika pale, nilichukia sana lakini tayari nilikuwa nimeshaingia kwenye mtego huo.

“Siku iliyofuata, nikiwa kwenye jengo hilo, nilikutana na mwanamke mmoja wa kitanzania ambaye aliniambia kuwa mwenye eneo hilo ana biashara kama hiyo New Delhi na kama ningekuwa tayari, ningeenda naye huko siku hiyo hiyo maana alikuwa na safari ya kwenda huko.

“Huko ndiko nilikokutana na Watanzania wengi na kugundua kuwa wengi walifika bila ya kujua wanakuja hapa kufanya nini na wengine sasa wamekuwa wabobezi wa shughuli hizi.

“Kwa kuwa nilikuwa tayari nimekwama, sikuwa na jinsi, nilianza kupambana na mpaka leo sijafanikiwa kupata fedha ya kutosha nauli na taratibu zote za kwenda nyumbani Tanzania.

“Mwaka 2017 niliugua sana, na bahati mbaya nikawa sipati huduma ya hospitalini, nililishiwa dawa, lakini sikupewa nafasi ya kuwasiliana na ndugu zangu na hata kupatiwa matibabu na ikawa rahisi kwangu kushambuliwa na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza,” alisema.

Dalali anena

Gazeti hili lilizungumza na madalali wa biashara hiyo eneo la Chattarpur jijini Delhi, ambao walidai mabinti hurubuniwa kwa maelezo kuwa watapata maisha bora na watatengeneza fedha nyingi kuliko ajira za Tanzania.

“Kuna mitandao mikubwa ya ukahaba India, ukiwa na mabinti wako wanne, umekuwa tajiri, watakupa fedha nyingi na utatengeneza fedha ndiyo maana hii biashara imekuwa ngumu kudhibitiwa,” alisema.

Katika eneo hilo, gazeti hili lilibaini kuwa kutokana na eneo hilo kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu wa mataifa mbalimbali, madalali wa biashara hiyo hutumia mbinu ya kumchangamkia kwa kutaka kumsalimu na kumsaidia kila mtu anayefika eneo hilo, wakitaka kujua alikotoka na anachokitafuta.

“Ukiwa kwenye eneo hili, lazima tukuhoji na mara nyingi unapofika huku, wengi wanakuja kwa ajili ya kununua huduma kwa wanawake wanaojiuza hapa.

“Sisi tunakuwa tayari kumpeleka mtu kwa mabinti iwapo tutaafikiana juu ya malipo kwani na sisi hupata japo fedha kupitia kwenye madili kama hayo," alifafanua mmoja wa madalali hao.

Itaendelea kesho...

TAKRIBANI mifugo 12,000 katika vijiji ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck, aliyekuwa India

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi