loader
Picha

Chadema kuchangishana bilioni 15/-

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuanzia mwakani kila mwanachama atalipia ada ya uanachama ya Sh 2,500 kwa mwaka, badala ya Sh 1,000 ya sasa kama mkakati wa kujitegemea.

Kwa sasa chama hicho kinategemea ruzuku ya serikali pekee. Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe wakati akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema jijini Dar es Salaam jana.

Katika mkutano wa jana, ulizinduliwa mfumo wa kidijitali ujulikanao kama ‘Chadema Digital’. Mbowe alisema Chadema kinafanya mabadiliko ya katiba ili kuruhusu kuanzishwa kwa harambee ya kidijitali aliyoiita ‘Digital Fundraising’ ambapo kila mwanachama atachangia ada ya Sh 2,500 kupitia simu yake ya mkononi.

Mbowe alisema mfumo huo utakuwa na uwezo wa kukata ada hiyo moja kwa moja kutoka kwenye simu ya mwanachama au mwanachama anaweza kutuma mwenyewe kupitia simu yake.

“Chadema kina wanachama zaidi ya milioni 6.5, kila mmoja akichangia ada ya Sh 2,500 tutakusanya Sh bilioni 15 kwa mwaka badala ya kutegemea ruzuku ya Sh bilioni tatu ya serikali, tunataka kujitegemea,”alisema.

Mbali na hilo, alisema kuanzia mwakani watajenga chama chenye nidhamu, maadili na kuwawajibisha viongozi watakaoshindwa kutimiza majukumu yao. Alisema haiwezekani kuwa na viongozi wasiofanya vikao, hawana daftari la kumbukumbu ya wanachama na wasiojua idadi ya wanachama wao.

Kwa mujibu wa Mbowe, mabadiliko ya katiba yao pia yatahusu chama kuanza kufanya mikutano au vikao vyao kwa njia ya ‘video’ lakini pia watafanya kampeni za kidijitali ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi. Katika hatua nyingine, alisema kuwa Chadema kinachukizwa na barua wanazoandikiwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa kwa kuwa barua hizo zinawafanya wao kuwa kama chama cha utani au hawaielewi katiba yao.

Mpaka gazeti hili linaenda mitamboni jana, uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti taifa na makamu wake ulikuwa haujafanyika. Ulitarajiwa kufanyika saa 5:00 usiku na matokeo kutolewa saa 9:00 usiku wa kuamkia leo. Wakati Mbowe akielezea mikakati hiyo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa nchini visiwe na utukutu bali vifanye shughuli zao kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa, Katiba ya nchi na katiba zao.

Jaji Mutungi ambaye aliwakilishwa kwenye mkutano huo na Msaidizi wake, Sisty Nyahoza, alisema Ofisi ya Msajili ambayo ni mzazi na mlezi wa vyama, watakuwa wakali dhidi ya vyama vitukutu.

“Msajili katika jukumu lake la usajili anakuwa kama mzazi, anaposimamia vyama anakuwa kama mlezi, kwa hiyo hakuna mzazi au mlezi anayependa mtoto wake awe mtukutu, hivyo vyama vyote 19 vya siasa viheshimu sheria ya vyama vya siasa, katiba na kanuni ya vyama vyao, hatupendi watoto watukutu, mkiwa watukutu na sisi tutakuwa wakali, “alisema.

Maneno hayo ya Msaidizi wa Msajili yaliwafanya wajumbe wa mkutano mkuu kugonga meza kwa sauti ya juu. Hali kama hiyo ya kupigiwa kelele na kugongewa meza kwa sauti ya juu pia ilimkuta Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Ada-Tadea, John Shibuda. Shibuda alikuwa miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa waliopewa nafasi ya kutoa salamu katika mkutano huo.

Shibuda aliwaeleza wajumbe wa mkutano mkuu kwamba dhamira ya Rais John Magufuli ni kuendelea kuheshimu mfumo wa vyama vingi na hazuii vyama kufanya shughuli zao za kisiasa bali anachotaka kusiwepo na lugha ya kudhalilishana.

“Siamini kama Serikali ya Awamu ya Tano na Rais Magufuli wanadhamira ya kufuta mfumo wa vyama vingi, imani ya Rais Magufuli na chama chake ni kumsifu...,” alisema Shibuda kabla ya kukatizwa kwa kelele za meza zilizokuwa zikigongwa kwa sauti ya juu.

Baada kelele hizo, ndipo Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe aliposimama na kuingilia kati kelele hizo kwa kuwataka wajumbe kuwa na nidhamu hata kama mgeni wao aliwakosea, kauli hiyo iliungwa mkono na Shibuda. Katika hatua nyingine viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa nchini walipata nafasi ya kutoa salamu.

Miongoni mwa viongozi hao ni Fahmi Dovutwa wa Chama cha UPDP aliyesema kuwa Chadema ni tegemeo la mabadiliko katika uchaguzi mkuu ujao na kumuunga mkono Mbowe kwa kauli yake ya kutaka kuwe na maridhiano. “Tuko pamoja na Chadema katika kupigania demokrasia nchini, tunawatakia moyo wa kuvumiliana kwa matokeo yoyote ya uchaguzi mtakaoufanya leo (jana), katika zama hizi tunahitaji viongozi aina ya Mbowe,” alisema Katibu Mkuu wa CCK Renatus Muhabi.

Naye Mwakilishi wa Chama cha CUF, Abdul Kambaya alisema kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa hatokani na mashinikizo ya mitandao ya kijamii bali mahitaji yao na demokrasia ndiyo yatawapa kiongozi wanayemtaka. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Elizabeth Mhagama, aliwaeleza wajumbe hao kuwa wakifanya mabadiliko mazuri ya sera, uongozi mzuri, wawe na uhakika watafikia mabadiliko wanayoyataka.

Askofu Mkuu wa Moravian, Emmaus Mwamakula, aliwataka Chadema kuwa wavumilivu, wakomavu na wawajibikaji kwa maslahi ya wananchi wote kwa kuwa upinzani una wajibu wa kushiriki chaguzi zote huru na haki.

Naye Shehe Hamis Kundecha alisema ni wajibu wa chama cha siasa kusema pale wanapoona mambo hayaendi sawa. Kupitia teknolojia ya kidijiti, Tundu Lissu aliwaambia wajumbe hao kutoka Ubelgiji kuwa amepona na anajiandaa kurudi. Mkutano huo ulihudhuriwa na jumla ya wajumbe 1,080 kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

1 Comments

  • avatar
    Raphael mwaluko
    20/12/2019

    Hiyo pesa itakuwa inawanufaisha wao na matumbo yao

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi